January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kibanda: Waandishi tunalengwa

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda

Spread the love

NI imani kubwa ya Jukwaa la Wahariri wa Tanzania (TEF) kwamba Jeshi la Polisi nchini lilipanga makusudi kudhalilisha waandishi wa habari kwa kipigo.

Mwenyekiti wa Jukwaa, Absalom Kibanda amesema kilichotokea Makao Makuu ya Polisi, askari kupiga waandishi wa habari waliokuwa kazini, hata kidogo hakikuwa kitendo cha “bahati mbaya.”

“Tunajua na huu ndio ushahidi wetu, waandishi walionesha vitambulisho vya kazi kwa wakubwa wa Polisi… walilengwa makusudi ili kuwakomoa,” amesema.

Kibanda alieleza hayo siku moja baada ya askari wa kikosi cha kuzuia ghasia (FFU) kujeruhi waandishi kwa kipigo wakati walipokuwa wakifuatilia kuitwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Polisi (DCI), kwa mahojiano kuhusu kauli aliyoitoa hivi karibuni kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho.

Waandishi wa habari waliojeruhiwa katika tukio hilo, ni Josephat Isango wa kampuni ya Free Media, Shamim Ausi wa gazeti la Hoja na Yusuph Badi wa kampuni ya Tanzania Standard Newspaper (TSN) ambayo ni ya serikali.

“Kwa maana hiyo, tukio hili linathibitisha kwamba polisi wamekuwa wakitushambulia kwa makusudi sisi waandishi wa habari… wanatekeleza maelekezo ya wakubwa zao. Ndio kusema wanapata baraka za viaongozi wao,” anasema.

Kibanda alijenga hoja kwa kutumia tukio la Septemba 2 mwaka jana, ambapo askari wa kikosi hicho cha FFU walimuua Daud Mwangosi kwa kumpiga risasi za mipira.

Mwangosi, mwandishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, aliuliwa wakati akiwa katika kazi pale polisi walipokuwa wakitaka kuzuia viongozi wa Chadema kufika eneo la kufungua tawi la chama hicho, kijiji cha Nyololo, nje kidogo ya mji mdogo wa Mafinga.

Mwangosi alimiminiwa risasi kwa kutumia bunduki ya kufyatulia mabomu ya machozi wakati wa vurugu. Polisi aliyehusika alitekeleza ukatili huo akiwa karibu na Mwangosi, kitendo kinachoelezwa kitaalamu kama cha kukusudia kumdhuru aliyelengwa.

Kibanda alisema kwa kuwa Mwangosi alipigwa akiwa mikononi mwa Polisi, mbele ya Kamanda wa Polisi Mkoa Michael Kamuhanda ambaye baadaye alipandishwa cheo, na safari hii wakipiga waandishi baada ya kujitambulisha kwa vitambulisho vya Idara ya Habari MAELEZO, huwezi kusema ni bahati mbaya.

Mwangosi alipigwa alipokuwa anawaeleza polisi kuwa waliyekuwa wanampa kipigo cha “mbwa mwizi,” Godfrey Mushi, ni mwandishi wa habari.

Ripoti za uchunguzi wa tukio hilo, ikiwemo ile iliyoandaliwa na timu ya wahariri chini ya udhamini wa Jukwaa hilo, zilithibitisha kuwa matumizi ya silaha hiyo yanapaswa kuwa kwa hatua hata ya mita 150.

Kibanda alisema matukio hayo yameonesha dhahiri namna Polisi wanavyotumia vibaya silaha kudhuru waandishi wa habari katika kuonesha walivyo na chuki nao.

“Kiashiria kingine kinachotuonesha kwamba polisi wamekuwa wakijenga uadui na vyombo vya habari, ni hatua ya polisi ya kutoshiriki kwa namna yoyote katika mkutano baina ya vyombo vya habari na vile vya ulinzi na usalama ambako Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal alikuwa mgeni rasmi.

Katika mkutano huo ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Dk. Bilal alihimiza vyombo vya dola kujenga ushirikiano mzuri wa kikazi kwa kuwa ushirikiano wao unasaidia kufanikisha kazi ya kujenga nchi.

“Ndugu zangu juzi tu tulikuwa na mkutano muhimu ambao viongozi wa polisi walialikwa. Sio tu viongozi wa jeshi la polisi hawakuhudhuria, hawakutuma hata wawakilishi,” alisema Kibanda na kusisitiza:

“Mnaona wamepiga na kujeruhi waandishi wenzetu, wala hawajasema chochote. Tunataka uongozi uchukue hatua dhidi ya askari waliohusika kuwapiga waandishi. Ukimya wao utakuwa ni ujumbe kwetu kwamba tukio lilipangwa mapema.”

Isango, aliyekuwepo kwenye mkutano wa uongozi wa Jukwaa, uliofanyika Hoteli ya Belmonte, jijini, ameiambia MwanaHALISI Online, kwamba alipigwa baada ya kuwa amejitambulisha na kutoa kitambulisho chake.

“Walifukuza watu kwa kutumia mbwa wao, huku wakiwapiga. Wakanigeukia mimi na kunipiga miguu na mikononi na kunitishia mbwa… wametufanyia unyama kwa makusudi, walitujua ni waandishi wa habari,” alisema.

Isango amesema anaamini jeshi la polisi linatumika vibaya kwa kujiingiza katika siasa.

error: Content is protected !!