May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kibatala atumia Biblia mahakamani kuwatetea kina Mbowe

Spread the love

 

KIONGOZI wa Jopo la Mawakili wa Utetezi, Wakili Peter Kibatala, katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, ametumia vifungu vya Biblia kuwatetea wateja wake katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).

Wakili Kibatala ametumia Biblia kuwatetea wateja wake leo Ijumaa, tarehe 28 Januari 2022, akimuuliza maswali ya dodoso shahidi wa 12 wa Jamhuri, Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Denis Urio, mahakamani hapo mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo yenye mashtaka sita ya ugaidi, ni waliokuwa makomando wa JWTZ, Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Wakili Kibatala alimuomba Luteni Urio asome kitabu cha Yohana sura ya nane mstari wa 31 hadi 39 na Waefeso sura ya nne mstari wa 25 hadi 32, ambapo shahidi huyo alisoma vifungu hivyo.

Baada ya kusoma vifungu hivyo, Wakili Kibatala alimuuliza shahidi vimebeba ujumbe gani, ambapo alijibu akidai, vinaelekeza usiogope bali sema kweli, huku ujumbe mwingine alidai unaelekeza tusameheane pamoja na kusema kweli.

Wakili Kibatala alimuuliza shahidi huyo kama anafahamu maisha ya Mbowe na wenzake yanazungukwa na ushahidi wake, ambapo alijibu akidai kuwa anafahamu ingawa yako mikononi mwa mahakama.

Katika ushahidi wake mkuu alioutoa juzi akiongozwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula, Luteni Urio alidai mahakamani hapo kuwa, Mbowe alimuelezea mipango yake ya kupanga njama za kufanya vitendo vya ugaidi, alipokutana naye ana kwa ana Julai 2020, maeneo ya Mikocheni, Dar es Salaam.

Alidai kuwa, kabla ya kuonana na Mbowe, mwanasiasa huyo alimpigia simu akimtaka waonane, ambapo alimkatalia na kumuomba azungumze naye kwenye simu, ombi lililokataliwa na Mbowe.

Luteni Urio amedai, baada ya Mbowe kukataa kuzungumza naye kwenye simu, mwanasiasa huyo alimuomba wakutane, ndipo walipokutana akamueleza mipango hiyo.

Shahidi huyo wa Jamhuri anadai kuwa, alipokutana na Mbowe, alimuomba amtafutie makomandoo wa JWTZ, waliofukuzwa kazi au kustaafu, ili wamsaidie katika harakati za chama chake kuchukua dola 2020, kwa gharama yoyote ile.

Ikiwemo kudhuru viongozi wanaonekana kuwa kikwazo kwa vyama vya upinzani. Kulipua vituo vya mafuta na maeneo yenye mikusanyiko ya watu, kufanya maandamano yasiyo na kikomo.

Pia kukata miti iliyoko pembezoni mwa barabara kisha kuyapanga magogo katika maeneo hayo, lengo ni kuzua taharuki kwa jamii na kuonesha Serikali imeshindwa.

Luteni Urio pia alisoma meseji anazodai alitumiwa na Mbowe mahakamani hapo, zinazoomesha namna alivyompa maelekezo ya kuwatafuta makomando wa kutekeleza mipango hiyo, lakini pia namna alivyomtumia pesa za kuwaratibu na kuwafikisha kwake jijini Dar es Salaam.

Shahidi huyo anaendelea kutoa ushahidi wake.

error: Content is protected !!