Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe: Shahidi augua, ashindwa kutoa ushahidi
Habari za Siasa

Kesi ya Mbowe: Shahidi augua, ashindwa kutoa ushahidi

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, imeahirisha kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiki wa Chadema na wenzake, Freeman Mbowe na wenzake, hadi kesho Jumanne, tarehe 17 Januari 2022, baada ya shahidi wa Jamhuri, Inspekta Innocent Ndowo, kuzidiwa na maumivu ya kichwa akiwa kizimbani. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Tukio hilo limetokea leo Jumatatu, tarehe 17 Januari 2022, kwenye Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, wakati Inspekta Ndowo akitoa ushahidi wake, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, katika mahakama hiyo, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo yenye mashtaka sita ya ugaidi, ni waliokuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Jaji Tiganga ameahirisha kesi hiyo hadi kesho, ambapo ameamrisha upande wa mashtaka kuleta shahidi mwingine kesho, kama hali yake kiafya itakuwa haijatengamaa.

“Tunahairisha kama upande wa mashtaka ulivyoomba na maneno ya shahidi, tunaahirisha mpaka kesho saa 3.00 asubuhi, ambapo shauri linaendelea kusikilizwa na shahidi naamini kesho utapata nafuu kwa ajili ya kuja kutoa ushahidi. Kama inaonekana shahidi hali yake haijatengamaa, walete shahidi mwingine,” amesema Jaji Tiganga.

Jaji Joachim Tiganga

Wakati huo huo, Jaji Tiganga amemuomba Askofu Emmaus Mwamakula, aliyekuwepo mahakamani hapo, amuombee ili apone haraka.

“Tunaye Askofu, baada ya hapa naamini Askofu katika karma yake nyingine ya uponyaji, ataanzisha maombi. Kwa hiyo tunaahirisha hadi kesho, tukiamini kwamba shahidi atakuwa sawa, atapata matibabu leo na mimi nitakuombea shahidi,” amesema Jaji Tiganga.

Jaji Tiganga ameahirisha kesi hiyo baada ya Wakili Hilla kuomba ahirisho hadi shahidi huyo atakapopona.

“Ni rai ya upande wa mashtaka kwamba, nachelea kusema lini sababu sijui ataimarika lini. Naomba ahirisho mpaka afya ya shahidi itakapokuwa imeamirka,” amedai Wakili Hilla.

Wakili Hilla alitoa ombi hilo, baada ya Inspekta Ndowo kushindwa kuendelea kutoa ushahidi mahakamani hapo, ambapo sauti yake ilikuwa ya chini mno, hali iliyopelekea Jaji Tiganga amtake aongeze sauti ili watu waliokuwepo wasikie.

Baada ya Jaji Tiganga kutoa amri hiyo, Inspekta Ndowo alijibu akidai kichwa kinamgonga sana, ndiyo maana sauti yake ilikiwa chini.

“Mheshimiwa Jaji toka asubuhi kichwa kinanigonga ndiyo maana sauti yangu ilikuwa chini, muda unavyozidi kwenda kinazidi kunigonga,” amedai Inspekta Ndowo.

Shahidi huyo anatarajiwa kuendelea kutoa ushahidi kesho kama hali yake kiafya itaimarika.

Katika ushahidi wake, Inspekta Ndowo amedai alizifanyia uchunguzi simu nane za mkononi aina ya Tecno (4), Itel (2), Sumsung (1) na Bund (1), tarehe 9 Julai 2021.

Inspekta Ndowo amedai kuwa, vielelezo hivyo alivipokea tarehe 13 Agosti 2020, kutoka kwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), na kwamba alipangwa kuvifanyia uchunguzi katika maeneo matatu, ambayo ni mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii ya Telegram, WhatsApp, Facebook na ujumbe mfupi wa maneno.

Eneo la pili ni taarifa za usajili na miamala ya fedha na la mwisho ikiwa ni la mawasiliano ya kupiga na kupigwa za namba za simu zilizokutwa katika simu hizo nane.

Inspekta Ndowo amedai kuwa, uchunguzi wake ulibaini simu nne kati ya nane zilikuwa na shahidi na nne zilizobakia hazikuwa na ushahidi.

Alidai, baada ya kumaliza uchunguzi huo, alikabidhi ripoti za uchunguzi, kwa Askari Polisi aliyemtaja kwa jina la Inspekta Swilla.

Shahidi huyo wa 10 wa Jamhuri, amedai kuwa, tarehe 1 Julai 2021, aliandika barua kwenda kampuni za mawasiliano ya simu za Airtel na Tigo, kuomba taarifa za usajili na miamala ya simu, za namba hizo, ambapo maombi yake yalijibiwa tarehe 2 Julai 2021.

Miongoni mwa wamiliki wa laini hizo za simu ni za Mbowe na Hassan.

Inspekta Ndowo ametoa ushahidi wake baada ya Meneja wa Kitengo cha Sheria cha Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania PLC, Gladys Fimbari, aliyetoa mahakamani hapo taarifa za usajili na miamala ya fedha ya baadhi ya namba hizo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!