Monday , 5 June 2023
Home Gazeti Tangulizi Kesi ya Mbowe: Shahidi Jamhuri aibuka na Akwelina
Tangulizi

Kesi ya Mbowe: Shahidi Jamhuri aibuka na Akwelina

Spread the love

SHAHIDI wa nane katika kesi ya uchochezi namba 112/2018, inayomkabili Freeman Mbowe na wenzake wanane, ametoa ushahidi wake leo. Anaripoti Faki Sosi…(endelea).

Kwenye kesi hiyo leo tarehe 11 Septemba 2019, shahidi huyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba amesema, baada ya kutokea vurugu kwenye maandamano yalisofanywa na Chadema, alifanikiwa kubaini watu ambao wanaweza kuwa mashahidi kwenye kesi.

Kesi hiyo inamuhusi Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu-Taifa; John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu – Bara na Salumu Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu -Z’Bar.

Wengine ni Ester Matiko Mbunge wa Tarime Mjini; Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

Kwenye kesi hiyo, shahidi wa Jamhuri, Bernard Nyambari aliyekuwa Msaidizi wa Upepeli Mkoa wa Kipolisi Kinondoni amehojiwa na wakili wa utetezi Peter Kibatala kama ifuatavyo;-

 Wakili: Uliweza kumtambua mtu yeyote aliyekuwepo kwenye maandamano?

Shahidi: Natambua baadhi ya watu, nawajua walikuwa mstari wa mbele.

Wakili: Kina nani?

Shahidi: Nakumbuka nilimuona Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe; Katibu wa Chadema, Vicent Mashinji; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, pia nilimuona John Mnyika, Mbunge wa Kibamba,

Wakili: Wako mahakamani?

Shahidi: Wako

Wakili: Umewafahamuje, uliwajuaje?

Shahidi: Nilipata kuwajua kwanza ni watu ambao nilikuwa nawaona mara kwa mara kwa macho na kwenye shughuli za chama.

Wakili: Je, utaweza kuwatambua kuwaonesha mahakama watu hawa?

Shahidi: Ndio, ni miongoni mwa watuhumiwa kwenye kizimba.

Wakili: Mheshimiwa, anaweza kutoka kwenye kizimba kuwaonesha watuhumiwa?

Hakimu: Ndio, ni haki yake kisheria

Shahidi akatoka kuwatambulisha, alianza na Mbowe akafuata Mdee, Mashinji na kumalizia kwa Mnyika.

Wakili: Uliieleza mahakama, ulikwenda pale kama mpelelezi, shughuli zipi ulifanya eneo latukio?

Shahidi: Upelelezi wa shughuli baada ya kuwa maandamano yale yametawanya chini ya operesheni iliyoongozwa na SSP Gerald Ngichi, na hali ilikuwa imetengemaa kiasi fulani, niliweza kubaini watu ambao walikuwa kama mashahidi muhimu katika upande wangu ambao walikuwepo eneo la tukio ambao wanaweza kuwa mashahidi kwenye kesi hiyo….

Wakili: Uliweza kubaini baadhi ya mashahidi wanaofaa kwenye kesi ya maandamano, unaweza kuwakumbuka?

Shahidi: Shahidi mmojawapo Shaban Hassan Abdallah, yeye alikuwa mkazi wa maeneo yale, Anthony Boniface, Daud Kagisa, Daudi Ngoda.

Wakili: Ulimsema kulikuwa askari kama wanaweza kuwa mashahidi, unaweza kuwataja?

Shahidi: Mkuu wa operesheni hiyo Gerald Ngichi, Fikiri, Koplo Rahim hao ni mashahidi waliokuwa kwenye operesheni.

Wakili: Katika upelelezi wako wa awali, ulibaini nini kilikua chanzo cha maandamano?

Shahidi: Chanzo kutokana na upelelezi uliofanyika, unaeleza kwamba chanzo kilikuwa ni hotuba zilizokuwa zimetolewa na viongozi mbalimbali wa Chadema, waliokuwa kwenye uwanja wa Buibui, Mwanaymala katika mkutano wao wa kufunga kampeni za mgombea wa ubunge wa chama chao, jimbo la Kinondoni. Chanzo kilikuwa hotuba zilizotolewa.

Wakili: Unasema uliweza kubaini maamdamano hayo yalisababishwa na mkutano wa kufunga uchaguzi, ulitumia njia zipi za upelelezi au ulipata wapi taarifa kuhusiana na chanzo cha maandamano?

Shahidi: Njia nilizotumia katika kupata majibu ya chanzo cha maamdamano, ilikuwa kuhoji mashahidi mbalimbali ikiwemo raia wa kawaida na askari waliokuwepo kwenye eneo lililokuwa kunafanyika mkutano.

Pia kupitia mahojiano ambayo timu ya upelelezi ilifanya na watuhumiwa ambao wanashtakiwa kubaini uhusika wao katika maandamano hayo.

Lakini pia kupitia taarifa mbalimbali ambazo tumezipata kama timu ya upelelezi tulizozipata kutoka mitandao ya kijamii, mfano blogs kuona speech (maelezo) ambazo zilikiwa posted, zilisaidia katika upelelezi kujua nani alikuwepo kwenye maandamano.

Wakili: Umesema chanzo ni hotuba, kwani hotuba hizo zilihusu nini? zilisababisha nini kwa mujibu wa upelelezi wako?

Shahidi: Kutoknana na upelelezi nilioufanya, nilibanini chanzo ilikuwa hotuba ambapo katika hotuba zao, walitumia kauli za kuhamasisha watu waandamane kutoka eneo la mkutano kwenda ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.

Wakili: Umesema kwamba viongozi gani hasa waliotoa hotuba?

