January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kigaila awachimba mkwara polisi Dodoma

Spread the love

MGOMBEA ubunge jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chadema, Benson Kigaila amelitaka jeshi la polisi kufanya shughuli za kwa kufuata misingi ya kisheria na wasikubali kutumiwa na wanasiasa. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Mbali na hilo amesema iwapo jeshi la polisi litashindwa kufanya kazi zao basi watangaze wazi kuwa ni jeshi la kisiasa na siyo vinginevyo.

Kigaila alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wana habari juu ya mwenendo wa kisiasa kwa kudai kwamba jeshi la polisi mkoa wa Dodoma linawaonea wanachama wa vyama vya UKAWA na kuwabeba wagombea wa CCM.

Amesema inasikitisha kuona jeshi la polisi linafanya kazi za kisiasa badala ya kufanya kazi kwa kuzingatia haki na usawa.

“Tumeshuhudia jinsi jeshi la polisi linavyowabeba wagombea wa CCM kwa kuwapatia ulinzi lakini sisi tumekuwa hatupewi ulinzi na matokeo yake wanadai tunafanya fujo.

“Mbaya zaidi tunasikitishwa na jeshi la polisi kuanza kuwakamata vijana kwa madai kwamba ni wazurulaji hivyo ni vitisho kwa vijana na wanatumiwa na viongozi wa CCM,” amesema Kigaila.

Mgombea huyo amesema kwamba kwa sasa Chadema inakabiliana na upinzani wa vyama viwili ambavyo alivitaka kuwa ni CCM na jeshi la polisi ambalo linafanya kazi ya siasa.

Hata hivyo Kigaila alilitaka jeshi la polisi kutoingilia mambo ya kisiasa kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha machafuko.

“Tunajua kazi ya jeshi la polisi hivyo ni vyema wakaiweka mbali na siasa ila watimize wajibu wa kwa mujibu wa sheria taratibu na kanuni na kama wataendelea kutumiwa na CCM kama wanavyofanya hatutakubali,” amesema Kigaila.

Kwa upande wake mkuu wa polisi mkoa wa Dodoma, David Misime amesema jeshi la polisi halifungamani na chama chochote cha siasa na litakabiliana na mtu yoyote bila kujali cheo wala chama.

error: Content is protected !!