Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe, wenzake; Shahidi akiri kuruhusu matumizi ya risasi za moto
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Mbowe, wenzake; Shahidi akiri kuruhusu matumizi ya risasi za moto

Spread the love

SHAHIHIDI wa kwanza kwenye kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi wa Chadema, amekiri kuruhusu matumizi ya risasi za moto kwenye maandamano yaliyofanyika na chama hicho tarehe 16 Februari 2018. Anaripoti Faki Sosi…(endelea).

Chadema walifanya maandamana hayo kupinga mawakala wao kutoapishwa kwenye Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Kinondoni. Tukio la maandamano hayo lilifanyika siku moja kabla ya siku ya uchaguzi huo (16 Februari 2018).

Shahidi huyo ambaye ni Ofisa wa Jeshi la Polisi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, alilazimika kuruhusu askari kutumia risasi za moto katika maandamano yaliyofanywa na Chadema.

Viongozi wa Chadema wanaotuhumiwa kwenye keshi hiyo namba 112 ya mwaka 2018 ni;- Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa; Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu wa chama; Salum Mwalim, Naibu Katibu Mkuu Chadema-Zanzibar; John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Chadema-Bara.

Wengini ni Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; Halima Mdee, Mbunge wa Kawe na Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

Leo tarehe 17 kesi hii imeendelea kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo upande wa Jamhuri umefika mahakamani na shahihid mmoja kwa ajili ya kutoa ushahidi.

Faraja Nchimbi, Wakili wa Mkuu Serikali alimuuongoza shahidi aliyejitambulisha mahakamani hapo ambaye ni Mrakibu wa Jeshi la Polisi SSP Gelard Ngichi.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya Wakili wa Serikali Mkuu na shahidi wa upande wa mashtaka;-

Wakili Nchimbi: Mwajiri wako ni nani?

Shahidi: Wizara ya Mambo ya Ndani na kituo changu cha kazi, kwa sasa ni Mkoa wa Polisi wa Kinondoni Kanda ya Dar es salaam.

Wakili Nchimbi:  Hebu tufahamishe, Mkoa wa Polisi wa Kinondoni, wewe upo kama nani?

Shahidi: Ofisa operesheni wa Polisi.

Wakili Nchimbi: Mwaka gani umeajiriwa?

Shahidi: Mwaka 2000.

Wakili Nchimbi: Katika kituo cha kazi mkoa wa Kinondoni, upo kwa muda gani?

Shahidi: Tangu 2017.

Wakili Nchimbi: Umeieleza mahakama kuwa wewe ni Ofisa wa Operesheni wa Mkoa wa Kinondoni, mbali na hapo ulipitia sehemui gani za mafunzo ya polisi?

Shahidi: Nimehudhuria mafunzo ya ukaguzi wa polisi 2002 Chuo cha Polisi cha Dar es Salaam miezi tisa. Nimehudhuria semina mbalimbali za mafunzi ya Jeshi la Polisi.

Wakili Nchimbi: Ifahamishe mahakama ukiwa kama Ofisa wa Oparesheni, ni yapi majukumu yako ya msingi?

Shahidi: Kuhakikisha usalama wa raia na mali zao ndani ya mkoa sambamba na ulinzi katika maeneo yote yenye misongamano mikuba.

Wakili Nchimbi: Misongamano ya kitu gani?

Shahidi: Biashara, benki, biasha za kichumi maeneo yote kuhakikisha kuna usalama sambamba na usalama wa barabarani na askari wa doria.

Kusimamia mikutano mbalimbali ndani ya Mkoa wa Kinondoni na Kanda ya Dar es Salaam, kuhakikisha kuwa inafanyika kwa utaratibu na kuhakikisha usalama.

Wakili Nchimbi: Kama Ofisa wa Operesheni, mwezi Februari mwaka 2018 kulikuwa na tukio gani kuu au shughuli gani za msingi zilifanyika kwenye Mkoa wa Polisi wa Kinondoni?

