June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kifo cha Kamukara utata mtupu, Mengi, Mbowe, Kafulila wamlilia

Viongozi wa vyombo vya habari, vyama vya siasa wakiwa na majonzi siku kuaga mwili ya Marehemu Kamukara

Spread the love

UTATA umeghubika kifo cha mhariri, Edson Kamukara. Mazingira alimofia yamekosa maelezo dhahiri juu ya kilichotendeka.

Taarifa za awali zilisema alikufa kwa kuungua moto uliotokana na kulipuka kwa jiko la gesi; na kumuunguza sehemu kadhaa za mwili.

Walioingia ndani – ndugu, marafiki na majirani, hawakuona jiko lililolipuka.

Taarifa zingine zilisema alikufa baada ya kuugua malaria. Naye Kamukara alikuwa amelalamika awali kuwa “ana malaria.” Haikuthibitikika.

Pia zipo taarifa zinazosema kifo chake kilitokana na “mapafu kujaa maji.” Hakuna rekodi za daktari au mtaalamu yeyote wa eneo hilo la mwili.

Lakini maelezo ya baadaye kutoka hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam ambako kulitolewa hati ya kifo, yanasema kifo kilitokana na “mfumo wa hewa kushindwa kufanya kazi.”

Vilevile haikuelezwa ni kitu gani hasa kilisababisha mfumo wa hewa ushindwe kufanya kazi.

Utata unatokana na kauli zinazosigana za majirani; akiwemo Abdala Hamis, afisa habari wa chama cha ACT-Wazalendo.

Hamis na Kamukara walikuwa wanaishi katika jengo la ghorofa moja, Mabibo mwisho. Kamukara alikaa ghorofani.

Hamis alidai kuwa wakati Kamukata anakumbwa na “maradhi,” hakuwa nyumbani; lakini alipigiwa simu na mkewe, ambaye pia hakuwa nyumbani, akimweleza kuwa Kamukara ni mgonjwa sana; na kwamba yeye (mke) alipewa taarifa na mdogo wake aliyekuwa amemwachia mtoto nyumbani.

Taarifa nyingine zinasema Kamukara alifia kwenye ngazi za ghorofa hilo wakati majirani wakijaribu kumpeleka hospitali; na kwamba hiyo ilikuwa baada ya mshikamshike ya kumkamata kwani alikuwa hakubali kuguswa.

Naye Kamukara, katika mawasiliano yake ya awali simu ya mkononi kwa njia ya sms (gazeti linayo), alimwandikia mmoja wa waandishi wa habari akiwa Bukoba:

“Mama hajambo. Mimi nilifika huku nikaumwa hoi. Kifua kinabana; wakati mwingine kupumua kwa shida. Ila kuna baridi balaa. Lakini nimekwenda hospitali nikapewa dawa. Nasubiri nirudi nifanye vipimo vikubwa (22 Juni).”

Kamukara alikuwa ameomba likizo ya wiki moja kwenda Bukoba kumuona mama yake, Justina Kamukara. Alikuwa amepelekewa taarifa (Kamukala) kuwa mama ni mgonjwa.

Utata unazidi pale ndugu na marafiki walioingia nyumbani kwa Kamukara, wanaporipoti kuwa kulikuwa na damu iliyotapakaa sebuleni – ukutani na sakafuni na katika chumba chake cha kulala.

Taarifa za baadhi ya ndugu zinasema Kamukara alikutwa na “jeraha kubwa” kichwani – upande  wa kushoto. Hayakupatikana maelezo yoyote juu ya jeraha hilo; wala maswali kutoka kwa wanafamilia.

Kamukara alifariki Magharibi ya Alhamisi 25 Juni wiki iliyopita. Alikuwa mhariri wa gazeti la MwanaHALISI linalochapishwa kwenye mtandao wa intaneti (MwanaHALISI Online).

Katika mazishi hayo, kama ilivyokuwa jijini Dar es Salaam, 26 Juni mwaka huu, wakati wa kuaga mwili wake katika viwanja vya Leaders’ Club, mamia ya ndugu, marafiki na wananchi kwa jumla, walifurika kuomboleza kifo cha mwandishi kijana.

