July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi za uchaguzi kuamliwa ndani ya miezi nane

Spread the love

IKIWA zimebaki siku chache kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, Majaji wametakiwa kuhakikisha kila shauri la pingamizi litakalofunguliwa ambalo linalohusu masuala ya uchaguzi mwaka huu liamuliwe kwa muda unaotakiwa. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Kauli hiyo ilitolewa na Jaji Kiongozi, Shaban Lila katika semina ya siku mbili kwa majaji inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ajili ya kuwajengea uwezo majaji hao kusikiliza mashauri yanayotokana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.

Alisema inawezekana kesi hizo zikaamuliwa kwa muda muafaka ili kuweka kumbukumbu sawa na si lazima wafike mwaka mmoja bali itawezekana kuamuliwa ndani ya miezi nane ili kujenga heshima ya Mahakama.

“Kisheria kanuni zetu zinatuambia kila shauri litakalofunguliwa lisikilizwe na kuamuliwa ndani ya mwaka mmoja na kama mwaka mmoja litakuwa bado halijaamuliwa basi Jaji Mkuu atawasiliana na Waziri wa sheria na katiba na kuongeza muda wa miezi sita, kwa hiyo muda ni mwaka mmoja na nusu shauri liwe limeamuliwa, lakini tunaweza kuamua hata kabla ya mwaka mmoja,” amesema Jaji Lila.

Jaji huyo amesema baada ya hapo kama shauri linapitiliza muda basi litakuwa limekufa lenyewe na Jaji Mkuu Othman Chande amesisitiza wasifike huko na kutaka yaamuliwe kwa muda muafaka.

“Niliwasomea ujumbe mfupi wa simu (sms) majaji kutoka kwa Jaji Mkuu Othman Chande ambaye anasema mafunzo haya ni muhimu sana inabidi tujipange kiukweli mwaka huu na mashauri yote yaamuliwe kwa muda muafaka,” amesema Jaji Lila

Alibainisha Jaji Chande alikuwa anamaanisha kuwa katika miaka ya nyuma kwa mfano 2010 mashauri saba yalishindwa kuamuliwa ndani ya muda husika, hivyo anataka wahakikishe kila shauri litakalofunguliwa mwaka huu liamuliwe kwa muda unaotakiwa.

Amesema inawezekana kuamuliwa ndani ya miezi nane mara baada ya kufunguliwa kwa kesi ya kupinga matokeo.

“Kisheria baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa watu wanapewa siku 30 kuwasilisha mapingamizi yao mahakamani ya kupinga matokeo, pia sheria inatoa siku 14 kwa mtu kuomba mahakamani kama anauwezo wa kuweka fidia ya gharama kwa mwenzake na baada ya hayo mpaka siku kupangwa kesi kusikilizwa ni siku 14 zingine, ukijumlisha haya yote utakuta hayazidi miezi mitatu.

Aliongeza: “Kama mambo yote yatakamilika kwa muda wa miezi mitatu basi usikilizwaji unaweza kufanyika ndani ya miezi mitatu ikafika sita na kama watazidiwa wataongeza miezi miwili kwa yale yatakayoshindikana kwa miezi sita iwe nane wawe wamemaliza.”

Hata hivyo Jaji Lila aliwataka wanasiasa kufuata taratibu na kanuni za uchaguzi ili kuondokana na aina yoyote ya ukiukwaji wa haki za uchaguzi.

Amesema hali hiyo itaondoa migogoro na kupunguza idadi ya mashauri yatakayofunguliwa mara baada ya Uchaguzi Mkuu.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Jaji Lila amesema baadhi ya mafunzo ya awali walifanya tathmini kuangalia kama yalikidhi kiu na mahitaji ya majaji, lakini ikabainika kuna mahitaji ya kufanya mafunzo zaidi na kuwaomba UNDP kutoa mafunzo tena.

Amesema majaji 35 wa Mahakama Kuu kati ya 84 watapatiwa mafunzo ya jinsi ya kushughulikia maeneo manne yanayohusu migogoro ya uchaguzi.

“Lengo ni kupitia maeneo halisi ambayo kila siku yanakwenda mahakamani kama yenye migogoro na maeneo husika ni yale yanayohusiana na kampeni chafu, rushwa kwenye kampeni, kushawishi watu kupiga kura au kumpigia mtu kura na maeneo ya uhesabuji kura, ujazaji wa fomu za matokeo, kwa hiyo haya ni maeneo ambayo tumewaleta majaji hapa kujifunza vizuri,” amesema Jaji Lila.

Amesema mafunzo hayo wamepewa ili kukabiliana na aina ya migogoro hiyo kama itatokea katika uchaguzi ili waweze kukabiliana nayo kwa kutumia sheria na maamuzi mbalimbali ya mahakama za hapa nchini na nje zilivyoshughulikia maeneo hayo yenye matatizo yalipojitokeza.

Amesema hali hiyo itasaidia kukabiliana nayo mapema na kuyaamua mapema kwani watakuwa wamekiandaa vizuri kuamua kesi za aina hiyo.

error: Content is protected !!