Shahidi: Pamoja na shughuli za kila siku, kulikuwa kuna shughuli za maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni, tulikuwa tunasimamia kampeni ndani ya jimbo la hilo.

Wakili Nchimbi: Kama ofisa wa operesheni, ulikuwa una nafasi gani kwenye uchaguzi huo?

Shahidi: Nilikuwa  sambamba na kupokea maelekezo ya barua  na ratiba za mikutano ya kampeni kutoka kwa Mkurugenzi wa Kinondoni  na kusimamia ratiba ya kampeni hizo, mwanzo mpaka mwisho ambapo ilikuwa ni saa 12 jioni.

Wakili Nchimbi: Katika usimamizi huo, ulikuwa unahakikisha kuwa, muda fulani kampeni zianze na muda fulani ziishe, ufahamu huo wewe uliupata wapi?

Shahidi: Barua na ratiba zilikuwa zikitoka kwa Mkurugenzi wa Manspaa ya Kinondoni.

Wakili Nchimbi: Kampenzi hizi zilianza lini na hitimisho  lini?

Shahidi: Zilianza mapema Januari na kumalizika tarehe 16 Februari 2018 na uchaguzi ulifanyika terehe 17 Februari 2018.

Wakili Nchimbi: Utaratibu kwa kusimimia kampeni ulikuaje?

Shahidi: Ulisimamiwa na askari wote askari wa ulinzi askari wa barabarani askari, makachelo na kuhakikisha kuwa mambo yanaenda sawa bila kukiukwa sheria za nchi.

Wakili Nchimbi: Kama utakuwa na kumbukumbu ni vyama gani vilishiriki kwenye kampeni hizo?

Shahidi: Vyama kwa mujibu wa Katiba ni pamoja na (Chadema) Chama cha Wananchi  (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM ) pamoja na vyama vingene vilivyokuwa vikiendelea na kampeni.

Wakili Nchimbi: Kwa mujibu wa ratiba mliyopewa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), utaratibu na ratiba ilikuaje?

Wakati huo wakili wa upande wa washtakiwa (utetezi) Peter Kibatala ameinuka na kuileza mahakama kuwa, “Kama shahidi anasoma anatakiwa aombe ruhusa na sisi tuone na wazi kabisa anachosoma”

Wakili Nchimbi: Hakuna sehemu anayosoma

Wakili Nchimbi (anaendelea): Naomba nirejee kwa mujibu  muongozo au  ratiba muliyopewa na NEC utaratibu na ratiba ilikuaje?

Shahidi: Kutokana na ratiba ya mkurugenzi ilikuwa ikionesha kiwanja au eneo mkutano utakapofanyia.

Wakili Nchimbi: Ratiba ya muda ilikuaje?

Shahidi: Ratiba ilikuwa ikionesha kuanzia saa sita au saba mchana lakini muda wa kumaliza saa 12 kamili jioni.

Wakili Nchimbi: Mnamo tarehe 16 Februali 2018  kuazia asubuhi ulikuwa wapi?

Shahidi: Mimi na maofisa wenzangu tulikuwa tumepangiwa kusimamia kampeni za uchaguzi huo, tulikuwa Kituo cha Polisi Osterbay na kufuata maelekezo kutoka kwa Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni, kipindi hiko alikuwa ACP Murilo kuhusiana na utaratibu mzima wa kusimamia kampeni za mwisho za uchaguzi huo.

Wakili Nchimbi: Ni maelekezo gani muliyokuwa mkiyapokea?

Shahidi: Ni kuhakikisha mikutano yote wanapanga askari wa kutosha.

Wakili Nchimbi: Lengo la kuhimiza askari wa kutosha lilikuwa nini?

Wakili Nchimbi: Ilikuwa ni kuhakikisha ulinzi wa mikutano na raia wengine wanaoendelea shughuli nyengine, hasa maeneo ya barabarani ili kuhakikisha mikutano hiyo haingilii shughuli za uchumi hasaa askari wa barabarani askari wa upelelezi askari wa doria kuimarisha ulinzi.

