December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kibatala amkwamisha mteja wake Mbowe

Spread the love

WAKILI wa utetezi, Peter Kibatala amekwamisha kesi ya uchochezi inayomkabili Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa na wenzake. Anaripoti Faki Sosi…(endelea).

Wakili huyo hakutokea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo tarehe 30 Agosti 2019, kuendelea na shauri hilo bila kuwepo taarifa rasmi inayomuhusu.

Kutokana na kutokuwepo kwake, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ameahirisha kesi hiyo kwa kuwa, Wakili Kibatala ndiye aliyetakiwa kumhoji shahidi wa Jamhuri kwenye shauri hilo la jinai namba 112 la mwaka 2018.

Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Dk.Vicent Mashinji, Katibu Mkuu-Taifa; John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu – Bara na Salumu Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu -Z’Bar.

Pia Ester Matiko Mbunge wa Tarime Mjini; Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

Upande wa Jamhuri leo umeongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi; Dk. Zainab Mango na Wakili Mwandamizi, Simon Wankyo, Jackline Nyantori  na Salim Msemo. Upande wa utetezi umeongozwa na Prof. Abdallah Safari na Hekima Mwasipu.

Kwenye kesi hiyo, leo ilitarajiwa shahidi huyo wa saba ambaye ni Ofisa wa Uchaguzi Manispaa ya Kinondoni, aendelee kuhojiwa juu ya ushahidi wake.

Awali, upande wa utetezi uliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa kueleza kuwa, Wakili Kibatala aliyekuwa akitarajiwa kumaliza eneo lake la kumuhoji shahidi juu ya ushahidi alioutoa mahakamani hapo, bado anaendelea na shauri la jinai kwenye Mahakama Kuu.

Kauli hiyo imeelezwa na Prof. Safari na kwamba Wakili Kibatala aliitwa kwa (Summons) juu ya kesi hiyo tangu jana tarehe 29 Agosti 2019.
Prof. Safari ameieleza mahakama hiyo, wao walimaliza eneo lao la kumuhoji shahidi.

Baada ya saa moja na nusu, Hakimu Simba alirejea kwenye chumba cha mahakama ya wazi namba mbili (ilikuwa saa 8:05 mchana), ambapo Prof. Safari aliieleza mahakama kuwa wamemtafuta Wakili Kibatala bla mafanikio.

Wakili Nchimbi alitoa nyaraka iliyotoka Mahakama Kuu iliyoonesha kesi aliyokuwa akiendesha Wakili Kitala jana, iliahirishwa jana ile ile na kwamba taarifa za kuwa yupo Mahakama Kuu ni uongo. Ameomba mahakama kutoa karipio kwa Wakili Kibatala.

Prof Safari: Tumemtafuta, hatujampata yawezekana kuna kitu kimemsibu, hakuja ni vizuri awepo aulizwe kwanini hakuja. Shahidi aondoke, tutaendelea na mashahidi wengine akirejea tutamuita.

Nchimbi: ombi la utetezi ni kwamba wakili huyo yupo Mahakama Kuu kitu ambacho sio kweli, sisi tumeona kuwa wameiongopea mahakama. Tunaiomba itoe karipio.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Simba alitoa uamuzi wa kuarisha shauri hilo hadi tarehe 10, 11 na 12 Septemba 2019.

error: Content is protected !!