November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe yaahirishwa, kesi ndogo kuunguruma kesho

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano mkoani Dar es Salaam, imeahirisha usikilizwaji wa kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, hadi kesho tarehe 10 Novemba 2021, kwa ajili ya kuanza usikilizaji wa kesi yake ndogo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kesi hiyo ya msingi imeahirishwa leo Jumanne, tarehe 9 Novemba 2021, na mahakama hiyo mbele ya Jaji Joackim Tiganga, baada ya kesi hiyo ndogo kuibuka kufuatia mapingamizi ya utetezi, dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Adam Kasekwa, yaliyoletwa mahakamani hapo na shahidi wa nane wa jamhuri, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, SP Jumanne Malangahe.

Mapingamizi hayo yaliibuka baada ya SP Malangahe kuiomba mahakama hiyo iipokee nyaraka ya maelezo hayo, kama sehemu ya ushahidi wa upande wa mashtaka.

Katika hoja za upande wa utetezi, walidai Ling’wenya hakuwahi kuchukuliwa maelezo hayo kama ilivyodaiwa na SP Jumanne, kwamba aliyachukua baada ya kumhoji tarehe 7 Agosti 2020, Katika Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam.

Mawakili wa utetezi walidai kuwa, Ling’wenya alilazimishwa kusaini nyaraka ya maelezo hayo kwa kupewa mateso ya kisaikolojia. Na kwamba hakuisoma kujua kilichomo ndani yake.

Kufuatia mapingamizi hayo, upande wa jamhuri kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, uliiomba mahakama hiyo ianzishe kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, ili itoe uamuzi wa kisheria dhidi yake.

Awali akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, kutoa ushahidi wake, SP Jumanne alidai, alichukua maelezo hayo ya onyo ya Ling’wenya, tarehe 7 Agosti 2020, Katika Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam.

SP Jumanne alidai, alimpa haki zote Ling’wenya kabla ya kumhoji ikiwemo kumueleza kuwa anaonywa kwa kosa la kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi hivyo halazimishwi kutoa maelezo yake pamoja na pia na haki ya kuwa na mwanasheria au ndugu wakati anahojiwa.

Afisa huyo wa Polisi alidai, alimuonya mtuhumiwa huyo kuwa, maelezo hayo yatatumika mahakamani kama ushahidi.

error: Content is protected !!