Wakili Nchimbi: Baada ya hapo  nini kilifuatia?

Shahidi: Nilikwenda kwenye mikutano yote, nilianza Makumbusho viwanja vya vegasi kulikuwepo kampenzi za CUF, baadaye Mwananyala kwenye kampeni za Chadema nako mambo yalikuwa shwari, alikuwa SSP Dotto, ndiye alikuwa msimamizi wa askari walikuwa hapo na baadaye nikaenda Viwanja vya Biafra, kulipokuwa kuna Kampeni za CCM lakini baadaye nikiwa Vickoria  nilipata taarifa kutoka kwa SSP Dotto kuwa, kwenye kampeni za Chadema kuna uvunjifu wa amani.

 Wakili Nchimbi: Baada ya hapo.

Shahidi: Nilimueleza SSP Dotto awaonye viongozi hao na waache uchochezi na nia yao ya kuandamana lakini hawakutaka kutii amri hiyo na kuanza safari kutoka viwanja vya Buibui na kuelekea kupitia barabara ya Mwananyamala hadi Kawawa ambapo walikuwa wakielekea Magomeni kwenye ofisi za mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni.

Wakili Nchimbi: Uliwaona hao watu kwa umbali gani?

Shahidi: Mita mia moja wakiwa wanatoka barabara ya kawawa kuelekea Ofisi ya Mkurugenzi wa Manspaa Magomeni.

Wakili Nchimbi: Watu hawa unaweza kuwakadiria walikuwa watu kiasi gani?

Shahidi: Kati ya 600 na kuendelea.

Wakili Nchimbi: Umati huu unaweza kuelezeaje?

Shahidi: Wengi walivaa mavazi ya Chadema na wengine kaki wakiimba nyimbo ‘hatupoi hatutushwi haya twende lazima tufike kwa Mkurugenzi wa Manspaa ya Kinondoni’.

Wakili Nchimbi: Umati huo ulikuwa katika hali gani?

Shahidi: Walikuwa wanajazba huku wamebeba chupa za maji chupa za soda, majani na mawe.

Wakili Nchimbi: Ulichukia hatua gani?.

Shahidi: Nilielekeza vikosi vya doria kuwa viende vikaweke ulinzi kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wakahakikishe hakina mtu yoyote kuingia kwenye ofisi zile za serikali.

Baada kufika na kusogolea kwa karibu wale waandamanaji barabara zote kushoto kulia lakini pia kwenye barabara ya mwendokasi walijaa waandamanaji.

Nilimuelekeza dereva wangu apige honi na awashe king’ola kuwaondoa waandamanaji waliokuwa kwenye barabara ya mwendokasi.

Niliweza kupita barabara ya mwendokasi niliweza kupita  nipofanikiwa kupita katika yao nikatoa Ilani ya kuwa kusanyiko hilo sio halali hivyo watawanyike.

Wakili Nchimbi: Ilani hiyo ilikuaje?

Shahidi: Nilisema “Ilani ilani ilani mimi SSP Gelard Rich kwa jina la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania mkusanyiko huu ambao sio halali uliokusanyika hapa utawanyike mara moja venginevyo nguvu itatumika kuwatanya.
Tamko hilo mara tatu nilitoka kupitia kipaza sauti wakati gari ikitembea kuelekea mbele ya waandamanaji

 Wakili Nchimbi: Waandamanaji waliongozwa na kina nani?

Shahidi: Waandamanaji hawakutii viongozi wakiongozwa na Mbowe na Mwalimu ambaye alikuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Kinondoni na viongozi waliokuwepo hapa mahakamani .

Wakili Nchimbi: Taja majina yao.

Shahidi: Alikuwepo Mwalimu aliyekuwa kwenye gari la wazi Mbowe Heche Mdee Bulaya, Matiko wote walihamasishana twende mbele na hawatubabaishi lakini nilivyofika mbele kabisa mita 50 niliamuru askari wangu na nikatoa tena Ilani kama Nilivyotoa mara ya kwanza lakini waandamanaji hawakutii waliendelea huku wakiturushia mawe chupa za maji huku wakihamasisha kwa nyimbo zao kwamba ‘hatupoi’.

