November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe: Mkuu wa upelelezi Arumeru anaeleza alichoshuhudia

Spread the love

 

AFISA wa Polisi nchini Tanzania, Jumanne Malangahe, ameanza kutoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi, yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Ni leo Jumatatu, tarehe 8 Novemba 2021, kwenye Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, iliyopo Mawasiliano jijini Dar es Salaam.

Shahidi huyo wa nane wa jamhuri, ameanza kutoa ushahidi wake mbele ya Jaji Joackim Tiganga, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando.

Akiongozwa na Wakili Kidando, Malangahe amedai mahakamani hapo yeye ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Wakili Kidando: Ulipokuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru, nani alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Arusha (RCO)?

Shahidi: RCO alikuwa ACP Ramadhan Kingai.

Wakili Kidando: Elelezea tarehe 4 Agosti 2020 ulikuwa wapi katika majukumi yako ya kazi?

Shahidi: Tarehe 4 Agosti 2020 nilikiwa katika kituo changu cha kazi Wilaya ya Arumeru, ofisini kwangu. Majira ya jioni RCO Kingai akanitaarifu nijiandae kwa safari kuna kazi ya kwenda kufanya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Wakili Kidando: Nini kilifuata?

Shahidi: Nilijiandaa na muda mfupi saa moja kasoro aliwasili ofisini kwangu na kumpokea, alikuja na askari watano akiwemo yeye mwenyewe.

Wakili Kidando: Alikueleza nini?

Shahidi: Alituambia kuna kikundi cha kihalifu ambacho kinapanga kufanya matukio ya kihalifu hapa nchini ambayo kulipua vituo vya mafuta, kuanzisha vurugu na maandamano.

Pia, kukata miti au magogi na kuyaweka kwenye barabara ili kuzuia magari kupita na kuwadhuru viongozi wa Serikali akiwemo Sabaya.

Alisema baadhi ya wahalifu walikuwa wamewasili Moshi, na kwamba kikundi hicho kinaratibiwa na Mwenywkiti wa Chadema, Mbowe. Baada ya kutoa maelekezo hayo tulianza safari ya kuelekea Moshi.

Shahidi huyo kwa sasa anaendelea kutoa ushahidi.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Halfan Hassan Bwire, Adam Ksekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Hadi sasa upande wa mashtaka umeleta mashahidi nane pamoja vilelezo kumi mahakamani hapo, ambapo miongoni mwa mashahidi hao ni, Mrajisi wa Leseni za Bunduki kutoka Jeshi la Polisi, Kamisheni ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kitengo cha Udhibiti na Usajiliwa Silaha za Kiraia, SSP Sebastian Madembwe.

Wengine ni, Mwanasheria wa Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo, Fredy Kapala, mfanyabiashara wa mbege Rau Madukani, Moshi- Anita Varelian na Koplo Hafidhi Abdallah Mohammed.

Pia, wamo Justine Elia Kaaya, aliyekuwa msaidizi wa mkuu wa wilaya wa zamani wa Hai, Lengai Ole Sabaya  na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kinondoni, ACP Ramadhan Kingai. 

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!