July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kigwangala: Tanzania tuitakayo ni hii hapa

Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangallah akicheza ngoma na wanachama wake wa CCM jimboni kwake

Spread the love

TAIFA huru lililo na misingi imara katika kupambana na rushwa, kuinua kilimo, bajeti isiyo tegemezi, ukusanyaji mzuri wa kodi ndiyo Tanzania tuitakayo. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo na Hamis Kigwangallah katika Uwanja wa Parking Nzega mkoani Tabora wakati akitangaza rasmi nia ya kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwa atapata ridhaa ya chama hicho.

Kigwangala ambaye ni Mbunge wa Nzega amesema, dhamira iliyomsukuma kujitokeza na kuomba ridhaa ya chama chake ni kutaka kujenga uchumi imara, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha serikalini, rushwa, kuondoa utegemezi wa bajeti sambamba na matumizi mazuri ya rasilimali za taifa.

“Dhamira yangu ni kuondoa utegemezi wa bajeti, kubana matumizi, posho za vikao na kukuza uchumi. Hapa lazima tuwekeze katika kilimo na viwanda,” amesema Kigwangala.

Hata hivyo amesema, watu wengi wanaweza kushangazwa na hatua ya kujitosa katika urais wakati ni muhula mmoja tu amekuwa mbunge.

Katika hilo amesema, wenye uzowefu na Ikulu ni wanne tu nchini. Amewataja kuwa ni Mwalimu Julius Nyerere-Awamu ya Kwanza; Alhaji Ali Hassan Mwinyi-Awamu ya Pili; Benjamin Mkapa-Awamu ya Tatu na Rais Jakaya Kikwete wa awama hii ya nne na kwamba, wengine wote hawana uzoefu na urais hivyo wanafanana naye.

“Wanaweza kusema nina umri mdogo lakini wakumbuke kuwa Tony Blair (Waziri Mkuu Mstaafu Uingereza), Obama (Rais Obama) wa Marekani wote hawa waliingia madarakani wakiwa katika miaka ya 40 hivi.

“Blair alikuwa na umri wa miaka 44 na Obama alikuwa na miaka 47 na wameingia kuongoza mataifa makubwa.

“Uchaguzi ni mambo yajayo na sio historia. Uzoefu si hoja, uzoefu ni katika mambo mengine na si urais.” Amesema.

Amesema, Tanzania anayoitaka kuwa ni ile iliyo uchumi imara kutoka ndani na si kutegemea mabepari ambao ndio huchukua rasilimali za Taifa ikiwa ni pamoja na gesi na madini.

Hata hivyo amesema, haitaki Tanzania ambayo sasa hivi mtu ili ashinde ubunge ama urais lazima awanunue watu. “Mtu mpaka ashinde ubunge na urais lazima awanunue watu.”

Amepigia chapuo kizazi kipya ambapo amesema, imefika wakati sasa wale waliokuwepo serikalini kuanzia miaka ya 70 wakae pembeni na kuwashukuru kwa kazi waliyoifanya na kwamba, sasa hivi ni zama za kizazi kipya.

“Kila zama zina watu wake na kila kitabu kina wakati wake. Kizazi kilichopita tuwashukuru lakini tuwaambie inatosha. Waliokuwepo kwenye miaka ya 70 watupishe, hizi ni zama za kizazi cha sasa,” amasema Kigwangala.

Akizungumzia sekta mbalimbali nchini Kigwangala amesema, ipo haja ya kuwapa motisha wafanyakazi wa umma wanaoishi vijijini ili wapende na waendelee kutoa huduma katika maeneo hayo.

“Hawa wanatakiwa wajengewe nyumba bora, miundombinu, maji na afya ili wafanye kazi kwa uhodari,” amesema.

error: Content is protected !!