Wakili Nchimbi: Katika kutoa tamko la Ilani hawakutii nitataka unitajie kwa majina na vitu gani walivifanya.

Shahidi: Mgombea ubunge Mwali aliendelea kuhamasisha, Mbowe alikuwa ameshikana mikono na wenzake, Mdee, Mnyika, Heche Msigwa, Bulaya, Matiko na wengine ambao sikuwafahamu majina yao walikuwa wanaimba wanahamasishana.

Wakili Nchimbi: Nini kilichokufanya uwataje kuwa watu hao ni viongozi?.

Shahidi: Mimi nawafahamu ni viongozi wa kitaifa walikuwa kwenye mikutano mbalimbali lakini pia walikuwa ndio viongozi wa maandamano.

Wakili Nchimbi: Ni kitu gani kilichokufanya useme hawa ndio waliokuwa wakiongoza maandamano.

Shahidi: Walikuwa mstari wa mbele walikuwa wakihamasisha ‘haya twende’  huku wafuasi wakirusha chupa na mawe.

Wakili Nchimbi: Nini kitu gani kilikuwezesha ww kupata utambuzi?.

Shahidi: Niliwapita mbele waandamanaji na niliweza kuwaona kwa sura zao na majina yao.
Wakili Nchimbi:Ni muda gani?

Shahidi: Saa kumi na moja na nusu.

Wakili Nchimbi: Tusaidie na sisi tuweze kuwafahamu viongozi walikuwepo kwenye maandamano uende utuomeshe kama hapa Mahakamani?

Shahidi: Waliokuwepo kwenye kizimba.

Shahidi alitoka kwenye kizimba cha kutoa ushahidi na kwenda kwenye kizimba cha watuhimiwa na kuwagusa watuhumiwa kwa kuwagusa na kuwataja ambapo aliishia kwa Heche aliyemtaja kuwa ni Halima Mdee hakuwataja Bulaya, Matiko na Mashinji akarudi.

Wakili Nchimbi: Endelea…

Shahidi: Muitikio ulikuwa ni hafifu waandamanaji hawakusambaratika na wahakutii amri.

Wakili Nchimbi: Nini waandamanaji walifanya.

Shahidi: Waandamanaji waliendelea kuhamashana haya “twende hatupoi.

Wakili Nchimbi: Mawe yalirushwa kuwapokea wapi?.

Shahidi: Mawe yalielekezwa tulipkuwa sisi askari .

Wakili Nchimbi:Wakati hayo unaendelea viongozi wa Chadema walikuwa wapi?.

Shahidi: Walkuwa waliendelea kuhamasisha maandamano…Wakati polisi Wawili walijeruhiwa kwa mawe walianguka chini alikuwa askari PC Fikiri na Rahim

“Nikaamuru kikosi cha bomu kirudi nyuma na kikosi cha Silaha za moto kisonge mbele.”

Wakili Nchimbi: Nini hasa kilikufanya wewe uchukue uamuzi wa kurejesha nyuma kikosi cha mabomu na kusogeza mbele kikosi cha silaha za moto.

Shahidi: Nililazimika kutumia njia ya mwisho ya kutumia silaha za moto kutoka na waandamanaji kutotii ilani tatu.

Wakili Nchimbi: Waandamanaji hawa wengi walikuwa ni raia ni kitu gani kilikufanya uamuru zitumike silaha za moto?

Shahidi: Kwanza mabomu yale hayakuleta mafanikio ya kuzima maandamano yale pili kujeruhiwa kwa askari wangu wawili, tatu wale waandamanaji walisogelea askari wangu ambapo wangeweza kuchukua silaha za askari waliojeruhiwa.

Wakili Nchimbi: Ulitoa maelekezo gani juu ya matumizi ya silaha hizo za moto?

Shahidi: Nilitoa amri ya kupigwa kwa risasi hewani kwa ajili ya kusambaratisha waandamanaji?.

