Wednesday , 17 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Kifo cha mwanafunzi UDOM: Tume yamsafisha naibu waziri
Habari MchanganyikoTangulizi

Kifo cha mwanafunzi UDOM: Tume yamsafisha naibu waziri

Yasema hakina uhusiano na ajali aliyopata

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dk. Festo Dugange
Spread the love

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini (THBUB), imetoa matokeo ya uchunguzi wa kifo cha Nusura Abdallah, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kwa kusema, “kifo chake hakikutokana na ajali ya gari ya naibu waziri, Festo Dugange. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mwenyekiti wa THBUB, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu, amewaambia waandishi wa habari mjini Dodoma, tarehe 2 Juni 2023, kwamba kinyume na minong’ongo kuwa kicho cha Nusura kilitokana na na ajali ya gari iliyomhusisha naibu waziri Dugange, ukweli ni kuwa hakuna uhusiano wowote wa ajali hiyo na kifo cha mwanadada huyo.

Badala yake, Jaji Mwaimu alisema, kifo cha Nusura, kilichotokea mkoani Kilimanjaro, kimesababishwa na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inasema, Nusura alifariki dunia tarehe 1 Mei 2023 na ajali iliyomkuta naibu waziri Dugange, ilitokea usiku wa Aprili 25 kuamkia 26 mwaka huu.

Nusura alikuwa akisomea shahada ya kwanza ya Sanaa katika Sayansi ya Jamii.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume, Nusura alianza safari yake ya kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro, 27 Aprili 2023 kwa kutumia basi la Manning Nice, baada ya gari la Kapricon alilopanga kusafiria awali kuchelewa kuondoka.

Hata hivyo, Jaji Mwaimu amesema, basi hilo lilimfikisha Nusura Babati na baadaye alipanda gari ndogo aina ya Coaster hadi Arusha, kisha kumalizia safari yake hadi Moshi kwa basi la Ibra Line.

Alifika mjini Moshi majira ya saa tano usiku na kupokelewa na mchumba wake, Juma Mohamed Kundya na kwenda moa kwa moja hadi nyumbani kwake.

Jaji Mwaimu alisema, “lengo la safari hiyo, lilikuwa ni kuzungumzia masuala ya uchumba wao na kupanga siku ya kwenda kujitambulisha nyumbani kwao Singida. Alipanga kukaa hapo hadi tarehe 2 Mei 2023 ndipo angerejea Dodoma.”

Tume imegundua katika uchunguzi wake, kwamba Nusura aliwasiliana kwa mara ya mwisho na familia yake, 29 Aprili 2023 na 1 Mei 2023, ilikuwa mara ya mwisho kuwasiliana na rafiki anayesoma naye chuoni.

Jina la rafiki aliyekuwa anasoma pamoja na Nusura Chuo Kikuu cha Dodoma na ambaye aliwasilisha na mwanafunzi huyo, halikutajwa kwenye taarifa ya THBUB. Wala tume haikutaja jina la mtu wa mwisho wa familia aliyewasiliana na mwanadada huyo.

Mwenyekiti wa tume anasema, taasisi yake imegundua kuwa tarehe 1 Mei 2023, Nusura aliandaa chakula cha jioni nyumbani kwa mpenzi wake – Juma Kundya, mjini Moshi. Waliokula chakula hicho, ni Nusura mwenyewe, mchumba wake na mpwa wa mchumba wake.

Marehemu Nusura Abdallah

Alisema, baada ya kumaliza kula, Nusura alijisikia vibaya na kuanza kutapika hadi kuishiwa nguvu, hali iliyosababisha kufikishwa hospitali ya Faraja kwa matibabu.

Alisema, pamoja na jitihada na hatua mbalimbali za kitabibu zilizochukuliwa na madaktari wa hospitali hiyo, Nusura alifariki majira ya saa 5 usiku wa siku hiyo.

Kwa mujibu wake, vipimo vilivyofanywa na hospitali hiyo vilionesha kifo cha Nusura kilitokana na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu.

“Daktari aliyempatia huduma na ndugu wa marehemu walioutayarisha mwili kwa ajili ya maziko na kuuona mwili huo kabla ya maziko walithibitisha haukuwa na dalili za kupigwa, kujeruhiwa wala majeraha,” imeeleza taarifa ya Tume iliyosainiwa na mwenyekiti wake huyo.

Imesema, mabaki ya chakula walichokula Nusura, mchumba wake na mpwa wake, pamoja na matapishi yaliwasilishwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi na taarifa ilionesha kutoonekana kwa dalili zozote za kuwepo kwa sumu.

Kwa upande wa ajali iliyokuwa ikihusihwa na kifo cha Nusura, Tume ya Haki za Binadamu inasema,  gari lililohusika ni aina ya Toyota Land Cruiser GXR V8 yenye namba za Usajili T454 DWV, iliyokuwa ikiendeshwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange akiwa peke yake. Gari hiyo, ni mali binafsi ya Dugange.

“Kutokana na mazingira hayo, THBUB imebaini kuwa kifo cha Nusura hakikuwa na uhusiano wowote na ajali ya gari ya Dk Dugange iliyotokea usiku wa Aprili 25, 2023,” inaeleza.

Hata hivyo, THBUB haikuthibitisha yeyote kuhusika na kifo cha Nusura kutokana na vielelezo vya Hospitali ya Faraja, Mkemia Mkuu wa Serikali na maelezo ya mengine ya mashahidi.

Tume hiyo imependekeza Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine zichukue hatua kuwabaini wanaohusika na kutoa taarifa za uongo na chonganishi zinazosababisha taharuki katika jamii.

Imetaka jeshi hilo kwa kushirikiana na mamlaka za usafiri barabarani liweke vifaa vya kiusalama barabarani kama kamera ili kubaini matukio yanayotokea.

Tume imewataka wananchi kuepuka kutoa taarifa zinazochochea chuki na kusababisha uvunjifu wa Amani.

Vilevile, tume imetaka wananchi kuendelee kuwa na imani na vyombo vya dola katika kuzuia na kupambana na uhalifu na watoe ushirikiano katika kuvisaidia vyombo hivyo kutekeleza majukumu yake.

Nusura, alifariki dunia Mei mosi katika Hospitali ya Faraja iliyopo Himo mkoani Kilimanjaro, huku mazingira ya kifo hicho yakizua utata baada ya watu kukihusisha na ajali ya naibu waziri huyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia arejesha mikopo ya 10%, bilioni 227.96 zatengwa

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amerejesha utaratibu wa utoaji mikopo...

Habari Mchanganyiko

Sekta binafsi yasifu utekelezaji wa Mkumbi

Spread the loveSERIKAL imepongezwa kwa utekelezaji wa mapendekezo ya sekta binafsi kupitia...

Habari Mchanganyiko

Kamati ya bunge yapigia chapuo kilimo ikolojia

Spread the loveSERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imeshauriwa kushirikiana na wadau wa...

Habari Mchanganyiko

Serikali yapata hasara 113 milioni hospitali kuwapa misamaha wagonjwa wasiostahili

Spread the loveSERIKALI imepata hasara ya kiasi cha Sh. 111.76 milioni, baada...

error: Content is protected !!