Tuesday , 19 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe: Mahakama yatoa maagizo kwa shahidi wa Jamhuri, mawakili
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Mbowe: Mahakama yatoa maagizo kwa shahidi wa Jamhuri, mawakili

Spread the love

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, imemuamuru Luteni Denis Urio, shahidi wa 12 Jamhuri, ajibu maswali ya upande wa utetezi, huku akiwaagiza mawakili kutomuuliza maswali yasiyohusiana na kesi iliyopo mahakamani hapo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ni katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, waliokuwa makomando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Maagizo hayo yametolewa leo Alhamisi, tarehe 27 Januari 2022  na Jaji Joachim Tiganga, akitoa uamuzi mdogo wa pingamizi la Jamhuri dhidi ya ombi la upande wa utetezi, lililoitaka mahakama imuamuru Luteni Urio, kujibu maswali aliyosita kuyajibu.

Wakili wa Utetezi, Nashon Nkungu, alimuuliza maswali  Luteni Urio kuhusu baadhi ya taratibu za JWTZ, lakini alisita kuyajibu akidai ni kutokana na sababu za kiusalama kwa kuwa kesi hiyo inafuatiliwa na watu wengi ndani na nje ya nchi.  Pamoja na kutii kiapo chake cha jeshi.

Miongoni mwa maswali aliyosita kuyajibu ni lile alilotakiwa kutaja idadi ya vituo vya kijeshi vinavyofundisha mafunzo maalumu ya ukomando, na alipata  kiwango gani cha  mafunzo hayo.

Jaji Tiganga alimuamuru Luteni Urio ajibu maswali yanayomhusu na kwamba yasiyomhusu anaweza kusita kuyajibu.

“Nafahamu kwamba yawezekana kweli iko siri shahidi hawezi kuzitoa za JWTZ, mahakama kwa kufahamu hivyo naelekeza mawakili wanapomuuliza maswali wamuulize maswali yanayomlenga shahidi. Ukweli kwamba analotolea ushahidi ni taarifa rasmi aliyoitolea taarifa na hakusema alitoa taarifa JWTZ,” amesema Jaji Tiganga.

Jaji Tiganga amesema “Naelekeza kwamba, swali uliloulizwa linakuhusu wewe binafsi kuhusu mafunzo na ukiulizwa yanayohusu aina ya mafunzo uliyofunzwa unaweza kusita, sababu halihusiani na shauri liloko katika mahakama hii.”

 Jaji Tiganga alilitupa pingamizi la Jamhuri lililotaka mahakama hiyo isimuamuru shahidi kujibu maswali ya utetezi, akisema Sheria ya Ushahidi, kifungu cha 141, 155 na 158, vinaipa mamlaka mahakama kumlazimisha shahidi kujibu maswali  yanayohusiana na kesi iliyoko mahakamani.

Baada ya Jaji Tiganga kutoa uamuzi huo mdogo, Luteni Urio anaendelea kutoa ushahidi wake alioanza kuutoa jana Jumatano, ambapo anaulizwa maswali ya dodoso na Wakili Nkungu.

Katika ushahidi wake, Luteni Urio anadai katika nyakati tofauti  Julai 2020 Mbowe alimtumia kiasi cha 699,000 kwa njia ya mtandao, kwa ajili ya kumtafutia waliokuwa makomando wa JWTZ, kwa ajili ya kutekeleza harakati za chama chake kuchukua dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

Luteni Urio anadai kuwa, Mbowe alipanga kuchukua dola kwa gharama yoyote, ikiwemo kupanga njama za kudhuru viongozi wa Serikali wanaoonekana kuwa kikwazo kwa vyama vya upinzani, kuanzisha maandamano, kuchoma vituo vya mafuta na maene yenye mikusanyiko ya watu.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita ya ugaidi, ikiwemo linalomkabili peke yake la kutoa Sh. 699,000 kwa ajili ya kufadhili vitendo hivyo.

Huku mengine yakiwa ni kupanga njama za kudhuru viongozi, kuratibu maandamano na kushiriki vikao vya kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi. Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai hadi Agosti 2020. Katika mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Zanzibar mbioni kuanza uchimbaji mafuta na gesi baharini

Spread the loveSERIKALI ya Zanzibar, imekamilisha mchakato wa uchimbaji wa mafuta na...

Habari za Siasa

Wizara ya afya yataja mafanikio 10 miaka mitatu Samia madarakani

Spread the loveWIZARA ya Afya imetaja mafanikio 10 iliyoyapata ndani ya miaka...

Habari za Siasa

Mbozi walilia kuwa manispaa, majimbo 3

Spread the loveHALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imeeleza dhamira yake...

Habari za Siasa

Wabunge waitaka TPDC kuongeza kasi ya kuunganisha wateja gesi asilia

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini...

error: Content is protected !!