Spread the love

JESHI la Polisi Mkoa wa Kigoma, linawashikilia watu sita wakituhumiwa kuhusika na matukio saba ya mauaji yaliyotokea katika nyakati tofauti mkoani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma…(endelea).

Taarifa hiyo ilitolewa jana tarehe 1 Februari 2022 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kigoma, ACP James Manyama, akizungumza na wanahabari mkoani humo.

ACP Manyama alisema matukio mawili yalitokea wilayani Kankonko, wakati Buhigwe yalitokea mawili na Kasulu (3).

“Kule Wilaya ya Kankonko kulikuwa na matukio mawili ya mauaji, lakini pia Kasulu kulikuwa na matukio matatu ya mauaji na Buhigwe kulikuwa na matukio mawili. Katika matukio yote mawili jumla ya watuhumiwa sita waliweza kukamatwa,” alisema ACP Manyama.

ACP Manyama alisema “kwa maana kwamba kule Kakonko watuhumiwa wote waliohusika na matukio yale waliweza kukamatwa, lakini pia kwa Kasulu katika makosa yote matatu jumla ya watuhumiwa wanne waliweza kukamatwa.”

Kamanda huyo wa Jeshi la Polisi Kigoma, alisema katika tukio la mauaji ya watu wawili lililotokea wilayani Buhigwe, mtu anayedaiwa kuhusika aliuawa baada ya kushambuliwa na wananchi, akijaribu kutoroka kuelekea Wilaya ya Kasulu.

“Lakini nigusie tu kwamba, chanzo cha matukio yote ya kwanza ni ulevi wananchi wengine wanalewa na wanagombana. Jambo la pili ni wivu wa mapenzi kunakuwa na migogoro. Lakini pia migogoro ya kifamiia imepelekea mauaji kutokea,” alisema ACP Manyama.

ACP Manyama alisema tukio la mauaji wilayani Kasulu lilitokea tarehe 2 Januari 20222 ambapo Amos Buhaga (68), aliuawa kw akupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani maeneo ya kisogoni na watuhumiwa wawili, Ramadhan Yasin na David Antony, wakimtuhumu kwa imani za kishirikina.

Watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamni tarehe 20 Januari mwaka huu.

Katika tukio lingine, ACP Manyama alisema watu watatu wanaoshukiwa kuwa majambazi wamefariki dunia huku Askari G6335 Detective Coplo Issa, akijeruhiwa maeneo ya begani, katika majibizano ya risasi yaliyoibuka usiku wa Januari 30, 2022, katika Kijiji cha Nyarugusu.

ACP Manyama alisema, Askari walifanya ukaguzi katika eneo hilo na kukamata bunduki ya kivita AK47 yenye namba za usajili TX87101996, iliyokuwa na magazine mbili zenye risasi 47, maganda mawili ya risasi.

“Katika juhudi za kupambana na uhalifu Kigoma mapema tarehe 30 Januari majira saa 5.00 usiku, Kijiji cha Nyarugusu ambako kuna kambi ya wakimbizi kutoka Burundi na Congo askari polisi wakiwa doria walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa majambazi wenye silaha za moto wamevamia sokoni na kupora,” alisema ACP Manyama na kuongeza:

“Sababu eneo lile tunafahamu ni tete askari walikuwa doria eneo lile na kuweza kudhibiti hali, askari wetu wakati wanafika eneo lile tayari majambazi walishaanza kurusha risasi. Hivyo kwa kujihami ili kutoroka lakini kwa umahiri mkubwa wa askrai wetu waliweza kukabiliana nao,”

“Ambapo majambazi watatu waliweza kupigwa risasi ambapo walifariki baadae wakati wanapelekwa hospitalini kwa ajili ya kupata matibabu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *