January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kikwete afokee rushwa, si wahamiaji haramu

Wahamiaji
Spread the love

NIMEREJEA jijini Dar es Salaam baada ya ziara ya siku nane mkoani Kagera nikiwa katika msafara wa Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Ilikuwa ziara nzuri iliyopata nafasi ya kutosha katika vyombo vya habari. Kila mahali tulikopita tulipokelewa vizuri na Watanzania waliopigika lakini wenye ukarimu wa ajabu.

Tathmini ya kweli ya ziara ile ilikuwa inafanyika katika msafara ndani ya magari kwenye barabara za vumbi. Humo watu walikuwa wanafunguka kikweli kweli na kusema yaliyo mioyoni mwao. Kila rais alipomaliza hotuba na sisi tukaingia katika magari, mjdala ulianza kuhusu hotuba zake.

Sehemu ya pili ya tathmini ya ziara na hotuba zake ilikuwa inafanyika ndani baa na nyumba za wageni tulipokuwa tunajichanganya na wenyeji na kuwasikiliza wanasemaje juu ya serikali na rais wake.

Katika kilele cha sikukuu ya mashujaa kilichofanyika katika kambi ya jeshi la wananchi Kaboya wilayani Muleba, Rais Kikwete alitoa siku 14 kwa majambazi kusalimisha silaha na wahamiaji haramu kuondoka nchini kurejea kwao.

Amri hii aliirudia mara kadhaa, kila alipopita na kuhutubia. Bali, katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, alionekana kushtuka na kupunguza makali ya amri yake pale aliposema, “Sijatangaza vita na nchi yoyote.”

Napenda kujadili amri ya rais nikizingatia yale niliyoyasikia kutoka kwa wakazi wa mkoa huo niliozungumza nao wilayani Ngara, Karagwe na Misenyi.

Rais aliwakomaria maafisa uhamiaji, watendaji wa vijiji na vitongoji kwa kutoa vibali bandia kwa wahamiaji haramu. Kimsingi, alikubaliana na madai ya muda mrefu ya Rais Paul Kagame wa Rwanda na serikali yake wanaodai kuwa tatizo la wahamiaji haramu linasababishwa na rushwa na kile wanachoita, “Rushwa ya Kitanzania.”

Rais Kikwete aliwasema maofisa wake wanaopokea rushwa ya mifugo na kugawa ardhi na kutoa vibali. Ni kwa hali hiyo, wengi wa waliomsikiliza rais akitoa amri ile hawaamini hata kidogo kuwa inaweza kutekelezwa.

Rais hakupaswa kuwakemea maofisa wa uhamiaji na vijiji. Alipaswa kuwa na orodha ya wanaotuhumiwa na kuwataja hadharani katika ziara yake. Alipaswa kuwakatalia wakuu wa wilaya waliokuwa wanalialia wakati wa ziaya rais kuhusu tatizo hili la watendaji kupokea rushwa.

Tatizo kubwa linalokwamisha operesheni mbalimbali za wahamiaji haramu mkoani Kagera, ni ukweli kuwa vyombo vya dola vimeishaingiliwa na wahamiaji haramu. Ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Usalama wa Taifa (TISS), Polisi, mahakama, na hata Ikulu, wamo watumishi wenye uraia tata na hawa ndio wanaofanya kila njia kukwamisha zoezi la kuwakamata na kuwarudisha wahamiaji haramu makwao.

Baadhi ya mafia wateule wa vyombo hivi, ama wameoa wahamiaji haramu au wameolewa. Katika kuufanya mtandao huo uwe mkali na mgumu, hata watoto wa vigogo kadhaa nchini wameoana na wahamiaji haramu.

Katika kijiji cha Nyakayanja ambako rais alizindua mradi wa umeme, wananchi waliniambia kuwa hata mkufunzi wa Mgambo wa kijiji hicho, ni mhamiaji haramu. Lakini huyu ni ofisa wa ngazi ya chini katika jeshi.

Nilipofuatilia kwa Afisa uhamiaji wa wilaya hiyo aliyekuwa nasi katika ziara hiyo, alidai hata yeye amesikia tuhuma hizo na kuwa mara kadhaa mkufunzi huyo ametembelewa na ndugu zake kutoka Rwanda – lakini   wanaoishi na kufanya kazi Uganda.

