Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe yaunguruma Mahakama ya ufisadi 
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Mbowe yaunguruma Mahakama ya ufisadi 

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na wenzake wakiwa mahakamani
Spread the love

 

KESI ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya kula njama za kufanya ugaidi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, inaendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Kesi hiyo inasikilizwa leo Ijumaa, tarehe 3 Septemba 2021, mbele ya Jaji Elinazer Luvanda, ambapo Jopo la Mawakili  upande wa Jamhuri, wakiongozwa na Mawakili wa Serikali waandamizi, Robert Kidando akisaidiana na Nassoro Katuga,  wamewasilisha hoja kinzani dhidi ya mapingamizi matatu, yaliyowekwa na Mawakili wa Utetezi, juzi Jumatano.

Jumatano tarehe 1 Septemba 2021, Mawakili wa Mbowe na wenzake, waliwasilisha mapingamizi hayo, wakipinga washtakiwa wao wasisomewe hati ya mashtaka kwa madai kwamba, ni batili kutokana na kuwa na mapungufu kisheria.

Wakijibu pingamizi la hati ya mashtaka kutoonesha nia ya washtakiwa kutenda kosa, mawakili hao wa Jamhuri wamesema haina nguvu kisheria, wakidai mahakama hiyo ina uwezo wa kutoa tafsiri iwapo mashtaka yaliyomo katika hati hiyo, ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia Ugaidi.

Katika pingamizi hilo, mawakili wa Mbowe walitaka wateja wao waachwe huru, wakidai hawawezi kusikiliza kesi wakati kosa halipo. Wamedai shtaka la kwanza, tatu, nne na la sita, hayana vigezo vya kuwa makosa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia Ugaidi.

Katika pingamizi dhidi ya mashtaka kujirudia katika hati hiyo, mawakili wa Jamhuri wameipinga wakidai hayajajirudia.

Mawakili hao wa Jamhuri wameiomba mahakama hiyo watupilie mbali mapingamizi hayo.

Baada ya jopo hilo la mawakili wa Jamhuri kumaliza kuwasilisha hoja zao kinzani, Jaji Luvanda alitoa mapumziko ya dakika 30, ambapo baadae mawakili wa utetezi watamalizia kutoa hoja zao.

Inatarajiwa kuwa, mahakama hiyo ikimaliza kusikiliza hoja za pande zote mbili dhidi ya mapingamizi hayo, itatoa tarehe ya siku ya kutoa uamuzi.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Halfani Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Lingwenya.

Mbowe na wenzake wanashtakiwa kwa mashtaka sita , ikiwemo la kula njama za kufanya ugaidi na shtaka la kutaka kudhuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya,  yanayowakabili wote.

Na shtaka la kufadhili vitendo vya ugaidi,  kwa kutoa fedha za kufadhili ugaidi, linalomkabili Mbowe peke yake.

Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya makosa hayo kati ya tarehe 1 hadi 5 Agosti 2021, katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na  Morogoro.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!