December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kigogo THRDC autosa ubunge kisa uanaharakati

Onesmo Olengurumwa

Spread the love

 

MRATIBU wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema hana mpango wa kugombea ubunge wa Ngorongoro, mkoani Arusha, kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika tarehe 11 Disemba 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Olengurumwa ametoa kauli hiyo akizungumza na MwanaHALISI Online, leo Jumatano, tarehe 20 Oktoba 2021, baada ya kuenea uvumi kwamba ni miongoni mwa watu wanaotajwa kutaka kugombea Jimbo la Ngorongoro.

Kada huyo wa CCM amesema, hana mpango wa kurejea kwenye siasa aliyoaiacha 2010, kwa ajili ya kujikita katika masuala ya utetezi wa haki za binadamu.

“Mwaka huu pressure (shinikizo) zimekuwa kubwa zaidi, lakini bado sijasema chochote kama nitagombea . Kwa kuwa msimamo wangu wa kutokurudi katika siasa bado upo pale pale,” amesema Olengurumwa.

Olengurumwa amesema, ndoto yake ya kusaidia wananchi wa Jimbo la Ngorongoro alikozaliwa, bado iko palepale na kwamba anaweza kuitimiza bila ya kuwa mbunge.

“Huwa sigombei kwa kuwa naamini kazi ya utetezi wa haki za Binadamu, ina uhuru mpana wa kusaidia watanzania zaidi ya wana Ngorongoro,” amesema Olengurumwa.

Hata hivyo, Olengurumwa amesema anaendelea kushauriana na baadhi ya watu kuhusu suala hilo.

“Naendelea kusikiliza ushauri wa watu lakini mwisho wa siku nitaamua mwenyewe na kuwaeleza wana Ngorongoro kama nitagombea ama sintagombea kwa lengo la kuendelea kuwatumikia kama Mtetezi,” amesema Olengurumwa.

Kabla ya kuingia katika harakati za utetezi wa haki za binadamu, Olengurumwa aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM)mkoani Arusha kuanzia 2008 hadi 2012.

Aliwahi kugombea uenyekiti wa umoja huo wilaya ya Ngorongoro.

Mwanaharakati huyo amejizolea umaarufu wilayani Ngorongoro kutokana na kujitoa kwa hali na mali kutafuta suluhu za utatuzi wa migogoro ya ardhi inayowakabili wananchi wa maeneo hayo.

Hali iliyopelekea baadhi ya wananchi jimboni humo kumtaka agombee nafasi hiyo iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wake, William Tate Ole Nasha, kilichotokea tarehe 27 Septemba mwaka huu.

error: Content is protected !!