WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo amesema, wanafunzi 73,101 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Jafo amesema, wanafunzi hao watatakiwa kuripoti shuleni tarehe 18 Julai 2020 ili kuanza masomo tarehe 20 Julai 2020.
Waziri Jafo ameyasema hayo leo Jumatano tarehe 17 Juni 2020 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema, miongoni mwa wanafunzi waliochaguliwa wanafunzi 1,572 wakiwemo wasichana 685 na wavulana 887 wamechaguliwa kujiunga na shule za vipaji maalumu wakiwamo wanafunzi wanne wavulana wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wa vyuo, Waziri Jafo amesema, wanafunzi 9,264 wakiwemo wasichana 4,314 na wavulana 4,950 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya ufundi, vyuo vya afya na vyuo vya ualimu katika ngazi ya stashahada.
Waziri Jafo ametoa agizo kwa wanafunzi kuhakikisha wanaripoti katika kipindi cha wiki mbili tangu tarehe ya kufungua shule.
Leave a comment