November 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe, wenzake kuanza tena

Spread the love

 

JAJI Mustapha Siyani, kesho Ijumaa tarehe 10 Septemba 2021 ataanza kusikiliza kesi inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Mbali na Mbowe wengine ni – Halfani Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Lingwenya wanaokabiliwa na mashtaka ya ugaidi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo itaanza kesho Ijumaa saa 3:00 asubuhi na tayari wito wa kufika mahakamani hapo umekwisha kutolewa kwa wahusika ikiwemo magereza ili kuwawezesha kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao.

Jaji Siyani ambaye amekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, amepangiwa kusikiliza shauri hilo, baada ya watuhumiwa kumtaka Jaji Elizana Luvanda, kujiondoa kwenye usikilizaji wa kesi yao.

Miongoni mwa madai ambayo watuhumiwa wanaelezwa kutaka kufanya, ni pamoja na kutaka kulipua vituo vya mafuta na mikusanyiko ambayo imekuwa ikiwashirikisha watu wengi na kudhuru viongozi wa serikali akiwemo aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya.

Kwa sasa, Sabaya yuko gerezani jijini Arusha, anakoshikiliwa kwa madai ya wizi wa kutumia silaha na matumizi mabaya ya madaraka. Kwa mujibu wa Jamhuri, matendo yanayodaiwa kupangwa kutekelezwa na Mbowe na wenzake, yalilenga kusababisha taharuki katika jamii.

error: Content is protected !!