February 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya vigogo Chadema yaiva

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepanga kuanza kusikiliza kesi ya jinai inayowakabili viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Vigogo hao wa chama kikuu cha upinzani nchini, wako mahakamani wakikabiliwa na makosa kadhaa ya jinai, ikiwamo kufanya mkusanyiko usiokuwa halali na kusababishia mauwaji Akwilina Akwiline, aliyekuwa mwanafunzi katika chuo cha usafirishaji cha taifa (NIT).

Tukio hilo limetokea tarehe 20 Februari 2018, siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Kinondoni.

Mahakama imepanga kuanza kusikiliza shauri hilo mfululizo kuanzia tarehe 31 Julai mwaka huu.

Kesi hiyo Na. 112 ya mwaka 2018 inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Wilbard Mashauri.

Hakimu Mashauri, amefikia maamuzi hayo, kufuatia upande wa mashitaka uliongozwa na wakili mkuu wa serikali, Faraja Nchimbi, kuiambia mahakama kuwa upande wa jamhuri uko tayari kwa ajili ya usikilizaji wa shauri hilo.

Nchimbi ameiomba mahakama kupanga siku ya usomaji wa maelezo ya awali na baadaye kuanza kusikiliza mfululizo kesi hiyo. Upande wa mashitaka umeahidi kuwasilisha mahakamani orodha ya mashahidi wake na kuongeza kuwa watafika mbele ya mahakama kama ambavyo watahitajika.

Awali washitakiwa hao, wanaongozwa na mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, walikuwa wamewasilisha Mahakama Kuu, maombi ya marejeo, kupinga shauri hilo kusikilizwa na mahakama ya Kisutu.

Wengine kwenye kesi, ni katibu mkuu wa chama hicho, Dk. Vicent Mashinji; manaibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Bara, John Mnyika.

Wengine, ni mbunge wa Iringa Mjini na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, Peter Msigwa; mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Victoria na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha) na mbunge wa Kawe, Halima Mdee na mbunge wa Bunda Mjini na mjumbe wa kamati kuu, Esther Bulaya.

Katika shauri hilo Na. 126 /2018, Mbowe na wenzake waliiambia mahakama kuwa shitaka linalowakabili, limeangukia kwenye haki za msingi za kikatiba.

Mahakama imetupilia mbali maombi hayo kwa maelezo ya kuwa “yamewahishwa mahakamani.”

Hata hivyo, washitakiwa tayari wamewasilisha mahakamani kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi huo wa mahakama kuu.

Akizungumza mbele ya Hakim Mkuu Mkazi Mashauri, wakili wa utetezi, Nashon Nkungu, aliiambia mahakama kuwa licha ya ombi lao la marejeo kutupwa na mahakama kuu, wateja wake tayari wameweka nia ya kukata rufaa na wameshawasilisha mahakamani kusudio hilo.

Akaiomba mahakama ya Kisutu kutosikiliza shauri lililopo mbele yake hadi hapo rufaa hiyo itakaposikilizwa.

Hata hivyo, baada ya majibizano ya hoja hizo, Hakimu Mashauri amepanga usikilizwaji wa awali kufanyika tarehe 30 Julai mwaka huu.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 13 ya jinai, ikiwamo kufanya mkusanyiko usio halali; kusababisha ghasia, kukiuka agizo la kuwataka kutawanyika na kusababisha uvunjifu wa amani.

error: Content is protected !!