May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kifo cha Magufuli: Chato waomba wasitelekezwe

Samuel Magambo, Mwenyekiti wa Baraza la wazee Wilaya ya Geita mkoa wa Geita (Picha kwa hisani ya Azam Tv)

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Baraza la Wazee Wilaya ya Chato mkoani Geita, Samuel Magambo, amewaomba viongozi waliobaki madarakani kutowatenga pia, kutotelekeza wilaya hiyo, badala yake ikamilishe miradi ya maendeleo iliyoasisiwa na Hayati John Pombe Magufuli (61). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Magambo ametoa wito huo leo Ijumaa tarehe 19 Machi 2021, katika mahojiano yake ya Kituo cha Runinga cha Azam Tv, kuhusu kifo cha Hayati Magufuli, kilichotokea Jumatano tarehe 17 Machi 2021.

Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassani, Hayati Magufuli alifariki dunia katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Kufuatia kifo cha Hayati Magufuli ambaye ni mzaliwa wa Chato, Mzee Magambo amewaomba viongozi waliobaki madarakani kuziba pengo la kiongozi huyo aliyoliacha Chato.

Kwa kuendeleza ujenzi wa miradi iliyoanzishwa naye, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Chato na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato.

“Tunaomba waliobaki wajaribu kuendeleza Chato inavyokwenda, mfano hospitali aliyoiacha iwe ya rufaa, namuomba Mungu watakaokuwepo waiendeleze ilete manufaa, lakini pia uwanja wetu huu hapa wa ndege na mambo mengine mengi,” amesema Mzee Magambo.

Hayati Magufuli alizaliwa Wilayani Chato mkoani Geita tarehe 29 Oktoba 1959, na aliliongoza Jimbo la Chato kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika vipindi vinne mfululizo tangu mwaka 1995 hadi 2015.

Mwaka 2015 alichaguliwa kuwa rais wa Tanzania baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

Aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Magufuli akiwa kwenye Uwanja wa ndege wa Chato enzi za uhai wake

Mbali na ombi la miradi ya Chato kutotelekezwa baada ya kifo cha Rais Magufuli, Mzee Magambo amewaomba viongozi kutekeleza miradi iliyoanzishwa na kiongozi huyo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Siwezi kusema Chato tu, ni nchi nzima, watakaoshika madaraka baada yake,” ameomba Mzee Magambo.

Mzee huyo aliyekuwa karibu na Hayati Rais Magufuli enzi za uhai wake, amesema kiongozi huyo ameacha pengo wilayani humo, ambalo halitazibika.

“Kwa kweli kwa watu wa Chato hili pengo halitazibika, ila kwa uwezo wa Mungu hatuwezi kujua maana yake tunaweza kusema hata Baba wa Taifa Hayati Mwalimu, Julius Nyerere alivyokufa tulilia hatimaye wakaja wengine,” amesema Mzee Magambo.

error: Content is protected !!