January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe: Mahakama yagoma kupokea vielelezo vya Jamhuri

Spread the love

 

MAHAKAMA KUU, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam, imekataa kupokea mali zinazodaiwa kuwa za mshtakiwa wa kwanza, Halfan Bwire Hassan, kama kilelezo cha Jamhuri, kwenye kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Mahakaka hiyo imetoa uamuzi huo leo Jumatatu, tarehe 10 Januari 2022 mbele ya Jaji Joachim Tiganga, akitoa uamuzi mdogo wa mapingamizi ya upande wa utetezi dhidi ya upokelewaji wake.

Miongoni mwa mali zilizokataliwa kupokewa, ni baadhi ya vifaa na sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), zinazodaiwa kukamatwa nyumbani kwa Hassan, maeneo ya Yombo Kilakala, Dar es Salaam, tarehe 10 Agosti 2020, baada ya shahidi aliyeomba kuzitoa mahakamani hapo, askari polisi, Jumanne Malangahe, kufanya upekuzi.

Jaji Tiganga amesema mahakama hiyo imekataa kupokea mali hizo kama vilelezo vya jamhuri, kwa kuwa hazina uwezo kutokana kwamba, uchukuliwaji wake haukufuata sheria.

Ni baada ya Jaji Tiganga kukubali mapingamizi mawili, kati ya mapingamizi kadhaa yaliyowekwa na upande wa utetezi, kupinga upokelewaji wake.

Mapingamizi hayo mawili yaliyopokelewa na mahakama hiyo ni, lililodai shahidi hakuleta mahakamani risiti inayothibitisha mali zilizokamatwa, huku lingine likidai alishindwa kuweka alama zinazothibitisha uhalali wake, mbele ya mashahidi.

“Mahakama hii imeona katika hoja zote zilizoletwa na utetezi mengine yalishindwa kwa kuwa hayakuwa na mashiko kasoro mawili yaliyozungumzia ku-lebel vidhibiti na lile la hati ya ukamataji kutokuwa risiti.”

“ Mahakama inaona mapingamizi haya yana faida, yana athiri competence (uwezo) ya kielezo na kutofuata masharti hayo ya utaratibu wa uchukuaji mali. Mahakama inakataa upokelewaji wa vilelezo hivi kwa sababu nilizozitoa,” amesema Jaji Tiganga.

Jaji Tiganga amesema, kitendo cha shahidi huyo kuleta hati ya ukamataji mali peke yake, bila ya risiti kuna athiri uwezo wa upokelewaji wa mali hizo.

“Kushindwa kutoa risiti ni fatal na kinaathiri competence ya kielelezo na upokelewaji wake. Katika hali ya kawaida mahakama hii ilitakiwa iishie hapa,” amesema Jaji Tiganga.

Jaji Tiganga alitupa maombi ya jamhuri ya kupokea mali hizo kwa kuwa shahidi alileta hati ya ukamataji mali, akisema hati hiyo ni tofauti na risiti, licha ya kwamba vyote vina maudhui yanayofanana.

“Utolewaji wa hati ya ukamataji mali na risiti ni vitu viwili tofauti, mahakama inaona kutotolewa risti ni tatizo kwa maana hiyo ni vitu viwili tofauti ingawa content zake zinafanana,” amesema Jaji Tiganga.

Jaji Tiganga amesema, mali hizo hazikuwa na uwezo wa kupokelewa kwa kuwa uchukuliwaji wake ulikiuka sheria kutokana na alama zake kuwekwa bila ya uwepo wa mashahidi.

“Mark (alama) hiyo ilivyowekwa imekiuka masharti ya lazima yaliyopo katika kifungu cha 229 cha Muongozo wa Jeshi la Polisi (PGO), kwa sababu hiyo hii inaathiri uwezo wa kielelezo na upokelewaji wa kielelzo hicho,” amesema Jaji Tiganga.

Baada ya kutoa maamuzi hayo na vilelezo hivyo kupokelewa mahakamani, Jaji Tiganga aliamuru SP Malangahe aendelee kutoa ushahidi wake.

SP Malangahe anaendelea kutoa ushahidi wake, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando.

Mbali na Mbowe na Hassan, washtakiwa wengine katika kesi hiyo, iliyoko katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, ni Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online, MwanaHALISI TV na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!