July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kikwete, Lungu hawajui Tazara iko mahututi

Treni ya Tazara ikiwa katika safari zake za kawaida

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete na mwenzake wa Jamhuri ya Zambia, Edgar Lungu, wameahidi kushirikiana ili kuimarisha reli inayounganisha nchi hizi mbili (Tazara), ili kukuza biashara na uwekezaji.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana na mwenyeji wake, Rais Kikwete alisema, wakati umefika sasa wa kuifufua reli ya Tazara ambayo ni kiungo muhimu na alama kubwa ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Alisema, umuhimu wa reli hiyo ni wa kihistoria. Unahusisha nchi tatu za Tanzania, Zambia na China ambayo ndiyo iliyochangia ujenzi wake.

Alisema, “Upo umuhimu mkubwa wa kuifufua reli ya Tazara ili ifanye kazi kama awali. Hivyo tumezungumza namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili ikiwemo uendeshaji na ukarabati ili irejee katika hali yake ya awali.

“Nchi zetu mbili, zimekubaliana kuwekeza zaidi katika reli hiyo ikiwemo kuboresha uendeshaji na ukarabati wa miundo mbinu.”

Ukisikiliza maelezo haya ya Jakaya Kikwete, utaweza kugundua mara moja, kwamba hakuna kitakachofanyika. Reli haiyajengwa. Ukarabati hautafanyika na hivyo huduma hazitaboreshwa.

Hii ni kwa sababu, Rais Kikwete na pengine na mwenzake wa Zambia, hawafahamu matatizo ya Tazara.

Hili ni kwa sababu, yeyote mwenye dhamira ya kupatia ufumbuzi usafiri wa reli kati ya Tanzania hadi Zambia, hawezi kuita matatizo yaliyopo Tazara leo hii, kuwa ni changamoto. Tazara iko katika chumba cha wagonjwa mahututi; matatizo yake lazima yaitwe kwa jina lake halisi.

Tazara ya sasa, ni kama imekufa. Imeporomoka uzalishaji. Imeshindwa kufanya kazi kama ilivyokuwa imetarajiwa. Inashindwa kutoa huduma, huku migogoro kati ya wafanyakazi na menejementi ikizidi kuongezeka kila uchao.

Kisa: Washirika wa mradi huu – Tanzania na Zambia – wanategeana katika uwekezaji wa mtaji.

Tazara imeshindwa kuongeza uzalishaji kutokana na idadi ndogo ya vichwa vya treni, miundombinu chakavu na mazingira magumu ya kufanyia kazi. Nchi zote mbili zinalifahamu hili.

Rais Kikwete na mwenyeji wake – Edgar Lungu – wanajua kuwa serikali zao zingewekeza vya kutosha katika reli hii, kungepunguza kwa kiwango kikubwa gharama za usafirishaji wa mizigo na kungesukuma shughuli za kiuchumi.

Lakini badala ya kutoa kipaumbele kukabiliana na matatizo hayo, kila nchi imekuwa ikipunguza bajeti yake katika kuhudumia reli hii, mwaka hadi mwaka.

Tazara ilikuwa ikisafirisha tani za mizigo 1.2 milioni na abiria wasiopungua 1 milioni. Hivi sasa, inasafirisha tani na abiria wasiozidi 700,000.

Haikutarajiwa Kikwete na Lungu, wanaofahamu umuhimu wa kutumia reli, serikali zao ndiyo ziwe vinara wa kuihujumu. Duniani kote, usafiri wa treni ndio maarufu. Nchi kadhaa zimeshirikiana katika usafiri wa aina hii.

Mathalani, nchi za Ulaya zimeunda reli moja inayoitwa Eurostar inayotoa huduma kwa nchi mbalimbali. Moja ya safari ya reli hiyo, ni kutoka Uingereza, kupitia Ufaransa, Ubelgiji hadi Uholanzi.

Hivyo basi, ikiwa Kikwete na Lungu wanataka kwa dhati kufufua reli hii, wawekeze sasa. Waache ubinafsi.

Vinginevyo, kauli zao zitaishia kuwa porojo.

error: Content is protected !!