May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kikwete akumbusha alivyombeba Magufuli 2015

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akimtangaza John Magufuli kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM

Spread the love

 

RAIS mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, ameeleza ugumu aliopitia katika kumpitisha Hayati John Pombe Magufuli (61), kuwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2015. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kiongozi huyo mstaafu wa Tanzania ametoa kauli hiyo leo Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, katika ibada ya mazishi ya mwili wa Dk. Magufuli, iliyofanyika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Magufuli, Chato mkoani Geita.

Akizungumzia mchakato huo, Kikwete amesema, ugumu huo aliupata alipoamua kumpendekeza Dk. Magufuli kuwa mgombea urais wa CCM, kinyume na matakwa ya baadhi ya wajumbe wa vikao vya juu vya chama hicho.

Mwanasiasa huyo amesema, mnyukano mkali uliibuka pale alipowasilisha majina ya watu watano katika Kamati ya Maadili ya CCM, kufuatia baadhi ya wajumbe kudai waliokuwemo kwenye orodha hiyo hawatoshi kugombea urais.

“Na majina yale unakua nayo wewe mwenyewe, siri yako. Wako wengi walikuwa wanakuja wazee wastaafu wanasema fulani hivi, fulani usimuweke.”

“Majina yale mara ya kwanza niliyotoa kwenye Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM, mjadala mkali uliibuka kwa nini umemuacha fulani, hawa uliowaleta wote hawatoshi wepesi, tukabishana tukakubaliana,” amesimulia Kikwete .

Kikwete amesema myukano huo ulishika kasi zaidi, pale alipopeleka majina hayo katika Kamati Kuu ya CCM

“Tukaenda kamati kuu ndiyo ziliwaka, tumekaa mpaka usiku wa manane, ukitoka pale usiku wa manane kazi yangu kujenga hoja kwa nini haya majina matano yanafaa,” amesema Dk. Kikwete.

Anasema kwa kuwa wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania, alitumia mamlaka yake kuzima mgogoro huo.

“Nilijitahidi sana, wakati mwingine ukiwa rais na mwenyekiti una nguvu. Tukaanza kwa kishindo lakini tukazungumza kwa hoja tukakubaliana majina ni matano hatuongezi, hatupunguzi. Tukapiga kura,” amesema Kikwete.

Mwanasiasa huyo amesema, alilipendekeza jina la Dk. Magufuli katika kinyang’anyiro cha tano bora, kwa kuwa alikuwa na imani naye.

“Uteuzi wa kuwa mgomeba urais wa CCM 2015 sikusita kumpendekeza, katika majina matano niliyoyafikisha vikao vya juu vya chama mara ya kwanza kulikuwa na watu 38.”

“Kazi yangu kuwapunguza niwapate watano, lakini sikuwa na tabu na Magufuli, alikuwa wa kwanza halafu nikaongeza na wengine,” amesema Dk. Kikwete.

Mbali na Dk. Magufuli, wengine wane walikuwa ni; Balozi Asha Rose Migiro, Balozi Amina Salumu Ali, Januari Makamba na Bernad Membe.

Dk. Kikwete amesimulia hayo wakati anajibu madai yaliyotolewa na baadhi ya watu waliodai kwamba hakuwa hakutaka Dk. Magufuli agombee Urais wa Tanzania 2015.

“Wanasema akutukanaye hakuchagulii tusi, unaposikia vinong’ono JK hakumtaka Magufuli, labda JK mwingine, nimewasimulieni mchakato tulivyokwenda nao. Majina nimekuja nayo mie, tulipambana nayo mpaka matano, la kwanza ilikuwa Magufuli, nililiweka mie nashukuru mkutano mkuu lilikuwa lilelile,” amesema Dk. Kikwete.

Katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, kuliibuka mvutano ndani ya chama hicho, uliosababisha mwanachama wake mkongwe, Edward Lowassa, ahamie Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya jina lake kukatwa katika mchakato huo.

Alipohamia Chadema, Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, alipitishwa na chama hicho kugombea urais. Hata hivyo, aliangushwa na Dk. Magufuli, aliyetangazwa mshindi baada ya kupata asilimia 58 ya kura za urais.

Miaka kadhaa baadae, Lowassa alirudi tena CCM.

error: Content is protected !!