Wakili Nchimbi: Utekelezaji ulikuaje?

Shahidi: Askari walipiga risasi hewani kishindo kilikuwa kikubwa mpaka Mbowe alikimbia, sikuweza kuamini kama Mbowe angeweza kukimbia vile hadi miwani ikadondoka chini.

Wakili Nchimbi: Nini kiliendelea?

Shahidi: Waandamanaji walitawanyika, nikaamuru askari waanze kuwakatamata waandamanaji na kuwakamata watu 43.

Wakili Nchimbi: Watu hao muliwapeleka wapi?

Shahidi: Osterbay kwa ajili ya kuwafungulia kesi.

Wakili Nchimbi: Kuna mambo gani yaliendelea?

Shahidi: Kwa kuwa barabara na gari zote zilisimama, shughuli za biashara zilisimama, gari za kawaida lakini watu waliokuwa wanafanya biashara waliokuwa pembezoni, walikuwa wamekimbia tukatoa maelekezo warejee kwa kuwa, hali ya amani imetulia.

Wakili Nchimbi: Waandamanaji hao walikuwa viwanja vya buibui kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kulikuwa na ulazima gani wewe kuwazuia waandamanaji?

Shahidi:Muda ule Ofisi zilikuwa zimefungwa kwa hiyo hatutegemei mkutano kuandamana .

Wakili Nchimbi: Kulikuwa kuna shida gani watu hao kwenda kwenye Ofisi za Serikali?

Shahidi: Muda huo ni muda wa msongamano mkubwa wa magari. Watu waliohamasishwa huwa wanakuwa na hasira kali chochote kingeweza kutokea wangeweza kuchoma moto Ofisi za Serikali. Ule ulikuwa mkutano wa kufunga kampeni wangetumia barabara ile wangeleta msongamano.

Wakili Nchimbi: Kwani barabara ile ingetumika ingeleta shida gani?

Shahidi: Ile barabara inayotumiwa daladala lakini pia inakwena Hospitali ya Mwananyamala. Makundi ya watumiaji wa barabara hao.  Magari ya Mwendokasi, magari ya wagonjwa kutoka Hospitali ya Mwananyamala na kuelekea Muhimbili.

Wakili Nchimbi: Kuna taarifa gani nyengine juu ya maandamano hayo?

Shahidi: Wahalifu au vibaka waliingia kwenye maduka yaliyopo pembezoni mwa barabara hiyo na kuiba, pia watoto pamoja na wazee kupotea na kukutwa kwenye vituo mbalimbali vya polisi.

Wakili Nchimbi: Hali ya shughuli kwenye barabara ile na wakazi ilikuwaje? .

Shahidi: Shughuli zilisimama , magari yalisimama kupisha maandamano.
Pia kuleta matishio kwa wafanyabiashara wengine walifunga biashara zao wangine waliacha biashara zao wazi wakakimbia kufuatia maandamano hayo.

Wakili Nchimbi: Nini kiliendelea upande wako?.

Shahidi: Niliendelea na majukumu yangu ya kusimamisha ulinzi wa Mkoa mzima.

Wakili Nchimbi: Tupe taarifa ya jumla kuhusiana na majeruhi wengine wowote.

Shahidi: Nikiwa kituoni Osterbay majira saa mbili, tulipata taarifa mtu mmoja amejeruhiwa yupo hospitalini Mwananyala na baadaye tukapokea taarifa amefariki.

Wakili Nchimbi: Alikuwa akifahamika kwa jina gani .

Shahidi: Akwelina.

Itaendelea sehemu ya pili ya mahujiano kati ya upande wa washtakiwa (Wakili Kibatala) na shahidi wa kwanza (SSP Ngichi).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Tanesco yawasha mtambo namba 8 Bwawa Julius Nyerere

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Ramaphosa achaguliwa tena kuwa rais Afrika Kusini

Spread the loveRais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amechaguliwa na wabunge wa...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

error: Content is protected !!