Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe: Fuatilia RPC Kingai alivyohitimisha ushahidi wake
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Mbowe: Fuatilia RPC Kingai alivyohitimisha ushahidi wake

Kamanda wa Polisi wa Kinondoni (RPC), Ramadhan Kingai
Spread the love

 

KAMANDA wa Polisi Kinondoni, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ramadhan Kingai amehitimisha kutoa ushahidi wake katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzania nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kingai, aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Arusha, amemaliza kutoa ushahidi wake Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam leo Jumatano, tarehe 27 Oktoba 2021.

Mbele ya Jaji Joackim Tiganga, Kingai ameulizwa maswali ya mawakili wa Serikali, baada ya jana kuwa ameulizwa na mawakili wa utetezi, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya.

Mara baada ya kumaliza, Jamhuri inakusudia kumleta shahidi mwingine kwenye kesi hiyo.

Hivi ndivyo Kingai alivyofunga ushahidi wake;

Wakili wa Serikali: Jana Mtobesya alikuuliza wakati gani jalada la uchunguzi lilifunguliwa na wakati gani jalada la kesi lilifunguliwa?

Kingai: Jalada la uchunguzi tulikuwa tumefungua baada ya kukutana na Luteni Denis Urio katika ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai.

Wakili wa Serikali: Na jalada la kesi?

Kingai: Nilifungua baada ya mimi kupata taarifa kuwa vijana walipokuwa wanatafutwa na Luteni Urio kwa amri ya Mbowe ndipo tulifungua jalada.

Kibatala: Objection. Swali lilikuwa kwamba suala la kumtafuta Moses Lijenje. Je ulimuhoji mshitakiwa wa pili?

Jaji Tiganga: Wakili wa Serikali?

Wakili wa Serikali: Mheshimiwa sijauliza alichofanya cross-examination yeye, nipo kwa Mtobesya.

Jaji Tiganga: Uliza tena.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa kuhusu kuwa na taarifa za Moses Lijenje wakati unamhoji mshitakiwa wa pili. Je, ulijua taarifa hizo kabla au baada?

Jaji: kibatala umesikia swali?

Kibatala: Nimesikia lakini kaniondoa mimi sasa ni eneo la Mtobesya.

Kingai: Nilipata taarifa kuwa Freeman Mbowe alikuwa anatafuta kundi la wahalifu.

Wakili Mtobesya: Hakufika huko. Tt’s something a new alisema alikuwa anatafuta vijana.

Jaji: Ndiyo na mimi nimesikia hivyo jana ulisema alikuwa anatafuta vijana siyo kundi la wahalifu.

Kingai: Ndiyo nilipata taarifa kuwa Freeman Mbowe alikuwa anatafuta kundi la vijana walioachishwa kazi jeshini kwa dhumuni la kudhuru viongozi wa Serikali na pia mpango wa maandamano ya kushinikiza viongozi yasiyokuwa na kikomo na kwamba lengo la kufanya hivyo ni nchi isitawalike na ionekane imefeli kuelekea uchaguzi mkuu.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa hapa jana kuwa wakati mshitakiwa wa pili kama ulikuwa umempa onyo mshitakiwa wa pili kuhusiana na ukamataji. Wewe ukasema ulikuwa umeshampa haki zake. Haki zake zipi?

Kingai: Haki zake ni pamoja na kumfahamisha na kosa alilokuwa anashitakiwa nalo na kwamba halazimishwi Kusema lolote ila jambo analozungumza linaweza kutumika kama ushahidi dhidi yake mahakamani.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa kwamba matukio ya kula njama yalifanyika kati ya Mei 10, 2020 na tarehe tano Agosti mwka 2020 lakini katika ushahidi wako ulisema kula njama huku kulifanyika tarehe 25 Julai 2020 hadi tarehe moja Agosti 2020 huko Aishi Hotel. Unasemeje juu ya ushahidi wako kupingana na hati ya mashitaka?

Kingai: Naomba kuona hiyo hati ya mashitaka.

Jaji: Utetezi mapingamizi juu ya hilo?

Mtobesya: Hapana. Hakuna pingamizi. Apewe tu.

Kingai: Mie naona hakuna utofauti bado. Ipo in between bado.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa swali kuhusiana na maelezo ya mshitakiwa wa kwanza kwamba yaliandikwa Chang’ombe ukasema ndiyo. Ni kweli? Na maelezo mshitakiwa wa pili na watatu yalichukuliwa Central Dar es Salaam. Eleza kwanini uliamuru maelezo ya mtuhumiwa wa kwanza yachukuliwe Chang’ombe.

