JAKAYA Mrisho Kikwete, Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania, amesema Taifa litamkumbuka mwanasiasa mkongwe nchini humo, Bakari Harith Mwapachu (81), kwa mchango wake alioutoa enzi za uhai wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)
Mwapachu aliyewahi kuwa waziri wa katiba na sheria, alifariki dunia alfajiri ya jana Ijumaa tarehe 12 Februari 2021, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Mwapachu aliyehudumu tangu serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne, amewahi kuwa mbunge wa Tanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kati ya mwaka 2000-2010, mwili wake utazikwa leo Jumamosi jijini Tanga.
Kikwete akiwa madarakani kati ya mwaka 2005 hadi 2015, alifanya kazi na Mwapachu ambapo, katika ukurasa wake wa Twitter, Kikwete amezungumzia kifo cha mwanasiasa huyo, aliyezaliwa tarehe 25 Julai 1939.

Akiambatanisha picha ya Mwapachu aliyopigwa enza za uhai wake katika moja ya matukio walipokutana, Kikwete ameandika “Innalillah Wainna Ilaihi Rajiun. Kwa heri kaka yangu Mhe. Bakari Mwapachu.”
“Daima tutakukumbuka kwa moyo wako wa upendo, huruma na ucheshi. Vilevile utakumbukwa kwa mema mengi uliyoifanyia nchi yetu na watu wake na kwa mchango muhimu uliotoa kwa ujenzi wa taifa letu,” amesema Kikwete
Rais huyo mstaafu amesema “poleni wanafamilia na ndugu zangu wote kwa msiba mkubwa uliowakuta. Ni msiba wetu sote. Tunawaombea kwa mola awape moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na kuomboleza.”
“Tuendelee kuomba kwa Mola amsamehe makosa na amjaalie pepo marehemu wetu. Ameen.”
Leave a comment