June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya padre Mushi mtegoni

Mwili wa marehemu Evarist Mushi ukipelekwa makaburini tayari kwa kuhifadhiwa.

Spread the love

OKTOBA 3 mwaka huu inaweza kuwa siku ya mwisho kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) wa Zanzibar kutoa kisingizio cha kutokamilika kwa upelelezi wa kesi ya mauaji ya Padre Evarist Mushi kwani jaji anayeisikiliza amesema hawezi kuridhia kisingizio hicho.

Jaji Omar Othman Makungu amesema kesi hiyo kwa namna mwenendo wake ulivyo, haistahili tena kuwepo mahakamani. Anahofia kuwa inaweza kuendelea hivyo hata upande wa mashitaka ukipewa miaka miwili mingine.

Kauli yake hiyo, ilimaanisha kwamba hata yeye haoni kama mtuhumiwa anatendewa haki katika kesi hiyo kwa kuwa ikiwa imeshatajwa mara 22, bado upande wa mashitaka unasema upelelezi haujakamilika. Amepata hofu zaidi pale aliposhindwa kuona angalau ratiba ya namna uplelezi unavyoendelea ili labda ijulikane kwamba ni lini upelelezi huo unaweza kukamilika.

Kesi hiyo iliyoko mbele ya Mahakama Kuu Zanzibar, ilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Aprili 16, mwaka jana.

Omar Mussa Makame, mwenye umri wa miaka 36, alisomewa mashitaka ya kudaiwa kumuua Padre Mushi wa Kanisa Katoliki, Makao Makuu Shangani, mjini Zanzibar. Mauaji hayo kwa njia ya risasi yalitokea Februari 17, miezi miwili kabla.

Lakini hadi Septemba 3, kesi hiyo ilipoitwa kwa mara ya 22, bado DPP ameendelea kuomba kesi iahirishwe kwa sababu ya kilichoelezwa kuwa “upelelezi bado haujakamilika.”

Siku hiyo pia, kama ilivyokuwa huko nyuma kesi inapotajwa na kuombwa iahirishwe, Mwanasheria Abdalla Mgongo kutoka ofisi ya DPP, hakuwa na maneno mengi mahakamani.

“Mheshimiwa Jaji Mkuu kesi hii imekuja tena kwa kutajwa. Na ninaomba iahirishwe na kupangiwa tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa sababu upelelezi wake bado haujakamilika,” alisikika akiieleza mahakama iliyojaa wasikilizaji akiwemo mke wa mtuhumiwa pamoja na familia na rafiki zake.

Maelezo hayo ya mwanasheria kutoka serikalini, hayakuridhisha jopo la mawakili wanaomtetea mtuhumiwa, ambalo linaongozwa na Abdalla Juma, wakili maarufu Zanzibar.

Alipinga maelezo hayo na kutaka mahakama ifikirie sasa kuifuta kesi na kumuachia huru mteja wake ili aende kufanya shughuli zake za kuhangaikia maisha ambazo, alidai kuwa zinazorota kutokana na masharti ya dhamana yanayombana.

Omar, mwenye umri wa miaka 35, mkaazi wa Rahaleo, mjini Zanzibar, ambaye ni kiongozi wa kada za katikati wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyegombea uwakilishi wa jimbo la Rahaleo, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, yuko nje kwa dhamana.

Utetezi wake unaofanywa na jopo la mawakili wanaoongozwa na Abdalla Juma, umeibana serikali kwamba imeshindwa kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo, na kwa sababu, haina mpango madhubuti unaoelezwa kuwa unaonesha wamefikia hatua gani, hakuna sababu ya kung’ang’aniza kesi ibaki mahakamani.

Wakili huyo akishikilia hoja hiyo mbele ya Jaji Makungu Jumatano ya Septemba 3, kesi ilipoitwa kwa kutajwa ikiwa ni mara ya 22 tangu ifikishwe mahakamani, alieleza kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) wa Zanzibar hana uwezo tena wa kukamilisha upelelezi.

Alihoji kwamba sababu iliyotolewa na mwanasheria wa serikali si miongoni mwa sababu madhubuti hasa kwa vile haijaelezwa upalelezi utakamilika lini.

Akasihi mahakama kuu isitumike kumnyima haki ya kuwa huru mteja wake kwa kuwa inayo mamlaka ya kuifuta kesi na kumwachia huru mteja wake huyo, uamuzi aliosema hauna maana ya kuzuia kesi hiyo kuja kufunguliwa tena pale upelelezi utakapokuwa umekamilika.

