Tuesday , 23 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kifo cha Mama Kabendera: Chadema wamtumia ujumbe Rais Magufuli
Habari za Siasa

Kifo cha Mama Kabendera: Chadema wamtumia ujumbe Rais Magufuli

John Mnyika, Karibu Mkuu wa Chadema
Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemuomba Rais John Magufuli kumwacha huru Mwanaharakati Erick Kabendera, ili kuifuta machozi familia yake kufuatia kifo cha mama yake Verdiana Mujwahuzi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea). 

Wito huo umetolewa leo tarehe 3 Januari 2020 na John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema, kwenye Ibada ya Kuuaga mwili wa Mama Kabendera, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mt. Francis Xavier, Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

Mnyika amemuomba Rais Magufuli arejee ombi la Mama Kabendera, alilolitoa wiki mbili zilizopita kabla ya kifo chake, la kumuacha huru mwanaye, kwa kuwa ni tegemeo la familia yake.

“Siku chache kabla hajafariki alizungumza na vyombo vya habari, alieleza uchungu wake kwa mwanaye kuwa mahabusu gerezani. Akaeleza zaidi kwamba anamtegemea mwanaye kwenye matibabu yake. Na alimuomba Rais amuache Kabendera ili apate huduma anayostahili,” amesema Mnyika na kuongeza;

“Mama alisema maneno mazito sana kabla ya kifo chake na aliyaelekeza kwa Rais Magufuli. Akamuomba kama baba. Na mimi ninamuomba ayarejee maneno ya mama na atumie fursa hii kuifariji familia yake na kuwafuta machozi wafiwa kwa kumuacha huru Kabendera.”

Wakati huo huo, Mnyika ameiomba serikali kupitia upya sheria, ili watuhumiwa walioko mahabusu, wapate ruhusa ya kushiriki mazishi ya ndugu zao wa karibu.

“Msiba huu uwe fundisho kwa taifa. Mtu kama aliye mahabusu ambaye hajawekwa hatiani, apate nafasi ya kushiriki mazishi hata chini ya ulinzi. Wito wa Chadema, kama kikwazo ni sheria serikali ipeleke muswada bungeni ili kurekebisha. Ili kuwe na utaratibu wa watuhumiwa kiruhusiwa kuzika,” ameshauri Mnyika.

Mama Kabendera alifariki dunia tarehe 31 Desemba 2019, katika Hospitali ya Rufaa ya Amana Wilayani Ilala jijini Dar es salaam alikokuwa anapatiwa matibabu.

Na mwili wake unatarajiwa kupumzishwa katika makazi yake ya milele,  Jumatatu ya tarehe 6 Januari, mwaka huu, wilayani Bukoba mkoani Kagera.

Kabendera yuko mahabusu katika Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam, akituhumiwa kwa mashtaka ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kujihusisha na genge la uhalifu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kabendera yuko mahabusu kwa kipindi cha miezi mitano, tangu alipokamatwa mwezi Julai mwaka jana, na Jeshi la Polisi.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

error: Content is protected !!