October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kifo cha Mkapa: Askofu Ruwa’ichi, Jenerali Waitara watoa ya moyoni

Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam

Spread the love

YUDA Thaddeus Ruwa’ichi, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Jenerali George Waitara wametoa ya moyoni kuhusu maisha ya Hayati Benjamin William Mkapa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wakati Askofu Ruwaichi akisema, Watanzania wajipange kutunza mambo mema aliyofanya Mzee Mkapa, Jenerali Waitara ambaye ni Mkuu wa Majeshi Mstaafu amesema, Rais huyo anayo alama katika utatuzi wa changamoto za jeshi.

Mkapa, Rais wa awamu ya tatu amefariki dunia usiku wa kuamkia jana Ijumaa tarehe 24 Julai 2020, hospitalini jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumza katika msiba huo leo Jumamosi tarehe 25 Julai 2020 nyumbani kwa Mkapa, Masaki jijini Dar es Salaam, Askofu Ruwaichi amesema, Tanzania kwa sasa iko katika kipindi kigumu kufuatia msiba huo mzito.

“Tunatoa pole kwa mama Anna na watoto wake, tunatoa pole kwa Rais John Magufuli na Serikali yake katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

“Naomba tunapomuombea, tujipange kutunza vyema yale mazuri yote aliyotuachia maana yeye mwenyewe aliendeleza mema,” ameshauri Askofu Ruwa’ichi.

Jenerali George Waitara, Mkuu wa Majeshi Mstaafu amesema, Rais Mkapa ameacha alama nchini Tanzania pamoja na kutatua changamoto zilizokuwa zinalikabili jeshi.

Jenerali George Waitara, Mkuu wa Majeshi Mstaafu

“Baada ya kuniapisha kuwa mkuu wa majeshi, nilimuomba anisaidie jeshi lilipokuwa na matatizo, hakusita. Nilifanya kazi chini yake, tulifanya kazi nzuri sana, huduma jeshini zilirudi,” amesema Generali Waitara.

Amesema, enzi za uongozi wake, Rais Mkapa alikuwa msikivu na mwenyekufanyia kazi ushauri wa wengine.

Lazaro Nyalandu, Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii amesema, enzi za uhai wake Rais Mkapa alikuwa mpatanishi na mwenye mapenzi kwa nchi za Bara la Afrika.

“Binafsi huyu mzee namkumbuka kwa mengi, lazima niseme mawili. Niliwahi kuwa msadizi wa mke wake na baba.”

“Nilikua karibu nao, nimesafiri nchi mbalimbali nimeona akishughulikia masuala mbalimbali na hakutaka nchi ya Zimbabwe iguswe,” amesema Nyalandu, mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati

Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki amesema, katika uongozi wake alifanya kazi kubwa katika kufufua uchumi wa nchi.

“Mwaka 1999 alisaidia sana kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo mwaka 1977 ilikufa. Ilibidi ifufuliwe mwaka 1999 Mkapa akiwa na marais wengine. Ilikua si kazi rahisi lakini alifanikiwa,” amesema Kimbisa.

Amesema, Tanzania itaukosa ushauri muhimu wa Rais Mkapa, katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020.

“Tutamkumbuka kwenye uchaguzi huu, sababu siku za kufunga kampeni ama kufungua anakuwa msemaji mzuri wa kututia moyo. Lakini ameweka mfumo mzuri. Kwenye uchaguzi alituwekea utaratibu mzuri wa kuweka kampeni za kistaarabu,” amesema Kimbisa.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana tarehe 24 Julai 2020 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, mwili wa Mkapa utaagwa kwa siku tatu mfululizo kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kuanzia kesho Jumapili hadi Jumanne Julai 28 mwaka huu.

Baada ya mwili wake kuagwa, utakwenda kuzikwa kijijini kwao Lupaso mkoani Mtwara, Jumatano tarehe 29 Julai 2020.

error: Content is protected !!