Wednesday , 8 February 2023
Home Gazeti Tangulizi Kesi ya Mbowe, wezake: Mke wa mshtakiwa ‘tuliwatafuta waume zetu hadi mochwari hatukuwaona’
Tangulizi

Kesi ya Mbowe, wezake: Mke wa mshtakiwa ‘tuliwatafuta waume zetu hadi mochwari hatukuwaona’

Spread the love

 

LILIAN Furaha Kibona, mke wa mshtakiwa wa pili, Adam Kasekwa, ameieleza Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumi Uchumi, Dar es Salaam, namna alivyomtafuta mume wake bila mafanikio katika vituo vya polisi na mochwari. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Ametoa ushahidi huo leo Jumatano, tarehe 29 Septemba 2021, mahakamani hapo mbele ya Jaji Mustapha Siyani, akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Utetezi John Mallya.

Ni katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake.

Liliana amedai, baada ya kutopata mawasiliano ya mume wake, Kasekwa na mwenzie Mohammed Ling’wenya waliokwenda Moshi mkoani Kilimanjaro kikazi, alianza kutafuta mawasiliano ya mke wa Ling’wenya kujua nini kinaendelea.

Shahidi huyo amedai, baada ya kupata mawasiliano ya mke wa Ling’wenya aliyopewa na rafiki wa mume wake, aliyemtaja kwa jina la Shikunzi, aliwasiliana naye ambapo alimtaka atoke nyumbani kwake Chalinze mkoani Pwani, kuja Kimara mkoani Dar es Salaam.

Amedai, baada ya kufika nyumbani kwa mke wa Ling’wenya, maeneo ya Kimara, walimtafuta mke wa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Halfan Bwire Hassan, ambaye aliwataka wafike nyumbani kwake Temeke mkoani Dar es Salaam.

Lilian amedai, tarehe 13 Agosti 2020, akiwa na wenzake walianza zoezi la kuwatafuta waume zao ambao walikuwa hawajulikani walipo tangu tarehe 5 Agosti 2020.

Amedai, waliwatafuta katika vituo vya polisi vya Chang’ombe, Oysterbay, Tazara na Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, ambapo baada ya kutaja majina yao askari polisi waliyatafuta katika madaftari bila kuyaona.

Baada ya kutowaona katika vituo vya polisi, Lilian amedai kesho yake, tarehe 14 Agosti 2020, waliwatafuta katika Hospitali za Amana, Muhimbili na Mwananyamala, bila mafanikio.

Amedai, walifika hospitalini hapo na picha za waume zao kwa ajili ya kuwatafuta, na kuwa walifanya zoezi hilo katika wodi za hospitali hizo hadi mochwari (vyumba vya kuhifadhia maiti), lakini hawakuwaona.

Akiongozwa na Wakili John Mallya, Lilian amedai alilazimika kuoneshwa maiti zizliokuwamo mochwari moja baada ya nyingine, ili kumtambua mume wake lakini hakumuona.

Alipoulizwa na Wakili Mallya nini kilifuata baada ya kuwakosa katika maeneo hayo.

Lilian amedai, kutokana na uhaba wa nauli wenzake walimwambia arudi nyumbani kwake Chalinze mkoani Pwani, kisha wao wataendelea kuwatafuya. Amedai alifanya hivyo ila aliendelea kuwasiliana nao.

Amedai, waliamua kuwatafuta katika maeneo hayo, wakihisi huenda hawapatikani kwa kuwa walipata ajali.

Aidha, amedai mke wa Ling’wenya alimueleza kwamba wifi yake aliyemtaja kwa jina la Asma aliyekuwa anaishi Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, alimueleza kwamba waume zao walikamatwa na Jeshi la Polisi, mkoani humo.

Wakili Mallya alimuuliza taarifa za mahali alipo mume wake alizipata wapi, alijibu akidai alizipata kupitia taarifa ya habari ya saa 2.00 usiku iliyorushwa na ITV.

Amedai, taarifa hiyo ya habari ilisema mume wake na wenzake, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wanatuhumiwa kwa kesi ya ugaidi na uhujumu uchumi na kwamba wanarudishwa mahabusu ila hawakujua mahabusu gani.

Lilian amedai, baada ya kupata taarifa hiyo, aliwasiliana na wenzake kwa lengo la kufuatilia wako mahabusu gani.

Amedai, baba yake Ling’wenya alikuja Dar es salaam, akitokea Mtwara, wakati yeye akiwa Chalinze. Ambapo mzee huyo akiwa na mke wa Ling’wenya, walikwenda mahabusu ya Gereza la Keko, hawakuwaona na walipoenda mahabusu ya Gereza la Segerea, waliwakuta.

Wakili Mallya alimuuliza alichukua hatua gani baada ya kujua wako mahabusu, Lilian amejibu akidai, Jumatatu alikwenda Segerea lakini hakufanikiwa kumuona mume wake kwa kuwa ilikuwa siyo siku ya kuona wafungwa, akaelekezwa aende Jumamosi au Jumapili.

Amedai, alipofika Segerea siku ya Jumamosi, alimuona mume wake akiwa na hali mbaya kiafya tofauti na alivyotoka nyumbani kwake kuelekea Moshi.

Amedai, alivyofika gereza la Segerea na kutaja jina la mume wake, alisikia askari wakisema ni yule jamaa ambaye yupo kabatini.

Lilian amedai, alipoletwa alimwona akitembea kwa tabu kama vile inaonekana ameteswa.

Amedai, alimwona mme wake alikuwa amekonda sana na macho yameingia ndani kama yameganda, amekonda kwa kweli na pia alimwona akiwa na alama kwenye mkono wakati anakwenda Moshi alikuwa hana.

Shahidi anaendelea kutoa ushahidi

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Bunge lalia msongamano wa mizigo bandari Dar es Salaam

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji...

Habari MchanganyikoTangulizi

Haya hapa majina 12 ya familia moja waliofariki kwenye ajali Tanga

Spread the love  MAJINA 12 kati ya 17 ya waliofariki dunia katika...

Habari za SiasaTangulizi

Vigogo wanaokwamisha mradi Liganga na Mchuchuma kitanzani

Spread the love  NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Zungu, watu wanaokwamisha utekelezaji...

Habari MchanganyikoTangulizi

Hii hapa kauli ya Sheikh mpya mkoa wa Dar

Spread the loveSAA chache baada ya kuteuliwa kukaimu nafasi ya aliyekuwa Sheikh...

error: Content is protected !!