Kingai: Kwanza Chang’ombe ni Dar es Salaam. Pili huwezi kufananisha na Moshi. Halafu nilikuwa pia naangalia masaa manne.

Mtobesya: Objection! Mheshimiwa Jaji wamuelekeze shahidi wao vizuri. Hatutaki kila saa kusimamasimama.

Jaji: Jamhuri?

Wakili wa Serikali: Shahidi eleza sababu tu kwanini uliamuru maelezo ya mshitakiwa wa kwanza yachukuliwe Chang’ombe.

Kingai: Baada ya mshitakiwa kudanganya kuhusu makazi yake.

Mtobesya: Objection Mheshimiwa Jaji. Hayo ya kudanganya ni mapya. Sheria ya ushahidi ipo wazi. Haupaswi kuongea mambo mapya.

Jaji: Nafikiri shida ipo kwenye neno kudanganywa. Hata mimi sikusikia neno “Kudanganywa”. Ondoa hilo neno uendelee.

Wakili wa Serikali: Elezea kwanini uliamuru maelezo ya mshitakiwa wa kwanza yachukuliwe Chang’ombe.

Kingai: Kwanza ni kituo cha karibu cha Polisi lakini pia tulikuwa bado hatujajua makazi yake.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa kwamba mshitakiwa wa pili uliomuonya kuhusu kula njama ya kutenda matendo ya ugaidi. Kwanini hukumuonya na makosa mengine?

Kibatala: Objection! Hayo niliuliza mimi sikumuuliza kwanini hukumuonya kila shitaka. Nilikuwa nauliza kwa kila kosa. Kama mnataka twende hivyo tutaomba kumuhoji tena.

Jaji: Unasemaje Wakili wa Serikali?

Wakili wa Serikali: Nitarudia swali Mheshimiwa.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa swali kuhusiana na kuamini na kutoamini hasa kwenye sababu ya wakili.

Shahidi: Nilikuwa siamini kwamba Mkuu wa Wilaya anaweza kushusha bendera lakini pia ndiyo iwe sababu ya kumdhuru kiongozi wa Serikali. Lakini statement_niliamini sababu alitoa yeye.

Wakili wa Serikali: Mheshimiwa Jaji naomba kupatiwa kielelezo P1.

Wakili wa Serikali: Shahidi chukua karatasi hii (anampatia). Nitakuuliza maeneo ambayo ulihojiwa na mawakili wa utetezi.

Wakili wa Serikali: Tafuta eneo ulikohojiwa kuhusiana na kumfikisha mheshimiwa Mikocheni. Ukipata nitakuuliza swali.

Kingai anatafuta wakati mahakama iko kimya kumsubiri.

Kingai hajaona anachokitafuta hadi wakili wa Serikali anaingilia na kumuuliza:

Wakili wa Serikali: Baada ya kufika Dar es Salaam na kumfikisha Mheshimiwa Mikocheni, hujaona?

Jaji: Labda uchukue kwanza wewe usome halafu umuonyeshe.

Wakili wa Serikali: Kama hawatokuwa na pingamizi.

Kibatala: Hatuna [pingamizi] Mheshimiwa Jaji.

Wakili wa Serikali: Soma hapa.

Kingai: Baada ya kufika Dar es Salaam na kumfikisha Mheshimiwa Mikocheni mimi na Mohammed tulipewa laki mbili mbili baada ya kesho yake kuwa annakuja Lissu na kumpokea.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa kuwa huyo mheshimiwa ni nani ukasema. Sasa ieleze Mahakama huyo mheshimiwa ni nani.

Mtosebya: Objection! Mheshimiwa Jaji. Kifungu cha 61 cha Sheria ya Ushahidi kinasema nyaraka isitafsiriwe bali nyaraka ijieleze yenyewe. Hapo shahidi anaulizwa tafsiri.

Wakili wa Serikali: Naona hiyo objection haina mashiko kwa sababu tutakuwa hatuna cha kufanya.

Jaji: Nafikiri Mtobesya hoja yako inahusu thamani ya nyaraka. Sasa Mahakama itaangalia hicho anachokisema kipo kwenye nyaraka?

Mtosebya: Sawa Mheshimiwa Jaji.

Kingai: Ni Mheshimiwa Mbowe. Kwa sababu mheshimiwa aliyetajwa kwenye statement hii ni Mheshimiwa Mbowe na Mbowe mwenyewe anaishi Mikocheni.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa pia kuhusiana na kupewa laki mbili mimi na Mohammed. Huyu Mohamed ni nani?

