April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Membe: Musiba aangukia pua

Cyprian Musiba

Spread the love

PINGAMIZI tatu zilizowasilishwa na Cyprian Musiba, katika kesi namba 220/2018 iliyofungliwa na Bernard Membe, zimetupiliwa mbali. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam leo tarehe 27 Desemba 2019, imetupilia mbali maombi hayo huku ikitoa sababu tatu za kufikia uamuzi huo.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji De Mello na kusomwa na Msajili R. Massam mbele ya mawakili wa pande zote mbili.

Mahakama hiyo imeeleza, malalamiko ya mdai yalitakiwa kufikishwa katika Baraza la Habari kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Hoja ya pili ya mahakama hiyo imeeleza, kwamba katika pingamizi hizo, hakuna kesi ya msingi dhidi ya waidaiwa.

Na hoja ya tatu imeeleza, kesi ya msingi inakiuka kanuni 6, kanuni ndogo ya 3 ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Madai.

Pingamizi za Musiba na wenzake, yalifikishwa kwenye mahakama hiyo tarehe 03 Oktoba 2019. Kwenye kesi hiyo, Membe anawakilishwa na wakili Jonathan Mndeme.

Membe ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya awamu ya nne, amemshitaki Musiba anayejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Rais John Magufuli, kwamba amemchafua kupitia vyombo vyake vya habari.

Wengine walioshitakiwa kwenye kesi hiyo, ni pamoja na mhariri wa gazeti la Tanzanite na wachapishaji wa gazeti hilo. Kwenye mashitaka hayo, Membe anataka kulipwa Sh. 10 bilioni.

Kesi hiyo imepangwa kuendelea kusikilizwa tarehe 31 Machi, 2020.

error: Content is protected !!