July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kikwete kumfukuza kazi Jaji Warioba

RAIS Jakaya Kikwete akisaini muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba uliopitishwa na Bunge wiki mbili zilizopita, atakuwa amefukuza kazi Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba
Jaji Warioba na Rais Kikwete

Jaji Warioba na Rais Kikwete

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete akisaini muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba uliopitishwa na Bunge wiki mbili zilizopita, atakuwa amefukuza kazi Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

MwanaHalisi Online limeelezwa kuwa kwa kitendo tu cha kusaini muswada huo, rais atakuwa amefanya kazi yote ya Tume, ya miezi 18 kuwa sifuri.

Hii ina maana nyingine, gazeti hili limeelezwa. “Juhudi zote za kupata Katiba zitakuwa zimefifia na hata kutoweka; na Katiba mpya haitapatikana.”

Yote haya yanatokana na muswada wa sheria ambao umepitishwa na bunge ambao unataja kuwa muda wa Tume ya Warioba utamalizika pale itakapowasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum la Katiba.

Hii ina maana kwamba, Tume kwa umoja wake, haitashiriki katika mjadala ndani ya Bunge la Katiba; hivyo kuna uwezekano mkubwa wa upotoshaji wa makusudi katika fasili ya vifungu mbalimbali vya rasimu kwa manufaa ya watu binafsi au vyama vya siasa.

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (2011), inatamka kuwa Tume itaendelea kuwa katika mchakato hadi baada ya kufanyika kwa kura ya maoni ya kupitisha au kukataa Katiba mpya.

Katika muswada ambao rais anatakiwa kusaini, kipengele hicho kinachotambua umuhimu wa Tume katika hatua zote – kwa kutoa ufafanuzi juu ya vipengele mbalimbali na sababu za kuviweka – kimeondolewa na muda wa Tume umefupishwa.

Hatua hii katika muswada inazua utata juu ya nani watatoa ufafanuzi wa kitaaluma pale utakapohitajika; na hasa ule unaolenga kueleza “moyo wa tume” katika kufikia hatua husika.

“Hapa ndipo rasimu ya Katiba itachakachuliwa. Watajitokeza wajuaji, kila mmoja na lake na hata kuingiza yasiyokuwemo, ili kufanikisha matakwa yao,” ameeleza mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye anadai kuwa “tayari mchakato umepotea njia.”

Akisisitiza kutotajwa jina, mbunge kuyo amesema, “Yote yameanza kuwa wazi kwa kuangalia idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba. Unaweza kusema tu kwamba karibu wote wanatoka chama changu na watang’ang’ania kuendesha kikao kwa manufaa yao.”

Iwapo Tume ya Warioba itatupwa nje mapema, na vikao vya Bunge la katiba kuendeshwa kwa ushauri wa ushabiki wa waliowengi, basi kazi ya Tume itakuwa imezikwa.

Kwa njia hii, kodi za wananchi zipatazo Sh. 67.888 bilioni, sawa asilimia 12 ya bajeti ya serikali ya mwaka mmoja, ambazo zimetumiwa na Tume, zitakuwa zimeyeyuka bure.

Tayari uwezekano wa rais kusaini muswada unaofuta Tume mapema, umetishia baadhi ya makamishena wake.

MwanaHalisi Online lina taarifa za baadhi ya makamishena ambao wanadaiwa kusema kuwa iwapo rais atasaini muswada huo, “…atakuwa ametufukuza kazi; tutajiuzulu bila kusubiri kuambiwa,” amekaririwa mmoja wa makamishena akisema.

Amesema kusainiwa kwa muswada ni kama kuwafukuza kazi kabla hawajapata “fursa ya kutetea rasimu waliyoandaa katika vikao muhimu na hata mikutano ya wazi.”

Taarifa zinasema karibu makamishena 10 wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wako mbioni kujiuzulu iwapo Muswada wa Sheria ya Marekebisho utasainiwa na rais.

Gazeti hili limeshindwa kumpata Jaji Warioba kueleza taarifa zilizozagaa mitaani kuwa baadhi ya wajumbe wake wamekasirishwa na hatua ya bunge kupitisha muswada wenye lengo la kukwamisha mchakato wa Katiba mpya.

Gazeti limewahoji makamishena watatu juu ya hatua ya kujiuzulu, ingawa wote hawakutaka majina yao yatajwe.

