June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kibatala adai hati mpya kesi ya ‘walioidukua NEC’

Spread the love

UPANDE utetezi  katika kesi inayowakabili wataalamu wa teknolojia na mawasiliano, wanaotuhumiwa kusambaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kabla ya kuthibitishwa na Tume ya Uchaguzi (NEC), umeitaka Mahakama kufuta hati ya mashtaka baada ya kufariki kwa mshitakiwa namba saba katika kesi hiyo, anaandika Faki Sosi.

Mshitakiwa aliyefariki ni Jose Nim, raia wa Ufaransa ambapo watuhumiwa wengine ni Mashinda Mtei, mkazi wa Tengeru Arusha, Julius Mwita, Mkazi wa Magomeni Dar es Salaam, Frederick Fussi, mkazi wa Mbezi Dar es Salaam, Julius Matei, raia wa Kenya, Meshack Mlawa, Mkazi wa Keko na Anisa Rulanyan, mkazi wa Kawe.

Mbele ya Respecious Mwijage Hakimu Mkazi Mkuu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Peter Kibatala, wakili wa utetezi ameiomba mahakama hiyo itoe muda kwa upande wa Jamhuri kurekebisha hati ya mashtaka ya awali kutokana na hati hiyo kumtambua mtuhumiwa namba saba ambaye kwa sasa ni marehemu.

Shauri hilo lilifika mahakamani hapo kwa ajili ya maelezo kwa watuhumiwa (facts).

Kesi hiyo namba 267 ya mwaka 2015 ina mashitaka matatu ambayo ni pamoja na kutoa taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii wakati wakijua kuwa hazijathibitishwa.

Shitaka la pili linamkabili Matei na Nim, ambapo wanadaiwa kuwa Oktoba 26, 2015, wakiwa katika hoteli ya King iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam wakiwa na hati za kusafirilia zenye namba A1532119, na M7687807 walijiingiza katika ajira ya kukusanya na kusambaza matokeo ya urais ya uchaguzi mkuu kwa niaba ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinyume na sheria.

Shitaka la tatu linamkabili Julius Matei pekee yake ambaye ni raia wa Kenya mwenye hati ya kusafirilia namba A1532119, anadaiwa kuwa akiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam alijihusisha na biashara katika Saccos ya Wanama bila kibali.

Kesi hiyo imeahirishwa mpaka tarehe 31 Oktoba, 2016 ambapo mahakama hiyo itatoa uamuzi juu ya hoja za wakili wa upande wa utetezi.

error: Content is protected !!