July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kibamba: Mchakato wa Katiba Mpya usimame

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Deus Kibamba

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Deus Kibamba (kulia) akizungumza na waandishi wa habari juu ya kusimamishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya

Spread the love

JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA), limetaka kusitishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya hadi hapo utakapomalizika uchaguzi mkuu wa mwaka kesho.

Deus Kibamba, mwenyekiti wa JUKATA amewaambia waandishi habari jijini Dar es Salaam, kwamba ni muhimu mchakato huo kusimamishwa kwa sasa, ili kuwezesha taifa kupata katiba itakayoridhiwa na pande zote.

“Kwa utaratibu wa sasa, mara baada ya Katiba Mpya kupatikana, madai mapya ya katiba yataibuka. Hii ni kwa sababu, katiba inayotafutwa sasa, haitakidhi matakwa ya wananchi,” ameeleza Kibamba.

Amesema badala ya kuhangaika na zimwi ambalo litaweza kuangamiza nchi, ni vema serikali ikatumia muda huu uliosalia kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka kesho, kufanyia marekebisho baadhi ya sheria muhimu nchini.

Ametaja sheria hizo kuwa ni pamoja na muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC); sheria ya jeshi la polisi, sheria ya uchaguzi; sheria ya uchaguzi wa serikali za Mitaa, Sheria ya gharama za Uchaguzi na mgombea binafsi.

Amesema ili marekebisho hayo ya sheria yaweze kupita kiurahisi bungeni, amependekeza kuundwa Kamati Maalum itakayoshirikisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), NEC na vyama vya siasa.

Miswada yote hii itaandaliwa na kupelekwa katika bunge la Novemba 2014 kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya kwanza kabla ya wadau kutoa yao na kupitishwa rasmi Februali 2015.

Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi chini (1992), NEC imekuwa ikilalamikiwa kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wagombea wake.

Aidha, Kibamba ametaka uchaguzi wa Serikali za Mitaa nao usitishwe kwa sasa na kushauri ufanyike kwa pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Uchaguzi huu unasimamiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia. Huyu ni kada wa CCM na mbunge wa chama hicho. Hivyo basi, ni vema uchaguzi huu ukasimamiwa na Tume huru ya uchaguzi itakayoundwa,” ameeleza.

https://twitter.com/Profesy/status/492625668921114625

Akizungumzia umuhimu wa kuwapo Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika mchakato wa Katiba Mpya, Kibamba amesema, “Tume ya Mabadiliko ya Katika iendelee kufanya kazi mpaka kukamilika kwa zoezi la kura ya kura ya maoni. Hii itasaidia kuondoa mkanganyiko wa kujadili vifungu ambavyo havimo kwenye Rasimu iliyoko bungeni.”

“Tangu mwanzo tulikubaliana Tume ya Warioba ifanye kazi hii hadi mwisho wa mchakato. Lakini kulifanyika maamuzi potofu ya kuiondoa tume katika mchakato huu. Tunataka tume irejee na ifanye kazi yake ya kikatiba ya kufafanua rasimu,” amesisitiza Kibamba.

error: Content is protected !!