Tukiwa katika wilaya mpya ya Kyerwa, baada ya rais kuhutubia umati mkubwa na kurudia amri yake kuhusu wahamiaji haramu, diwani mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), tuliyekuwa naye katika gari alitueleza mimi na wenzangu kuwa serikali ilifanya makosa kumhamisha Afisa mmoja wa uhamiaji aliyepelekwa Pemba.

Afisa huyo alionekana angeweza kufanikisha zoezi la kurejesha wahamiaji hao haramu waliokuwa Karagwe na Kyerwa. Afisa huyo aliyetajwa kwa jina moja la Mtalasha, anasemekana alikataa rushwa peke yake huku kamati nzima ya ulinzi na usalama ya wilaya ikihongwa mamilioni ya shilingi na mifugo. Matokeo yake, afisa huyo alipozwa kwa kupandishwa cheo na kuhamishiwa Pemba ili zoezi hilo likwame.

Katika wilaya ya Misenyi, wananchi tuliokutana nao walitueleza kuwa uongozi wa wilaya hiyo umelainishwa kwa kupewa ng’ombe na wahamiaji haramu. Hata orodha iliyoandaliwa na mkuu wa mkoa ili itumike kuongoza zoezi hilo, haiwezi kufanya kazi kwa sababu mkuu wa wilaya ya Misenyi anasemekana ameshaandaa utetezi mzito wa kulinda wahamiaji haramu.

Aidha, wahamiaji haramu kutoka Rwanda, Uganda na Burund,i si wote wanaoishi vijijini na maporini. Katika nyumba ya wageni ya Tindamanyire ambako tulilala, tuliambiwa na wahudumu wa nyumba hiyo kuwa wahamiaji wengi wanaishi hapo mjini Kayanga, lakini uongozi wa wilaya hauwezi kuthubutu kuwagusa.

Wahamiaji haramu wanamiliki vitalu vikubwa vya mifugo katika ranchi ya Kitengule na Mabale na baadhi yao wamewagawia vigogo kadhaa ili walindwe. Mmoja wa wahamiaji haramu huyo, anaishi mkoani Dodoma. Anamiliki vitalu kwa ubia na watu walioko Ikulu na makao makuu ya polisi.

Nilipoongea na baadhi ya maafisa uhamiaji wa mkoa na wilaya, hasa baada ya rais kuwasema hadharani kuwa wanahusika, wao walijitetea kwamba tatizo la uhamiaji haramu ni kubwa kuliko rais anavyolidhania.

Walidai kuwa hata wale walio na vibali vinavyodaiwa ni halali, bado ni tatizo kwa sababu vibali hivyo havina kumbukumbu katika vijiji wala wilaya wanakotoka. Hii ina maana watu hao walipata vibali vyao kutoka makao makuu ya uhamiaji jijini Dar es Salaam kwa vimemo vya wakubwa.

Walibainisha kwa mfano sakata la Meya wa Bukoba Mjini ambaye alivuliwa uraia na serikali ya awamu ya tatu wakati huo akiwa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera. Meya huyo alikuja kurejeshewa uraia wake katika mazingira yenye utata.

Kwa mantiki hiyo, na kwa maoni ya watu niliokutana nao, amri ya rais kuhusu majambazi na wahamiaji haramu mkoani Kagera, haitekelezeki hata kidogo. Hata angetoa mwaka mzima. Haitekelezeki. Inahitajika dhamira thabiti ya uongozi na utawala kusimamia zoezi hili mpaka mwisho. Taifa letu kwa sasa halina mtu wa kusimamia zoezi gumu kama hili.

Uadilifu wa vyombo vya dola unatia shaka; na wananchi hawana imani na matamshi ya rais wao. Vibali vya kuishi nchini na hata vile vya uraia vinatolewa kama njugu pale mtu anapokuwa na fedha.

Pamoja na kwamba sheria za nchi yetu hazijaruhusu uraia wa nchi mbili, lakini wahamiaji haramu wengi wanamiliki passpoti mbili. Hivi mtandao wa wahamiaji haramu ni mrefu na umejikita hata katika vyombo vya maamuzi ya kidola.

Ndiyo maana operesheni zote za suala hili hufeli kabla hata halijaanza. Kisingizo cha kukosekana fedha ni kidogo kuliko tatizo la rushwa. Katika zoezi lililopita, mkuu mmoja wa wilaya mkoani Kagera alifanikiwa kupakia malori matatu (Mafuso) yaliyojaa ng’ombe kutoka Karagwe hadi huko kwao! Hayo ni matunda ya rushwa.

error: Content is protected !!