Mmoja wa makamishena alimwambia mwandishi, “Sikuingia humu kutafuta kazi. Nilijisikia nafanya kazi ya utume. Sasa kama kazi yenyewe inaharibiwa hatua za mwisho na kwa nia mbaya, sina sababu ya kubaki humu. Nitaharibu hadhi yangu.”

Amesema, “Mimi naogopa kuingiza nchi yangu kwenye machafuko. Ikiwa sheria hiyo itasainiwa na rais na kubaki kama ilivyo, nitajiuzulu. Sikubaliani na muswada unaotuzuia kwenda kwenye Bunge la Katiba kutetea rasimu.”

“Nilikula kiapo kwa sheria ya awali iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sheria hiyo iliekeleza kuwa kazi za Tume zitakoma baada ya rasimu kupigiwa kura ya maoni. Kuondoa rasimu mikononi mwa Tume mapema, kunaweza kusababisha uchakachuaji, jambo ambalo linaweza kuingiza nchi kwenye machafuko,” ameeleza.

Akiongea taratibu na kwa msisitizo, Kamishena huyo alikumbusha yaliyotokea Kenya pale kura ya maoni ilipofeli kutokana na mwanasheria mkuu wa serikali kuwasilisha bungeni kitu tofauti na kilichopelekwa na Tume ya Katiba.

“Tuna mfano hai. Mapendekezo yote ya Tume yalichakachuliwa. Mimi siwezi kuwa sehemu ya kuingiza nchi kwenye machafuko. Naogopa hilo.”

Rasimu ya katiba imebeba Ibara 240 na kila ibara ina mapendekezo yake yanayoonyesha sababu za kuwepo kwake; ikiwa ni pamoja na mfumo wa Muungano wa serikali tatu.

“Sasa nani anakwenda kutolea ufafanuzi mambo haya? Nani anasimamia hili? Katika mazingira ambamo tumetukanwa hadi kutuhumiwa kutaka kuvunja Muungano, hili ni jukumu letu. Tunapaswa kwenda mbele ya Bunge la Katiba kutoa ufafanuzi. Vinginevyo, siwezi kuendelea kuwa mjumbe wa tume,” ameeleza kamishena huyo.

Kamishena huyo bado ana matumaini kuwa “…serikali na hasa Rais Kikwete, ataliangalia jambo hili kwa uzito unaostahili.”

Kamishena mwingine wa Tume amesema, “Hata mimi nitajiuzulu. Siwezi kuruhusu kutumiwa kisiasa. Hatua ya kuvunja Tume wakati Bunge la Katiba linajadili rasimu, ni sawa na serikali kuwasilisha bajeti bungeni bila kuwa na Baraza la Mawaziri.”

Anauliza, “Hoja za wajumbe wa Bunge la Katiba dhidi ya rasimu zitajibiwa na nani? Zitajibiwa na Chikawe (Mathias Chikawe,) ambaye hata hakushiriki kuandaa rasimu na ambaye amekuwa mpinzani mkubwa wa rasimu hii? Nafikiria kujiuzulu.”

Ofisa mmoja wa tume hiyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria, amekiri kuwapo taarifa kuwa baadhi ya wajumbe wameamza kujadili jinsi ya kujiuzulu.

Amesema kinachosababisha wajumbe hao kujiuzulu ni kile alichoita, “Kutokuwapo nia safi ya serikali katika jambo hili.”

Kamishena wa tatu aliyehojiwa amesema muswada unaodai saini ya rais “…una lundo la utata.” Ametaja baadhi ya vipengele vyenye utata ni pamoja na kile kinachohusu kuitwa kwa mwenyekiti au kamishena  kwenye Bunge la Katiba “kutolea ufafanuzi mambo yatakayohitaji ufafanuzi.”

“Atakwenda kama nani wakati Tume itakuwa imeshavunjwa? Sisi tunakula viapo na tunafungwa na maadili. Viapo vyetu vinakoma mara tume itakapovunjwa. Hivyo kumuita mjumbe au mwenyekiti wakati Tume haipo kisheria, atakuwa anakuja kama nani?” anahoji.

Tayari Tume ya Katiba iko kwenye hatua za mwisho za maboresho ya kinachoitwa, “Rasimu kamili ya Katiba,” inayotarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa katika Bunge la Katiba.

Rasimu hiyo yaweza kuwasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Katiba au mwakilishi wake.

