Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe yaibua dosari sheria ya ugaidi
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Mbowe yaibua dosari sheria ya ugaidi

Spread the love

 

KESI ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, imeibua dosari katika sheria ya kuzuia ugaidi, baada ya kushindwa kutoa uamuzi katika pingamizi moja kati ya matatu, yaliyowasilishwa na washtakiwa hao. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mapingamizi hayo yaliwasilishwa Jumatano iliyopita na Mawakili wa Utetezi wakiongozwa na Peter Kibatala, akisaidiana na Jeremiah Mtobesya.

Ni katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Uhujumu Uchumi, wakipinga wateja wao kusomewa hati ya mashtaka kwa madai ni batili, kutokana na kuwa na upungufu kisheria.

Mapingamizi hayo yalikuwa ni, makosa kujirudia katika hati ya mashtaka, hati hiyo kutoeleza nia ya washtakiwa kutenda kosa na sheria iliyotumika kuwashtaki Mbowe na wenzake, kutotafsiri makosa ya ugaidi.

Leo Jumatatu, tarehe 6 Septemba 2021, kabla ya kujitoa kusikiliza kesi hiyo, Jaji Elinaza Luvanda, alishindwa kutoa uamuzi dhidi ya pingamizi la sheria hiyo ya ugaidi, kwamba imeshindwa kutafsiri matendo ya ugaidi.

Na kuwaelekeza mawakili wa pande zote warejee taarifa rasmi za Bunge (Hansard), kuhusu michango ya wabunge wakati wanachangia muswada uliotunga sheria hiyo.

“Majibu yanaweza kupatikana katika hansard ya Bunge ya michango ya wabunge, kuhusu muswada wa sheria hiyo, kama nilivyosema jambo hili linachukua muda. Kimsingi sitapenda kuhitimisha katika hatua ya awali.”

“Badala yake nitaacha uwazi kwa pande zote kutoa ufafanuzi hapo baadae. Hivyo hoja hiyo naiachia hapa,” amesema Jaji Luvanda.

Awali, Mawakili wa utetezi waliomba mahakama hiyo iwafutie mashtaka wateja wao, wakidai hakuna kosa la msingi baada ya sheria hiyo kushindwa kutafsiri makosa ya ugaidi, kama sheria za nchi nyingine zinavyofanya.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Halfani Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Lingwenya.

Lakini Jaji Luvanda alipinga hoja hiyo akisema, kila nchi inatengeneza sheria zake kulingana na mazingira yake.

“Marejeo yanatakiwa yafanywe katika maazimio ya Bunge ya kutunga sheria ya ugaidi, kuona kwa nini walizuia kuweka tafsiri ya vitendo vya kigaidi kwa kuunganisha siasa, dini na itikadi,

“Ninahisi Bunge lilitafakari na kuangalia mazingira ya jamii zetu, dhidi ya miongozo iliyotolewa ili kuzuia haki kutotendeka,” amesema Jaji Luvanda.

Jaji Luvanda amesema “maoni yangu Bunge halikuchagua kufuata mrengo wa mataifa mengine waliyochukua, kutafsiri matendo ya ugaidi bila kuhusisha siasa, dini na itikadi. Kwa maneno mengine haitoshi kusema sisi mfumo wetu wa kisheria unafafanana na nchi tatu ili tuwe sawa.”

Mbali na kuliweka kiporo pingamizi hilo, Jaji Luvanda alitupilia mbali mapingamizi mengine na kuuelekeza upande wa mashtaka kuifanyia marekebisho hati ya mashtaka katika maelezo ya shtaka la kwanza, nne na la sita.

“….nakubaliana na hoja (pingamizi) ya kwanza kuhusu changamoto ya kosa la kwanza, nne na la sita, kwamba makosa yaliyofunguliwa chini ya kifungu cha nne, waendesha mashtaka kutotumia baadhi ya maneno,” amesema Jaji Luavanda na kuongeza:

“….nakubaliana na Kibatala hayo maneno yangewekwa ili kuweka mpaka kati ya shauri la ugaidi na makosa ya jinai. Nawaelekeza upande wa Jamhuri ufanye mabadiliko katika kosa la kwanza, nne na la sita.”

Baada ya Jaji Luvanda kutoa maamuzi ya pingamizi hilo, alijitoa kusikiliza kesi hiyo, kufuatia maombi ya Mbowe na wenzake yaliyotaka ajitoe kwa madai hawana imani naye.

Hivyo, Jaji Luvanda aliiahirisha usikilizwaji wa kesi hiyo hadi itakapopangiwa jaji mwingine.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaKimataifa

Mwanaye rais jela miaka miaka 6 kwa dawa za kulevya

Spread the loveMwanawe rais wa zamani wa Guinea-Bissau amehukumiwa kifungo cha miaka...

Habari za SiasaTangulizi

Mapya yaibuka wamasai waliohamishwa Ngorongoro kwenda Msomera

Spread the loveMAPYA yameibuka kuhusu zoezi la Serikali kuwahamisha kwa hiari wamasai...

Habari MchanganyikoTangulizi

Baba aomba msaada kuzika miili ya familia yake iliyofunga bila kula kuonana na Mungu

Spread the loveWAKATI Mamlaka nchini Kenya, ikiendelea kukabidhi miili ya watu waliofariki...

Habari za Siasa

Rais Samia ampongeza mpinzani aliyeshinda urais Senegal

Spread the loveRAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amempongeza mwanasiasa wa...

error: Content is protected !!