Shahidi: Viongozi wa Chadema nawazungumzia waliokuweko kizimbani.

Wakili: Unaweza kuielezea mahakama ,hotuba zilikuwaje kutokana na upelelzi uliofanya?

Shahidi: Hotuba ambazo zilibeba maneno yanayotengeneza chuki  kwa wananchi dhidi ya serikali na vyombo vya dola, na kuwafanya wale waliokuwa wakihutubiwa kuwa na hisia hasi na hata kuwapelekea waweze kuandamana.

Wakili: Kwa mujibu wa upelelezi ulioufanya, maandamano ambayo umeelezea hapa mahakamani yalikuwa na madhara gani?

Shahidi: Kwa mujibu wa upelelezi niliofanya na mahojiano na  mashahidi, maandamano kwanza yalitengeneza hofu kubwa kwa wananchi wa eneo ambapo watu walipita walishindwa kufanya shughuli zao wakihofia usalama wao.

Maduka yalifungwa kutokana na hofu iliyokuwepo. Maandamano pia yalipita barabarani bila utaratibu ambao ungeruhusu magari kupita kwa urahisi na kusababisha usumbufu kwa watumiaji barabara na magari.

Wakili: Kuna hatahari nyingine yoyote iliyotokana na hayo maandamano kwa mujibu wa upelelezi wako?

Shahidi: Maandamano hayo yalipelekea baadhi ya watu kuumia kwa kurushiwa na kupigwa mawe, miongoni mwa watu walioumia ni askari wawili. Waliumia baada ya kupigwa mawe na waandamanaji.

Wakili: Unawafahamu kina nani?

Shahidi: Anaitwa CP Fikiri, Kituo cha Polisi Oysterbay na Koplo Hakimu ambaye anafanya kazi Oysterbay.

Wakili: Taarifa gani nyingine ulipokea?

Shahidi: Kwenye matokeo ya upelelezi yalionesha kutokana na vurugu za maandamano, kuna tukio la mtu mmoja wa jinsia ya kike kufariki.

Wakili: Kwa mujibu wa upelelezi wako, mtu huyo alifariki akiwa wapi?

Shahidi: Matokeo ya upelelezi yanaonesha kwamba, mtu huyo alifariki katika Hospitali ya Mwananyamala.

Wakili: Unasema alifariki akiwa Mwananyamala, mtu huyo anaitwa nani?

Shahidi: Ni binti, jina lake alikuwa anaitwa Akwelina Akwilini Maftaha, alikuwa ni mwanafunzi.

Wakili: Alifariki kwa sababu ya nini?

Shahidi: Uchunguzi uliofanyika na matokeo yake yalibainisha alifariki kutokana na majeraha aliyopata ya risasi.

Wakili: Kwa mujibu wa upelelezi uliofanya, alipigwa risasi akiwa wapi?

Shahidi: Uchunguzi umebaini kwamba Akwilina alipigwa risasi akiwa eneo la Mkwajuni ambapo ilikuwa center (kituo) ya maandamano.

Wakili: Unasema alikiwa Mkwajuni akifanya nini?.

Shahidi: Uchunguzi unaonesha kwamba, marehemu alikuwa anasafiri kupitia daladala lililokuwa anatokea njia ya Magomeni kwenda Moroko, alijeruhiwa na risasi alipokuwa kwenye siti ya gari.

Wakili: Umesema kuna askari waliumia? walihudumiwaje nani aliwahudumia?

Shahidi: Askari walioumia walitibiwa katika Hospitali ya Polisi ya Kilwa Road.

Wakili: Kwa mujibu wa upelelezi wako, uliweza kubaini waliumia nini?

Shahidi: Wakati wa upelelezi niliweza kuwahoji na kuwaona wakiwa hospitali, mmoja ambaye ni Fikiri alikuwa na jeraha kichwani mwingine Koplo Rahim alijeruhiwa shingoni pamoja ma mkononi.

Wakili: Baada ya kukamilisha upelelezo wako, ulifanya nini?

Shahidi: Baada ya mimi na timu yangu kumaliza upelelezi kwa kufanya mambo yote muhimu kuhoji watuhumiwa kwa nyakati tofauti baada ya kukamilisha yote hayo, nilifungua jalada na kupeleka ofisi ya taifa ya mashtaka ili waweze kusoma na kuona mashtaka gani watuhumiwa wanaweza kufunguliwa.

Wakili: Umeeleza katika upelelezi wako ulipata taarifa ya kifo cha Akwilina, ulihusikaje katika upelelezi wa kifo?

Shahidi: Katika upelelezi wa tukio hili kwa ujumla, kulikuwa na timu mbili, kuna timu ambayo niliiongoza yenyewe ilijikita.

Wakili: Ulihusikaje?

Shahidi: Lilipelelezwa, najua mtu alikufa katika maandamano.

Kuna timu ambayo ilikuwa inafanya upelelezi wa tukio la kifo cha Akwilina.

Kwenye kesi hiyo, upande wa Jamhuri unawakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi; Dk. Zainab Mango; Wakili Wankyo na Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori

Upande wa utetezi umeongozwa na Prof. Abdallah Safari, Peter Kibatala, Dickson Matata, Hekima Mwasipu na Ekson Kilatu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

MichezoTangulizi

Yanga malizeni ugomvi na Fei Toto – Rais Samia

Spread the love  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kifo cha mwanafunzi UDOM: Tume yamsafisha naibu waziri

Spread the loveTUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini (THBUB),...

Habari MchanganyikoTangulizi

Bosi NIC apandishwa kizimbani, akabiliwa na mashitaka 365

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar: Bakharesa hajavamia shamba letu

Spread the love  IKULU Visiwani Zanzibar, imeeleza kuwa eneo la kiwanda cha...

error: Content is protected !!