Baada ya mjadala wa katiba kupitishwa bungeni, rasimu itaitwa “Proposed Constitution” – Katiba inayopendekezwa kwa wananchi. Rasimu itapelekwa kwa rais kama ilivyo na nakala kuwasilishwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

MwanaHalisi Online limegundua kuwa wakati bunge linapitisha muswada wa kusitisha shughuli za Tume mapema, tayari limepitisha, katika kikao cha bajeti kilichopita, zaidi ya Sh. 2.3 bilioni za kutumiwa na Tume katika kipindi ambacho tayari itakuwa imevunjwa.

Mkutano wa Bunge la bajeti uliopita, umeidhinisha pia Sh. 1.05 bilioni kutumiwa kuendeshea vikao maalum wakati Bunge la Katiba linaendelea. Fedha hizo ni malipo ya chakula, posho, viburudisho na usafiri.

Aidha, Bunge limeidhinishia Tume kiasi kingine cha Sh. 1.307 bilioni kwa kazi za kuitangaza kwenye vyombo vya habari na kuhamasisha wananchi kuunga mkono rasimu iliyopitishwa na Bunge.

Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) na mkurugenzi wa sheria wa chama hicho anasema hatua ya kufuta Tume kabla ya kumaliza muda na majukumu yake, “…inadhihirisha jinsi CCM wasivyofurahishwa na Rasimu iliyotolewa na Tume.”

Alisema, “Walipotunga sheria ya Tume ya Katiba, tuliwaeleza tuweke misingi thabiti ya uwazi na mustakabali wa tume. Hawakutusikiliza. Waliliburuza jambo hili. Waliamini tume itakayoundwa itafanya watakavyo. Leo matokeo yamekuwa tofauti, ndiyo maana wameamua kuwakomoa.”

Lissu amesema, “Pale mwanzo CCM walidhani Tume itakayoundwa itakubali kupokea maelekezo yake. Sasa walipoona ni tofauti, ndiyo hii hasira ya kuleta sheria ya kuivunja kabla ya kura ya maoni kufanyika.”

Mwanasheria huyo mashuhiri nchini anasema, siyo tu kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba isingevunjwa hadi kura ya maoni kufanyika, bali wajumbe wa Tume hiyo wangekuwa sehemu ya Bunge la Katiba.

“Kabla ya marekebisho haya, Tume ilikuwa imalize muda wake baada ya Tume ya Uchaguzi kuitisha kura ya maoni. Leo watu walewale waliosema ni muhimu tume hii iwepo hadi mwisho wa mchakato huu, ni haohao waliopitisha sheria ya kuivunja mapema,” anaeleza.

Hatua ya serikali kuchomeka marekebisho makubwa kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ndiyo chimbuko la upinzani kuungana na kupinga muswada huu. Upinzani unadai serikali imeingiza vifungu 11 bila kushirikisha Zanzibar na kwamba vyote vinapendelea chama tawala.

Miongoni mwa vifungu hivyo, ni Ibara ya 22 (1) (C) kuhusu uteuzi wa wabunge 166 wa Bunge la Katiba kutoka nje ya Bunge la Muunagno na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Taarifa zinasema kwenye muswada wa awali, rais alielekezwa kuteua mjumbe mmoja kutoka miongoni mwa majina matatu yatakayopendekezwa na taasisi zilizotajwa na sehria hiyo.

Akizungumzia hilo, Lissu anasema, “Sheria hii, ilikuwa ndogo sana. Muswada ulikuwa unataka rais aelekeze taasisi zinazohusika kupeleka kwake majina yasiyozidi matatu kwa ajili ya uteuzi. Lakini siku mbili kabla ya muswada kuwasilishwa bungeni, serikali ilichomeka kifungu kinachotaka taasisi kupendekeza majina tisa badala ya matatu,” anaeleza Lissu.

“Siyo hivyo tu. Muswada umempa mamlaka rais kuteua watu wengine kutoka nje ya orodha aliyokabidhiwa na taasisi husika,” ameeleza Lissu.

Lissu anahoji, “Sasa hao watakuwa wanamwakilisha nani? Watakuwa wanawakilisha taasisi au rais aliyewateua? Kama tulitaka watu hawa wawakilishe taasisi kwa nini tunatunga sheria ya aina hii?”

Vyanzo vya taarifa vinasema muswada wa awali uliojadiliwa na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria na baadaye kuwasilishwa kwenye serikali ya Mapinduzi  Zanzibar, ulikuwa na vifungu vitano.

Aidha, taarifa zinasema, mbali na Zanzibar kutoshirikishwa, muswada haukushirikisha hata Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

error: Content is protected !!