May 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kiganja anafichua kilichofichika

Mohamed Kiganja, Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT)

Spread the love

UNAIKUMBUKA habari iliyoandikwa na gazeti hili katika toleo Na. 361 la Oktoba 17-23, 2016, iliyokwenda kwa maneno ‘Rais Magufuli ashtukia dili.’ Kama haukubahatika kuisoma itafute isome zaidi ya mara moja, anaandika Erasto Masalu.

Ukimaliza kusoma habari hiyo, fumba macho, sasa tafakari kauli za Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja. Hapo utakuwa umefichuliwa ni kwanini kumekuwa na sarakasi za mabadiliko ya miundo ya klabu za Simba na Yanga.

Habari hiyo iliyoandikwa ukurasa wa mbele zaidi ya mwezi mmoja sasa, ilikuwa inaelezea jinsi serikali ilivyojipanga kukwamisha mchakato wa mabadiliko ya klabu hizi kwa hofu ya kisiasa.

Kwa bahati mbaya, habari hiyo ilikuwa moja ya habari chache zilizowahi kuchapishwa na MwanaHALISI, katika historia yake, na kukataliwa na umma wa wasomaji. Mhariri alipokea simu nyingi za wasomaji wakimshutumu kwa kuchapisha habari ile. Tena wakisema “mmetumika kupinga mabadiliko” kwa maslahi ya watu wachache.

Wengi wa watoa maoni walijigawa katika itikadi za kinazi za klabu za Simba na Yanga, kuliko kuwa na hoja za kimantiki za maudhui ya habari yenyewe.

Lakini ukweli wa habari hiyo ulikuwa wazi – mkakati wa serikali kuhakikisha matajiri hawamiliki timu hizo kwa kuwahofia kuja kupata nguvu kwa jamii ambazo zinaweza kutumika kwa maslahi ya kisiasa; kama ilivyokuwa katika baadhi ya nchi jirani hasa DR Congo.

Kiganja alitangaza na kushikilia kwamba serikali imesitisha mchakato wa mabadiliko ya katiba za klabu hizi na kuzitaka “kwanza zifuate utaratibu.”

Kiganja alianza kutoa maelekezo ya kusitisha mipango ya kukodisha na kuuza klabu, akisema kwenye katiba zao hakuna sehemu panaposema zitakodishwa au kuuzwa.

Wengi walipokea maelekezo hayo kwa nia njema huku wakiamini kuwa ilikuwa ni utaratibu wa kawaida kutoka kwa serikali, kwa kuwa ndiyo msimamizi wa sera ya michezo nchini. Sasa ndio kila mtu anaona kwamba nyuma ya agizo au “amri” ya serikali, kuna ajenda mahsusi ya kukwamisha mpango wa Simba na Yanga kutafuta maendeleo ya kweli kupitia michezo.

Maelezo hayo yalikuwa msumari kwa Yanga ambao tayari walikuwa wameshaingia makubaliano ya awali ya kukodisha klabu yao, lakini kwa Simba kwao ilikuwa kama angalizo kuelekea katika mchakato huo.

Kauli ya Kiganja iliungwa mkono na Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye alinukuliwa akisema:

“Kumekuwa na mijadala ya mabadiliko ya mifumo namna ya kuendesha klabu zetu, kimsingi serikali tunaunga mkono mabadiliko chanya katika klabu za Simba na Yanga, lakini cha kwanza michakato hii lazima iwe na uwazi na wala isigubikwe na rushwa.”

Wakati wengi wakiamini mambo yanaenda sawa huku wakisubiri kuona klabu hizo zinafuata taratibu walizowekewa na serikali kupitia BMT, sasa Kiganja amefichua kile kilichokuwa kimejificha na kuwafanya wengi wasielewe lengo la serikali.

Kiganja amekuja mara ya pili. Safari hii anachokisisitiza kinapingana na alichokisema awali, baada ya klabu ya Simba kutangaza mkutano wake wa dharura wa wanachama kwa lengo la kujadili ajenda ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji klabu yao.

Simba ilitangaza kuwa mkutano huo utafanya mabadiliko ya katiba ili kuendana na matakwa ya serikali na kuendelea na mipango yao, lakini kabla ya kufikia siku ya mkutano, Kiganja ameibuka na kutoa maelezo ambayo ukiyapima, anaonesha kuhofia kitakachofanyika hakitakuwa sahihi.

Anasema kwa mshangao kwamba ni kwanini wanaotaka kununua klabu hizo wasianzishe klabu zao? Anaelekeza wale anaoita wataka kununua klabu za Simba na Yanga, wajiulize ni malengo gani yalitumika katika kuanzishwa klabu hizi?

Hakuyaeleza haya kama msingi wa hoja yake awali. Hakusema haya alipohimiza mabadiliko ya miundo ya klabu lazima yafuate taratibu za katika za klabu zao. Sasa viongozi wa klabu kwa mfano ya Simba wanapoitisha mkutano ili kuwapa wanachama wao nguvu ya kuamua mustakbali wa klabu yao, Kiganja anazuia.

Maelezo yake ofisa huyu mwandamizi serikalini, yanatoa majibu kuwa hata yale maelekezo ya awali aliyoyatoa ya haja ya klabu kubadilisha katiba zinapotaka kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji, yalikuwa ni “danganya toto” maana inadhihirika sasa kuwa serikali ina malengo tofauti.

Hapa ndipo wasomaji wa gazeti hili wanapolazimika kurudi nyuma kwenye ile habari waliyoichukia na kushutumu mhariri kwa kuichapisha. Wanachama wa Simba na Yanga wakae chini kutafakari, wakijua kwamba klabu ni zao si za serikali. Basi na wapi zielekee ni jukumu lao.

Lakini wakienda hivyo wanavyotaka, kwa upande mwingine wajue kuwa maana yake wamejiandaa kukabiliana na mkono wenye nguvu ambao Kiganja ni mtumwa tu wa malengo ya wakubwa zake.

error: Content is protected !!