October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kichaa cha Mbwana tishio kwa watoto

Spread the love

UGONJWA wa kichaa cha mbwa umetajwa kuwa tishio kwa watoto wenye umri chini ya miaka 15. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo tarehe 28 Septemba 2019, siku ambayo dunia inaadhimisha ugonjwa wa kichaa cha mbwa. 

Taarifa ya wizara hiyo inaeleza kwamba, asilimia 30 hadi 50 ya waathirika wa kichaa cha mbwa barani Afrika,  ni watoto chini ya umri wa miaka 15.

“Inakadiriwa  kuwa, kati ya asilimia 30 hadi 50 ya waathirika wa kichaa cha mbwa, ni watoto chini ya miaka 15,” inaeleza taarifa hiyo.

Wizara ya afya imeeleza kwamba, tafiti zinaonesha kuwa watoto wa rika hilo huathirika zaidi, kutokana na wengi wao kuwa karibu na mbwa hasa wanaofugwa.

“Tafiti zimeonesha waathirika wakuu wa ugonjwa huu ni watoto chini ya miaka 15, kwa saabu wao ndio wanaokuwa karibu zaidi na mbwa (anayefugwa). Na pia hupenda kucheza na kuchokoza mbwa wasiowafahamu njiani,” imeeleza taarifa ya Wizara ya Afya.

Aidha, wizara ya afya imesema takwimu zinakadiria kwamba ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa husababisha  vifo 59,000 kila mwaka duniani, ambapo kati ya vifo hivyo, asilimia 36 hutokea barani Afrika.

“Mwaka huu 2019, kuanzia mwezi Januari hadi Agosti, watu 16,290 wametolewa taarifa ya kuumwa na mbwa na vifo 8 vimeripotiwa kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa.  Hata hivyo, tatizo la kichaa cha mbwa ni kubwa zaidi ya takwimu hizi.

Kwani hazijumuishi vifo vinavyotokea nyumbani na waathirika ambao hawakufika katika vituo vya kutolea huduma za afya,” inaeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema mwaka 2019, ulitokea mlipuko wa ugonjwa wa kichaa cha mbwa katika Halmashauri za Wilaya ya Ulanga na Malinyi, ambapo watu 292 waliumwa na mbwa na kati yao 4 walipoteza maisha.

“Katika kudhibiti mlipuko huu, kupitia Dawati la Afya Moja, Wizara ya Mifugo ilipata chanjo 16,000 kwa ajili ya kuchanja mbwa.  Zoezi la kuchanja mbwa lilitekelezwa Mwezi Aprili hadi Mei, 2019.  Aidha, Elimu ya kujikinga dhidi ya kichaa cha mbwa ilitolewa kwa shule za msingi na viongozi wa kata,”  imeeleza taarifa hiyo.

Kufuatia changamoto hiyo, wizara ya afya imetoa wito kwa jamii kuchukua hatua za haraka juu ya mtu aliyeathirika na kichaa cha mbwa, ikiwemo kumuwahisha katika kituo cha afya au hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

“Endapo mtu ataumwa na mbwa, hatua ya kwanza muhimu ni kuosha jeraha kwa dakika 10 au zaidi kwa maji mengi yanayotiririka na sabuni.  Kidonda kisifungwe.  Kisha apelekwe haraka katika kituo cha kutolea huduma za afya ili kupata chanjo ya kichaa cha mbwa.

“Mtu aliyeumwa na mbwa awahi kwenda kituo cha kutolea huduma za afya na kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo, na ni muhimu kumaliza dozi.  Wizara imekwisha kutoa maagizo kwa mikoa na Halmashauri kuhakikisha kuwa chanjo hizi zinakuwepo katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya wananchi watakaohitaji,”  inaeleza taarifa hiyo.

Wizara ya Afya, imewataka wananchi wanaofuga mbwa, kuwadhibiti ili wasidhurule ovyo kuepusha maambukizi ya kichaa cha mbwa.

“Mbwa wafungiwe ndani wakati wa mchana na wasiachwe kuzurura hovyo, kwani wanaweza kupata maambukizi endapo watakutana na mnyama aliyeambukizwa. Kuhakikisha mazingira yote ni safi, ili kutowapa chakula mbwa wanaozurura mtaani na kuzoea kuja katika mazingira tunamoishi,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, wizara ya afya imeitaka jamii kutoa elimu kwa watoto sambamba na kuwakataza kutochokoxa mbwa wasiowajua.

error: Content is protected !!