January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kikwete kulinda watuhumiwa Escrow

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete, amepanga kulinda na kutetea watuhumiwa wakuu katika ukwapuaji wa zaidi ya Sh. 321 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ndani ya Benki Kuu ya Taifa (BoT), MwanaHALISI Online limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya serikali na Ikulu jijini Dar es Salaam zinasema, Rais Kikwete amepanga kuwatetea kwa nguvu zake zote, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi.

“Prof. Muhongo na Maswi, hawawezi kuondoka ndani ya serikali hii. Hawa watu wanamtandao mkubwa sana ndani ya serikali na katika Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ambao unafanya kazi kubwa ya kuwatetea,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya serikali.

Amesema, “Mtu pekee ambaye anataka kutolewa kafara na ambaye kwa hakika, hakuhusika kwa namna yoyote ile na miamala iliyofanyika, ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.”

Kuvuja kwa taarifa kuwa Rais Kikwete amepanga kutetea wizi katika Akaunti ya Escrow, kumekuja siku tatu baada ya Prof. Tibaijuka kuhutubia mkutano na waandishi wa habari ambapo alieleza kusikitishwa kwake na njama za kumuhusisha katika kashfa hiyo.

Prof. Tibaijuka amekiri kupokea kiasi cha Sh. 1.6 bilioni kutoka kwa James Rugemalira, ambaye ni mmoja wa wanahisa katika kampuni ya kufua umeme wa dhaurura ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Hata hivyo, mbunge huyo wa Muleba Kusini amesema, fedha hizo hazikuwa zake; zilitolewa kama mchango kwa shule ya Sekondari ya Barbro Johansson ya jijini Dar es Salaam na Kajumulo Girls High School, iliyoko Bukoba.

Amesema, yeye aliupokea mchango huo na kuufikisha kunakohitajika. Wala hakujua kuwa fedha zilizotolewa na Rugemalira, zimetoka kwenye Akaunti ya Escrow, wala hakujua kama fedha hizo ni uharamu.

“Alichoniambia nikafungue akaunti ya kupokea fedha hizo katika benki ya Mkombozi. Nami nikafanya kama ambavyo mwenye fedha alinielekeza. Katika hili, sioni kosa langu na hivyo, siwezi kujiuzulu,” ameeleza Prof. Tibaijuka.

Prof. Tibaijuka hakuwahi kuhojiwa na chombo chochote kile; hakuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (PAP) wala bunge lenyewe.

Kiongozi mmoja kutoka madhehebu ya kidini amesema, ikiwa Rais Kikwete atamuondoa Prof. Tibaijuka katika nafasi yake kutokana na madai hayo, “hatakuwa amemtendea haki.”

Anasema, “Umma unafahamu kwamba anayejiita mmiliki wa kampuni ya PAP, alikabidhiwa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow, kabla ya kuwa mmiliki halali wa kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Anasema, “Ushahidi wa hili, unapatikana katika kesi iliyokuwa imefunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na James Rugamalira, dhidi ya Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndulu, kampuni ya PAP na Benki ya Stanbic, tawi la Tanzania.”

Nyaraka zinaonyesha Rugamalira alifungua shauri hilo mara baada ya kujiridhisha kuwa fedha zilizokuwapo katika akaunti ya Escrow zimechukuliwa, huku yeye akiwa bado hajaweza kulipwa asilimia 90 ya hisa zake katika IPTL. Rugemealira alikuwa akidai mamilioni ya shilingi baada ya kuuza asilimia 30 ya hisa zake katika IPTL.

Katika shauri hilo lililomalizika kwa njia ya usuluhishi, Mahakama Kuu ya Tanzania, pamoja na mengine, ilisema, “…baada ya kampuni ya VIP kulipwa fedha zake zilizotajwa katika mkataba, itailipa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) kodi yote ya mapato inayotokana na mkataba inayofikia Sh. 38.8 bilioni.”

Kiasi hicho cha fedha kimetokana na makadirio ya Mamlaka ya Mapato (TRA), kupitia kadirio la kodi Na. 427038820 la tarehe 15 Januari 2014.

“Kwamba baada ya VIP kulipa kodi hiyo kwa TRA, fedha zake zilizobaki hazitalipwa kwake mpaka pale itakapowasilisha Cheti cha Kulipa Kodi na hati za kuhamisha asilimia 30 ya hisa zake katika IPTL kwa mwanasheria wa PAP, na wasilisho hilo lilitakiwa kufanyika kabla ya saa 10 jioni ya tarehe 27 Januari 2014,” yameeleza makubaliano kati ya Rugemalira na aliowashitaki.

Aidha, Rugemalira alitakiwa mara baada ya kulipwa fedha zake zote kama zilivyotajwa katika mkataba wake, ikubali kuhamishwa asilimia 70 ya hisa za Mechmar Corporation ya Malyasia; uridhiaji huo sharti urudishwe nyuma kuanzia tarehe ya mauzo na uhamishaji wa hisa hizo kwa PAP.

Habari kamili soma MwanaHALIS Online Jumatano wiki hii:

error: Content is protected !!