February 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kifo cha Akwilina, Polisi ‘hawachomoki’

Spread the love

RISASI iliyokatisha maisha ya mwanafunzi wa chuo cha usafirishaji cha taifa (NIT), jijini Dar es Salaam, Akwilina Akwilini, huenda ilifyatuliwa na askari wa jeshi la polisi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akwilina, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa NIT, aliuawa kwa risasi Ijumaa iliyopita, maeneo ya Mkwajuni, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Kifo cha binti huyo wa miaka 22, kilitokana na hatua ya askari polisi kuwafyetulia risasi za moto, wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika vurugu hizo, zilizotokea Ijumaa ya tarehe 16 Februari, watu wengine kadhaa wamejeruhiwa kwa risasi na wanaendelea na matibabu katika hospitali ya taifa ya Muhimbili (MNH).

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alikiri kuwa Akwilina amekufa kwa risasi, lakini akadai huenda risasi hiyo imerushwa na waandamanaji wa Chadema.

Alisema, “…tunaendelea na upepelezi. Kwa kuwa waandamaji walikuwa na silaha za jadi na walilenga kuwajeruhi polisi, adhima ambayo waliitimiza, basi upo uwezekano kwamba wao pia walitumia silaha za moto ambayo imesababisha kifo cha mwanafunzi huyo.”

Mambosasa amesema, jeshi lake lililazimika kutumia silaha za moto, ili kuwatawanya viongozi wakuu wa Chadema na wafuasi wao, waliokuwa wakielekea kwenye ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Kinondoni.

Hatua ya viongozi hao, kuelekeza wafuasi wao kwenda kwa msimamizi huyo wa uchaguzi, Aron Kagurumjuli, ilitokana na hatua yake ya kugomea fomu za viapo na barua za utambulisho kwa mawakala wa Chadema.

Chadema walianza kutembea kutoka uwanja wa Buibui, Kinondoni, muda mfupi baada ya mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara.

Polisi walianza kukabiliana na wafuasi wa Chadema, katika eneo la Mkwajuni, ambapo askari polisi kadhaa waliokuwa kwenye magari zaidi ya matano, walitanda na kuweka vizuizi barabarani.

Barabara ambayo iliwekwa vizuizi na jeshi hilo, ni ile inayotoka Morocco kwenda Magomeni; na barabara zote mbili zinazotumiwa na mabasi yaliyoko kwenye mradi wa mwendo kasi.

Miongoni mwa magari yaliyotumika kuziba barabara hizo, ni pamoja na lile yenye Na. PT 2093 na PT 4117 ambalo lilibeba maji ya washawasha.

Barabara inayotumia magari yanayotokea Magomeni kwenda Morocco, ziliachwa wazi. Gari iliyombeba Akwilina ilikuwa ikitokea Mabibo kwenda Makumbusho na hivyo ilitumia barabara ya Magomeni –Morocco.

Polisi waliokuwa mbele ya waandamanaji, mbele ya kituo cha mwendokasi cha Mkwajuni, ndio waliofyatua mabomu ya machozi na risasi za moto kuelekea upande wa waandamanaji.

Wakati polisi wakitawanya waandamanaji kwa silaha za moto, magari yanayotokea Magomeni yaliendelea kupita.

MwanaHALISI linaripoti kuwa kuna uwezekano mdogo mno kwa waandamanaji kurusha risasi na kumpata Akwilina ambaye alikuwa kiti cha nyuma cha gari aliyokuwa amepanda.

Risasi iliyomuua mwanafunzi Akwilina na iliyomjeruhi kichwani Abbas Abdallah, kondakta wa daladala ya Mabibo – Makumbusho – ilirushwa kutoka upande wa kutokea Magomeni na kuingia ndani kupitia kioo cha nyuma cha daladala hiyo.

Wakati haya yanatokea, waandamaji walikuwa hawajalipita gari ambalo Aqulina alipanda, jambo ambalo linathibitisha madai kuwa risasi hiyo ilirushwa na mtu aliyekuwa nyuma ambako ndiko walikokuwa polisi.

Waandamaji walikuwa mbele wakitazamana na polisi na magari yanayotokea Magomeni.

Mwandishi wa habari hizi alikuwapo eneo la tukio. Alikuwa miongoni mwa waliokamatwa na polisi, kwa madai ya kuwapiga picha za picha mnato na (video), wakati wanawakabili waandamanaji.

Mchoro unaonesha eneo la tukio alipopigwa risasi Akwilima Akwilini
Mchoro unaonesha eneo la tukio alipopigwa risasi Akwilima Akwilini

Kwa mantiki rahisi, kama wangekuwa wanarusha risasi basi zingeipiga daladala hiyo katika sehemu yake ya mbele au ubavuni – kulia na siyo kwenye kioo cha nyuma.

Laiti polisi wangetaka kuwakabili waandamaji pekee kwa silaha za moto (jambo ambalo si sahihi pia) wangeweza kuweka kizuzi ili magari na pikipiki zisiendelee kupita kutokea upande wa Magomeni kuelekea Mwananyamala.

Hata hivyo, waliacha magari hayo yapite huku wakiendelea kurusha risasi za moto na mabomu, jambo lililosababisha baadhi ya madereva wa pikipiki kuanguka kwa mshituko na hata wengine kutelekeza pikipiki zao.

Ushahidi mwingine unaonesha kuwa risasi za mto zilikuwa zikitokea upande waliokuwa wakitokea polisi, ni kwamba waandamanaji waliojeruhiwa kwa risasi, wote walipigwa risasi zikitokea upande wa Magomeni.

Kama waandamanaji walikuwa na silaha za moto na risasi iliyomuua Akwilina ilitoka kwao, basi waandamanaji hao walikuwa upande mmoja na polisi na walikuwa wamechanganyika nao, jambo ambalo halikuonekana.

Tangu kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo, makundi kadhaa ya wanaharakati, vyama vya siasa, viongozi wa madhehebu ya kidini na asasi za kiraia, zimekuwa zikitoa wito kwa serikali kuunda tume huru kuchunguza tukio hilo.

Aidha, Mtandao wa Wanafunzi Tanzania umelaani mauaji hayo na kumtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kujiuzulu mara moja ili kuonesha uwajibikaji kutokana na tukio hilo.

error: Content is protected !!