October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe, wenzake yaibua mapya

Spread the love

 

KESI ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, imechukua sura mpya baada ya taarifa za washtakuwa wawili kukinzana na za upande wa Jamhuri. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Wakati mashahidi wa jamhuri wakidai watuhumiwa hao, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya, baada ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu Kituo kikuu cha Polisi Moshi, Kilimanjaro na kusafirishwa hadi kituo kikuu cha polisi Dar es Salaam, washtakiwa hao wamekana kufikishwa kituoni hapo.

Leo Jumanne, tarehe 28 Septemba 2021, Ling’wenya ameieleza Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, kwamba hakuwahi kufikishwa Kituo cha Polisi cha Kati cha Dar es Salaam.

Ling’wenya ambaye ametoa madai hayo mbele ya Jaji Mustapha Siyani, akiongozwa kutoa ushahidi wake katika kesi ndogo ya kesi hiyo, na Wakili wa utetezi, Nashon Nkungu.

Wakili Nkungu alimuuliza Ling’wenya kama anamfahamu Detective Msemwa na kama aliwahi kuwapokea kituoni hapo, ambaye amejibu akisema hamfahamu na wala hakuwa fikishwa kituo kikuu cha Polisi Dar es Salaam bali alifikishiwa Tazara na baadaye kupelekwa Mbweni.

 

Hivi karibuni wakati anatoa ushahidi wake kwenye kesi hiyo ndogo, akiongozwa na Mawakili wa Jamhuri, Detective Msemwa, alidai yeye aliwapokea watuhumiwa hao aliokabidhiwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Arusha, ACP Ramadhan Kingai.

Kisha, alidai aliwasajili katika Detention Register (kitabu cha mahabusu), ambacho alikionesha mahakamani hapo na kupokelewa kama sehemu ya kielelezo cha ushahidi wa jamhuri.

Wakili Nkungu alimuuliza mshtakiwa huyo kama aliwahi saini Detention Register, kama ilivyodaiwa na shahidi huyo wa jamhuri alipokuwa anatoa ushahidi wake, ambaye amejibu akidai hakufanya hivyo.

Ling’wenya na Kasekwa, waliokamatwa na Jeshi la Polisi, maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro, tarehe 5 Agosti 2021, wakati waaatoa ushahidi wao, walidai baada ya kufikishwa Dar es Salaam, waliwekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi cha Tazara kisha kuhamishiwa Kituo cha Polisi Mbweni, mkoani humo.

Kesi hiyo ndogo imetokana na pingamizi la utetezi dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Kasekwa, wakipinga yasitumike mahakamani kama ushahidi wa jamhuri kwa madai yalichukuliwa kinyume cha sheria.

Shahidi anaendelea kutoa ushahidi wake…

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!