Waliofika katika viwanja vya Leaders’ Club jijini Dar es Salaam kuaga mwili wa Kamukara ni pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT) na mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Wengine ni Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Sued Kagasheki; Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa; Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Nevile Meena, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na mwakilishi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Deogratius Temba.

Katika viwanja vya Leaders’ Club baadhi ya wadau wa habari walieleza namna walivyomfahamu Kamukara.

Alikuwa Mengi aliyesema, “… watu wengi wanamung’unya maneno wanapozungumzia mazuri ya Edson. Ukweli ni kwamba, hata katika siku za karibuni kama wiki mbili tatu zilizopita Edson alikuwa na habari kubwa sana.”

“Alitambua kwamba ile habari ingeweza kuhatarisha maisha yake. Hata alipewa ahadi kwamba kama angeacha kuandika ile habari angepata mamilioni. Lakini kijana wetu aliamua kuandika na kutochukua fedha,” alisema Mengi.

Mengi alieleza kuwa Kamukara “…hakuwa mpokeaji wala mtoaji rushwa. Sio kweli kwamba, mishahara midogo ndio inawafanya watu kuchukua rushwa. Kamukara alikuwa kijana wa kawaida. Rushwa ni tabia ya mtu.”

Naye Mbowe alimwita Kamukara “Kamanda;” hii ni kutokana na Kamukara alivyowajibika na kujituma kama mpambanaji kwa manufaa ya taifa.

Alisema,  “Kamanda Edson ametutoka katika kipindi kigumu…ni kipindi tete ambacho kinategemea uimara na uthabiti wa tasinia ya habari,” alisema Mbowe.

Akizungumza kwa niaba ya CUF, Bwire alisema, “Kamukara hakuwa na woga katika habari ambazo wanahabari wengine watahisi kwamba zinaweza kuwaumiza. Yeye aliweza kuandika kwa sababu aliangalia Watanzania wanataka nini…”

Deogratius Temba alikuwa rafiki wa karibu wa Kamukara. Anasimulia katika Facebook yake, Juni 26 mwaka huu, “…alipokuja Dar es Salaam kutafuta kazi nilimkaribisha na kuishi naye chumba kimoja, Ilala, Bungoni.

“…..tuliishi wote chumba kimoja na kulala kitanda kimoja kwa muda wa miaka miwili. Hiyo ilikuwa kati ya mwaka 2008 na 2010,” aliandika Temba na kuongeza kuwa anakumbuka harakati zao za kuhakikisha sauti za wanyonge zinasikika.

Neville Meena alisema, “Edson Kamukara alitarajiwa kubeba majukumu makubwa katika vyumba vya habari. Tulimtazama kama mtu ambaye ataongoza vyombo vyetu vya habari katika siku zijazo kutokana na uwezo, msimamo, mtizamo na fikira zake.”

Akiongea na mwandishi wa habari hii, Jumatatu wiki hii kwa njia ya simu, David Kafulila, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR – Mageuzi) alisema Kamukara alikuwa mwenye haiba ya uadilifu, ukomavu wa mawazo, mwenye huruma, upendo na utu.

“Kamukara alishikilia bango, akisaidiwa na kijana mwenzake Josephat Isango, la kuhakikisha gazeti la Tanzania Daima linakomalia ufisadi katika Akaunti ya Tegeta Escrow,” alisema Kafulila. 

“Siamini kama ni wao wamekudhulumu uhai; wala siamini kama ni wenye hofu ya ndoto yako ya kutumikia taifa hili kwa kuanzia ubunge mwaka huu! Naamini bado uchunguzi unahitajika ili kupata ukweli halisi,” amesema Kafulila.

Kamukara alizaliwa kiijijini Ihangiro, 27 Machi 1980. Ana shahada ya uandishi wa habari kutoka Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT) kilichopo jijini Mwanza.

error: Content is protected !!