November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe: Shahidi wa 7 aelezea Bwire alivyokamatwa

Spread the love

 

ALIYEKUWA Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Wilaya ya Arusha, Inspekta Mahita Omari Mahita, ameanza kutoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashataka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ni katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, iliyopo Mawasiliano jijini Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joackim Tiganga.

Inspekta Mahita ambaye ni shahidi wa saba wa Jamhuri katika kesi hiyo, ameanza kutoa ushahidi wake mahakamani hapo, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, leo Ijumaa, tarehe 5 Novemba 2021.

Akiongozwa na Wakili Hilla, Inspekta Mahita amedai kwa sasa yeye ni Askari Polisi, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, na kwamba kituo chake cha kazi ni mkoani Morogoro.

Alipolizwa awali alikuwa anafanya kazi wapi, Inspekta Mahita alijibu akidai alikuwa anafanya kazi Kituo Kikuu cha Jeshi la Polisi Arusha, akiwa Msaidizi wa Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai Wilaya ya Arusha.

Wakili Hilla alimuuliza nini kilitokea tarehe 4 Agosti 2020, Inspekta Mahita amejibu akidai akiwa ofisini kwake alipigiwa simu na Afande wake ACP Ramadhan Kingai, akimtaka aende ofisini kwake. Alipokwenda afande huyo alimuagiza awatafute askari wawili, ambapo alimtafuta Detective Francis na Koplo Goodluck.

Inspekta Mahita ambaye ni mtoto wa Inspekta Jenerali wa Polisi mstaafu (IGP), Omar Mahita amedai, ACP Kingai aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Arusha, aliwaambia wanatoka kwa ajili ya safari ya kazi.

Inspekta Mahita amedai kuwa, Afande Kingai aliwaambia amepewa maelekezo ya kuunda kikosi maalum, akiwemo yeye, ASP Jumanne, Goodluck, Francis na PC Aziz.

Shahidi huyo amesema, alipoulizwa tarehe 9 Agosti 2020 nini kilitokea, amejibu akidai alipewa taarifa za Bwire “tulizokuwa tumezipata kwamba. Mtuhumiwa alikuwa anatokea Buguruni kwenda maeneo ya Chang’ombe tukaweka mtego.”

Alipoulizwa ni mteo gani, amejibu “tukiweka askari track wa usalama barabarani akalisimamisha basi aina ya costa ambayo mtuhumiwa alikuwa amepanda. Afande Kingai aliniambia nipande kumuangala ndani.”

Inspekta Mahita amedai, alipoingia “nikamkuta kakaa zile siti za kati” kisha amedai akajitambulisha kwamba “naitwa Inspector Mahita na kwamba natokea Arusha na kwamba anashitakiwa kwa makosa ya kutaka kutenda ugaidi.”

Amedai, afande Kingai na yeye akajitambulisha akamuonya na baadaye akaweka mahabusu ya pale pale Chang’ombe na wakati huo ilikuwa saa 4 usiku.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Halfan Hassan Bwire, Adam Ksekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi ina mashtaka sita ya ugaidi, ikiwemo la kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi, linalowakabili washtakiwa wote wanne.

Shtaka la kutoa fedha za kufadhili vitendo hivyo, linamkabili Mbowe. Lingine ni, la kumiliki silaha aina ya bastola kinyume cha sheria, linalomkabili Kasekwa.

Shtaka lingine ni la kukutwa na vifaa vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), linalomkabili Bwire huku lingine ni la kula njama za kutaka kudhuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hahi, Lengai Ole Sabaya.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya tarehe 1 Mei hadi 1 Agosti 2020, katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro, Arusha na Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo na wenzie wanadaiwa kwenda kinyume na Sheria ya Kuzuia Ugaidi na Sheria ya Kuzuia Uhujumu Uchumi.

Hadi sasa upande wa mashtaka umeleta mashahidi saba pamoja vilelezo kumi mahakamani hapo, ambapo miongoni mwa mashahidi hao ni, Mrajisi wa Leseni za Bunduki kutoka Jeshi la Polisi, Kamisheni ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kitengo cha Udhibiti na Usajiliwa Silaha za Kiraia, SSP Sebastian Madembwe.

Wengine ni, Mwanasheria wa Kampuni ya Mawasiliano ya MIC Tanzania Ltd (Kampuni ya Tigo), Fredy Kapala. Anita Varelian, Koplo Hafidhi Abdllah Mohammed, Justine Elia Kaaya na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kinondoni, ACP Ramadhan Kingai.

Askari Polisi, SSP Sebastian Madembwe (46), ambaye ni shahidi wa sita wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake leo Alhamisi, anaendelea kutoa ushahidi sasa hivi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam. Yupo kitengo cha udhibiti na usajili wa silaha

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!