August 12, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Yerricko Nyerere ‘yapigwa kalenda’

Spread the love

KESI ya kuchapisha machapisho ya upotoshaji na uchochezi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, inayomkabili kijana Yerricko Nyerere imeahirishwa kutokana na kutokuwepo kwa hakimu anayesikiliza kesi hiyo, anaandika Faki Sosi.

Respecious Mkeha ndiye hakimu anayesikiliza kesi hiyo ambapo katika hatua ya sasa, upande wa Jamhuri ulipanga kupeleka mashahidi wake katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, linapoendeshwa shauri hilo.

Yeriko ambaye alidaiwa kuwa, Oktoba 25, 2015 katika eneo lisilojulikana alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook akiandika, “piga kura leo huku ukikumbuka kifo cha Mwangosi, mateso ya Ulimboka na Kibanda, mateso ya kijana wetu wa JKT. Ukikumbuka hayo fanya uamuzi sahihi bila ushabiki.”

Pia anadaiwa kuwa, Oktoba 24, 2015 mshtakiwa huyo alichapisha taarifa za uongo kupitia mtanda wa Facebook akiandika, “siku ya leo mpaka siku ya kuapishwa Lowassa, taifa hili halihitaji amani bali taifa hili linahitaji haki tu, amani ilishatoweka siku nyingi, kilichosalia ni uvumilivu tu.”

Yerricko pia anadaiwa kuchapisha taarifa nyingine iliyosema, “Uchaguzi huu ni vita, anayedhani ni demokrasia apimwe akili. Hii ni vita kati ya umma na dola, ni vita kati ya wema na ubaya, ni vita kati ya shibe na njaa , ni vita kati ya masikini na matajiri, CCM si chama cha siasa kwa sasa ni muungano wa kihalifu unaolindwa na baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola.”

Oktoba 24, 2015 pia, kijana huyo anadaiwa kuchapisha taarifa zingine katika mtandao wa Facebook akieleza kuwa, “Umma umekosa amani na furaha, fursa pekee waliyoipata watanzania ni kwenda kumchagua rais wao kesho (Oktoba 25).

Jaribio lolote litakalofanywa na CCM na vibaraka wao la kukwamisha matakwa ya umma litaondoa hata ule uvumilivu kidogo walionao watanzania na kisha vitazaliwa vichaa chongo ambavyo hata risasi na mabomu hayatavizima.

Aidha, taarifa nyingine iliyochapishwa na Yerricko na hatimaye kusababisha kushitakiwa kwake, ni ile iliyosema, “mipango ya hujuma ya JK toka Ngurdoto Arusha muda huu. Yupo na wakuu wote wa mikoa na wilaya Tanzania nzima pia wakuu wa vyombo vya dola na wanadhimu mbalimbali.

“Wakuu wa mikoa wanaelezwa kuwa, NEC kwa kushirikiana na CCM tayari wameshatengeneza kura bandia kwa kutumia mfumo wa kalamu za kichina.”

Yerricko anashitakiwa kwa jumla ya makosa matano, akidaiwa kutenda kinyume na sheria ya makosa ya mitandao iliyotungwa na kupitishwa na Bunge la Tanzania Februari mwaka jana kuelekea uchaguzi mkuu.

Kesi hiyo itasikilizwa tena tarehe 5 Oktoba, mwaka huu. Ambapo itaendelea katika hatua ya upande wa mashitaka kuanza kutoa ushahidi wake juu ya mashitaka hayo.

error: Content is protected !!