July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kikwete afagiliwa uteuzi wa Magufuli

Viongozi wa juu wa CCM wakiwa kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho mjini Dodoma

Spread the love

VIONGOZI  wa dini mkoani Dodoma wamempongeza Waziri wa Ujenzi Dk, John Magufuli kwa kuteuliwa na chama chake kuwania urais kwa kusema kuwa nafasi hiyo imemstahili. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Wakizungumza na Mwanahalisi Online, baadhi ya viongozi wa dini mkoani hapa wamesema kuwa Dk, Magufuli ni mmoja wa viongozi ambao ni wachapakazi kwa hiyo nafasi aliyopewa na chama chake inamfaa.

Shekhe Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Mustapha Shaaban amesema  kuwa Chama cha Mapinduzi kimempitisha mtu ambaye hakutajwa sana midomoni mwa watu kuwa atashinda, na hakuwa kwenye orodha ya watu waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushika nafasi hiyo.

“Lakini suala la mtu kuwa kiongozi liko mikononi mwa Mwenyezi Mungu ambaye humchagua mtu amtakaye,” amesema Shekhe Shaaban na kuongeza kuwa,

“Katika mchakato mzima wa kumpata mgombea wa nafasi ya Urais kupitia CCM, Mungu aliamua kuweka mkono wake kwa kutumia hekima, busara na sababu anazozijua yeye na ndiyo maana akampitisha mtu ambaye alikuwa hapewi nafasi kubwa ya kushika nafasi hiyo.”

Amesema  katika mchakato wa kumpata mgombea huyo kwa kupitia CCM kuna baadhi ya majina yaliyokuwa yanapewa kipaumbele lakini kwa kuwa madaraka na uongozi vinatoka kwa Mungu aliamua kumpa Dk, Magufuli.

“Dk, Magufuli hakuwa miongozi mwa watu waliokuwa wanategemewa kushinda katika kinyang’anyiro hicho,” amesema  Shekhe Shaaban.

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Pentecoste Holiness Association Mission (PHAM) Kanda ya Kati, Julius Bundala amesema  kuwa Dk, Magufuli alistahili nafasi hiyo kwa kuwa hata kazi zake alizokuwa akizifanya katika nyadhifa mbalimbali alizozishika serikalini zilikuwa zinaonekana.

“CCM imemteua mtu ambaye mioyo ya watu wengi inamkubali kwa kuwa hana kashfa yeyote na ni mchapakazi hodari kwa kuwa kazi zake nyingi ni za uhakika na zinaonekana, CCM imepata chombo cha ushindanishi,” amesema  Askofu Bundala .

error: Content is protected !!