September 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kigogo TPA, wakili  waunganishwa kesi uhujumu uchumi, mwingine asakwa

Afisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani

Spread the love

JAPHETI Jirori, aliyekuwa Meneja Usimamizi wa Akaunti za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Wakili Arnold Temba, Mkurugenzi wa Kampuni ya ELA Advocate na Mnengele Associates, wameunganishwa katika kesi ya uhujumu Uchumi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Jirori na Temba wameunganishwa katika Kesi ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kiasi cha Sh. 8 bilioni, fedha zilizokuwa mali ya TPA, iliyokuwa inawakabili watu nane, wakiwemo watumishi saba wa TPA, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza.

Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa tarehe 26 Juni 2020 na Doreen Kapwani, Afisa Uhusiano wa Takukuru kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Brigedia Jenerali, John Mbungo.

Wakati washtakiwa hao wawili wakiunganishwa kwenye kesi hiyo, Takukuru inamsaka Deodatus Chrispian Iranghe, Mfanyabiashara jijini Dar es Salaam, ambaye pia anadaiwa kuhusika katika mashtaka hayo.

Takukuru imetangaza dau nono la Sh. 10 milioni, kwa mtu atakayewapa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo.

“Tunaendelea kuukumbusha umma kwamba tunaendelea kumtafuta Iranghe na tunatoa wito kwa atakayekuwa na taarifa za kuwezesha kupatikana kwa mtuhumiwa huyu, basi atoe taarifa katika ofisi yoyote ya TAKUKURU iliyoko karibu naye na zawadi nono ya Sh. 10 milioni itatolewa,” inaeleza taarifa hiyo.

Brigedia Jenerali, John Mbungo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru

Washtakiwa wengine ambao walisomewa mashtaka yao tarehe 12 Juni 2020 mahakamani hapo ni, Deogratius Belian Lema, aliyekuwa Mhasibu Mwandamizi TPA makao makuu. Alike Chikondano Mapuli, aliyekuwa Mhasibu Mwandamizi TPA makao makuu.

Marystella Charles Minja, aliekuwa Afisa Uhasibu TPA Makao makuu. Na Thomas Samuel Akile, aliyekuwa mhasibu wa kituo cha bandari Mwanza.

Wengine ni, Ibrahim Bunyonga Lusato, aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Bandari Kituo cha Mwanza. Wendelin Damian Tibuhwa, aliyekuwa  mhasibu wa Kituo cha Bandari Mwanza. James Patrick Mbedule, aliyekuwa Mhasibu Kituo cha Bandari Mwanza, pamoja na Leocard Wilfred Pendo kipengele.

“Waendesha mashtaka watawasomea watuhumiwa hawa mashitaka yao mahakamani leo Juni 26 2020 na kuunganishwa na wale washtakiwa nane wa awali. Washtakiwa nane walisomewa mashtaka yao tarehe 12 Juni 2020,” inaeleza taarifa

Amesema washtakiwa hao walifikishwa mahakamani baada ya kubainika walihusika kutenda makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, yakiwemo, kula njama kutenda kosa, kughushi, kuunda genge la uhalifu, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuisababishia mamlaka hasara pamoja na utakatishaji wa fedha haramu.

 “Katika uchunguzi wake Takukuru ilibaini kwamba makosa hayo yalipelekea kusababisha upotevu wa fedha kiasi cha zaidi ya Sh. 8 bilioni, mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania, TPA,” inaeleza taarifa ya Doreen.

error: Content is protected !!