“Wakili wa serikali ameshindwa kuieleza mahakama yako majibu ya uchunguzi wa vinasaba yatakuwa yamerejeshwa lini. Hawajui kwa sababu hakuna kinachosubiriwa. Naomba mahakama ilitambue hili na iamue kuifuta kesi hii… haina maana kwamba ikitakiwa kesi hii haitafunguliwa tena. Atakuja tu mteja wangu. Naomba aachiwe huru ili aendele na shughuli zake za kimaisha,” alieleza.

Mwanasheria kutoka Ofisi ya DPP, Abdalla Mgongo alishikilia hoja yake ya awali, na iliyozoeleka sasa, kuwa mahakama iiahirishe kesi na kupanga siku nyingine wakati upelelezi ukisubiriwa kukamilika.

Mwanasheria Mgongo alieleza kwamba vielelezo vilivyopelekwa Tanzania Bara kwa ajili ya uchunguzi havijapatikana matokeo yake. Aliomba kesi ipangiwe siku nyingine ya kutajwa.

Alipokuwa akijibu hoja za Wakili Juma, alieleza kuwa si kweli kuwa hawana programu ya vipi upelelezi unafanywa. Kwake anachokijua ni upelelezi kufanywa, sema tu wao sio wanaoshughulikia upelelezi huo bali ni polisi.

Alimbana wakili wa mtuhumiwa kutaja kifungu cha sheria kinachoishurutisha mahakama iingie katika kuifuta kesi kwa sababu alizozitaja wakili wa mtuhumiwa. “Kama upelelezi haujakamilika huwezi kusema kesi itakwendaje. Siwezi kuingilia kusema ni lini upelelezi utakamilika.”

Wakili Juma alipoomba kujibu hoja hiyo, alieleza kuwa kifungu hicho hakipo katika vitabu vya sheria za Zanzibar, lakini akafafanua mahakama inao uhuru wa kufanya hivyo kwa kuangalia mantiki ya hoja zake.

“Hakuna kifugu hicho. Lakini maelezo ya upande wa mashitaka yanathibitisha hakuna hatua ya maana ya kukamilisha upelelezi wa kesi. Mwanasheria wake ameshindwa kuieleza mahakama ratiba ya lini upelelezi utakamilika, tena ameeleza kwamba si wao wanaofanya upelelezi huo isipokuwa ni polisi.”

“Sasa si inatosha kuamini hakuna kinachopelelezwa. Ndo maana naomba mahakama ichukue uamuzi wa haki kufuta kesi,” alieleza.

Jaji Makungu baada ya kusikiliza hoja za pande hizo mbili, na yeye kutaka maelezo ya kutosha kutoka kwao, alisema analiona tatizo la upande wa mashitaka kushindwa kueleza bayana ni lini upelelezi utakamilika. Anakiri pia kwamba kesi hiyo ina muda mrefu inaishia kutajwa tu.

“Ni kweli si vizuri kuacha kesi tu ikitajwa mara 22 hii maana yake inaweza kuendelea hivyo kwa miaka miwili wakati tayari haistahili sasa kuwepo mahakamani. Ninatoa nafasi ya mwisho kwa upande wa mashitaka kuja kueleza ni lini upelelezi utakamilika, vinginevyo nitakuwa sina namna bali kuifuta kesi na kumuachia mshitakiwa,” alisema.

Jaji Makungu aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 3 itakapotajwa tena. Tangu Aprili 5 kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza, kufikia Septemba 3, ilipoitwa mara ya mwisho, imetimiza mwaka mmoja na nusu (miezi 16) na siku 19.

Mtuhumiwa anadaiwa kumuua kwa makusudi Padre Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Februari 17, 2013. Padre Mushi alipigwa risasi tatu ikiwemo ya kwenye paji la uso wakati akiwasili kwa gari kwenye Kanisa la Mtakatifu Teresa la Beit el Ras, nje kidogo ya mjini Zanzibar.

Mtuhumiwa ambaye alikamatwa kutokana na mchoro wa mkono ulioandaliwa na makachero wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), anashitakiwa chini ya vifungu 196 na 197 vya Sheria Na. 6 ya mwaka 2004 ya Zanzibar.

error: Content is protected !!