October 23, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kikwete: Jumuiya ya Afrika Mashariki itenge bajeti mahakama

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete ameziagiza nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kutenga bajeti katika mahakama zao ili ziweze kujiendesha na kumaliza kero za Wananchi. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifungua mkutano wa 15 wa shirikisho la mahakimu na majaji wa nchi sita za Afrika Mashariki (EAMJA) jijini Mwanza.

Rais Kikwete amesema mara nyingi kesi zimekuwa zikichelewa mahakamani kutokana na kutokuwepo kwa bajeti ya kutosha na bajeti hizo zikitengwa, kesi zitasikilizwa kwa wakati na kuwapa imani wananchi.

“Kama bajeti itatengwa katika mahakama, malalamiko toka kwa wananchi kuhusu ucheleweshaji kesi hautakuwapo kabisa, nazishauli mahakama zetu kutenga bajeti ili kumaliza malalamiko yaliyopo,” amesema Kikwete.

Hata hivyo Rais Kikwete alitumia muda huo kuwaaga mahakimu na majaji wa nchi hizo katika muda wake wa kuongoza nchi kwa miaka 10.

“Natumia nafasi hii kuwaaga kwani muda wangu wa kuongoza na kuitumikia nchi unamalizika Oktoba mwaka huu,” amesema.

Rais wa Chama cha Majaji nchini, Jaji Ignas Kitus, amesema lengo la mkutano huo ni kuhakikisha wanashauliana na kuleta imani kwa wananchi katika mahakama zao na kuondoa wasiwasi na watumishi wa mahakama.

Amesema asilimia kubwa ya wananchi hawana imani na na mahakama zao na sasa wanahitaji kubadilisha mtazamo na kuishirikisha Serikali katika utoaji wa fedha za kuendesha Mahakama.

Ignas aliiomba jamii kuwa mstari wa mbele katika kupigana na vitendo vya uchukuaji wa rushwa kwa kutoa taarifa pale wanaposhawishiwa kufanya hivyo katika mahakama.

“Jamii yetu ni lazima ihamasishwe namna ya kuichukia rushwa na kuiepuka ili usiwepo uwezekano wa kutoa,” amesema.

Hakimu, Dolphina Alego kutoka Kenya ambaye pia ni mhazini wa EAMJA, amesema mkutano huo utaweza kufafanua kwa pamoja kazi zinazofanywa na mahakimu na majaji.

“Tupo hapa mahakimu na majaji wa nchi sita kwa lengo la kujadiliana kazi tunazozifanya katika nchi zetu, hadi tutakapomaliza tutafikia muafaka,” amesema Alego.

Mkutano huo ulioshirikisha nchi za Tanzania (wenyeji), Zanzibar, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, ulikuwa na kauli mbiu, “Kuimarisha imani ya wananchi kwa mahakama za Afrika Mashariki kupitia uwajibikaji na mifumo ya kupima utendaji na usimamizi wa mashauri”.

error: Content is protected !!