January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kigogo TRA akimbilia “kwa Chenge”

Naibu Kamishna Upelelezi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Loicy Appolio

Naibu Kamishna Upelelezi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Loicy Appolio, akiwa mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma akisikiliza mashtaka yake

Spread the love

KAMA alivyofanya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), kukimbilia Mahakama Kuu kuweka pingamizi asihojiwe na Baraza la Sekretarieti na Maadili ya Viongozi wa Umma, ndivyo amefanya Loicy Jeconia Appollo-Naibu Kamishna Upelelezi wa Kodi waMamlaka ya Mapato (TRA). Anaripoti Deusdedit Kahangwa…(endelea).

Appollo amefika katika Baraza hilo leo na kusomewa mashtaka sita yanayohusiana na ukiukaji wa maadili ya viongozi wa umma, lakini akayakanusha yote na kisha akakataa kuhojiwa zaidi kwa madai kwamba halina mamlaka ya kisheria kuendesha kesi hiyo.

Akiwa mbele ya Baraza hilo lililokutana katika ukumbi namba 2 ulioko Karimjee jijini Dar es Salaam, Appollo alisomewa mashtaka mbalimbali na Mwanasheria wa Sekretarieti hiyo, Mwanaarabu Tale.

Kwa mujibu wa Tale, mnamo 24 Februari 2014, kupiti akaunti yake namba 0012102684801 iliyoko katika Benki ya Mkombozi Tawi la St. Joseph, Appollo alipokea shilingi 80,850,000 kutoka kwa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd.

Mwanasheria huyo alidai kwamba, kampuni hiyo inao uhusiano wa kikazi na TRA kama mlipa kodi. Kwa sababu hiyo Appollo akatuhumiwa kukiuka vifungu mbalimbali vya sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995 kama ilivyorekebishwa mwaka 2001.

Kwanza, Appollo anadaiwa kufanya kazi bila kuzingatia viwango vya juu vya maadili na hivyo kushindwa kulinda na kuimarisha imani ya wananchi na matumaini katika uadilifu, haki na kutopendelea kwa serikali, jambo ambalo ni kinyume cha ibara ya 6 (a) ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

Pili, Appollo anadaiwa kushindwa kupanga mambo yake kwa namna ambayo ingezuia kutokea kwa mgongano halisi wa maslahi au kuwepo na uwezekano wa mgongano au kuonekana kuwepo mgongano wa mashali katika utendaji kazi wake, jambo ambalo ni kinyume cha ibara ya 6(e) ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

Tatu, Appollo anadaiwa kuomba na kupokea fadhila za kiuchumi ambazo sio zawadi ndogo, wala ukarimu wa kawaida au fadhila ya thamani ya kawaida, jambo ambalo ni kinyume cha ibara ya 6(f) ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

Nne, anadaiwa kupata kwa makusudi manufaa makubwa ya kifedha, jambo ambalo ni kinyume cha ibara ya 12(1)(e) ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

Tano, Appollo anadaiwa kupokea zawadi yenye thamani inayozidi shilingi 50,000 na kukataa kuitaja na kuikabidhi kwa Afisa Mhasibu wa ofisi inayohusika, jambo ambalo ni kinyume cha ibara ya 12(2) ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

Shitala la sita halihusiani na miamala ya akaunti ya Escrow. Katika shitaka hili, anadaiwa kuficha taarifa muhimu alizopaswa kuingiza katika matamko yake ya Rasilimali na Madeni kwa kipindi kilichopo kati ya 31 Desemba 2011 na 31 Desemba 2014, matamko ambayo amekuwa akiyawasilisha kwa Kamishna wa Maadili kwa mujibu wa sheria.

Mwanasheria alisema kwamba, Appolo anamiliki Hoteli inayoitwa “Classic Hotel” yenye thamani ya shilingi 150,000,000/=, ikiwa imejengwa eneo la Kinondoni, jijini Dar es Salaam, na kwamba kuficha taarifa hizo ni kukiuka ibara ya 9(1)(c) ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.   

Mara baada ya Appollo kusomewa mashtaka hayo, amesema kwa mujibu wa amri ya Mahakama Kuu, mashtaka yote yanayohusu fedha zilizotoka katika akaunti ya Escrow hayawezi kujadiliwa na Baraza la Maadili au chombo kingine chochote cha serikali. Kwa hiyo akaomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Baraza kuhusu jambo hili.

Katika majibu yake, Mwenyekiti Jaji Hamis Msumi, amesema kuwa amepitia mepama malalamiko yake hayo lakini akaona kwamba hayana msingi wa kisheria.

Baada ya kuambiwa hivyo, Appollo aliomba ruhusa ya kwenda Mahakama Kuu kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa Baraza na mwenyekiti amemruhusu kukata rufaa na kuahirisha shauri hilo.

Appollo sasa amefuata njia aliyotumia Chenge na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip  Saliboko. Wote wamekata rufaa Mahakama Kuu wakihoji mamlaka ya Baraza la Maadili.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujuna, alichukua njia inayofana na hii japo ni tofauti kidogo.

Yeye alileta pingamizi mbele ya Baraza akidai kwamba tayari anakabiliwa na kesi ya jinai mahakamani kuhusu jambo hilo hilo. Hivyo, akasema kuwa kesi moja ikisikilizwa sehemu mbili kwa mpigo atakosa muda wa kuandaa utetezi wake.

error: Content is protected !!