Kingai: Ni Ling’wenya kwa sababu huko juu tulikuwa tunazungumzia Mohamed Ling’wenya na statement hii alikuwa anatoa mwenyewe.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa swali kama kwenye statement hiyo kama alivyoelezea yeye kama mshitakiwa wa pili kama alimfuatilia Sabaya katika maeneo aliyokuwa akienda Arusha. Uliulizwa swali wewe ukasema hapana. Sasa nitakupeleka kwenye statement halafu utafafanua.

Mtobesya: Objection! Samahani Mheshimiwa Jaji. Labda kwa maelekezo yako nitakubali maelekezo ya Mahakama. Anachoulizwa shahidi alishajibu kuwa hakuwa Arusha. Anaulizwaje jambo hilo hilo tena?

Jaji: Nafikiri ngoja tusubiri swali lake.

Kibatala: Jaji naomba umuangalie shahidi vizuri. Kuna zoezi linaendelea pale na dawati la jirani. Tuna- suspect anapewa information na watu wa pembeni yake.

Wakili wa Serikali: Kwa utaratibu wa Mahakama Kibatala anapaswa aongee kwa ushahidi kama kuna kitu kweli umekiona kitolee ushahidi, siyo kuja na neno una- suspect. Nani kafanya na kitu gani kimefanywa?

Jaji: Kibatala ulikusudia nimuonye, na tunachukulia una taarifa za kiintelijensia kwamba tumuonye shahidi kwa intelijensia yako?

Kibatala: Mimi nimesema Mahakama imuangalie.

Jaji: Basi kwa sababu mimi sijaona naomba upande wa Jamhuri waendelee kuuliza maswali.

Kingai: Katika kufuatilia nyendo za Sabaya tulienda Club Kokoriko lakini hatukumpata Mheshimiwa Sabaya siku hiyo.

Wakili wa Serikali: Eleza sasa kwenye statement hii kama mshitakiwa alifika Club Kokoriko.

Kingai: Alifika.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa pia swali kuhusiana na kama kuna sehemu yoyote kama mshitakiwa wa pili amechukuliwa finger prints katika statement hii. Ni kwanini katika statement hii hakuna maelezo ya kuchukuliwa finger print?

Kingai: Mimi kama mchunguzi nilishaona hakuna haja ya kuchukua finger prints. Haihitaji la kuchukua finger prints.

Ilikuwa ni baada ya kumpekua mshtakiwa namba moja na baada kukuta kijitabu ikabidi sasa kuchukua finger prints. Wakati nachukua maelezo mshitakiwa wa pili ilikuwa tarehe 7 Agosti mwaka 2020 kabla ya kupata kijitabu hicho.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa kama ulichukua sampuli za finger prints za pistol inavyodaiwa kukutwa na mshitakiwa wa pili. Sasa wewe kama mchunguzi ni kwanini hukuchukua finger prints na sampuli za DNA?

Shahidi: Mimi sikuona haja ya kuchukua finger prints kwa sababu mshitakiwa tulikuwa naye. Tunafanya finger prints kama mshitakiwa amevunja na hayupo. Sisi hatukua na hitaji hilo kama alivyouliza wakili.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa swali kuwa kwa kipindi chote baada ya kupata nia ya uhalifu, kama ulimtaarifu kiongozi aliyelengwa Ole Sabaya kama ulimpatia, ukasema hukumpatia na wala Kamati ya Ulinzi ya mkoa wa Kilimanjaro. Ni kwanini sasa?

Kingai: Tulikuwa na uhakika wa taarifa zetu. Hatukuwa na sababu za kuwaambia watu wengine kwa kuwa tunge- create pressure.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa wakati mtuhumiwa wa kwanza anakamatwa palikuwa na askari jeshi na ukasema hakukuwa na askari jeshi.

Kingai: Hapakuwa na askari jeshi kwa sababu mimi ndiyo nilikuwa Arresting Officer na nikisaidiwa na Inspector Mahita pamoja na ASP Mahita.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa kuhusiana na maandamano ukasema ni sheria inaruhusu lakini kwa kufuata taratibu. Eleza una maana gani?

Kingai: Ni kweli Sheria inaruhusu maandamano lakini kuna sheria zingine pia zinaweka taratibu kuwa kabla ya Kufanya maandamano awe amepata kibali.

Wakili wa Serikali: Kibali gani?

Kingai: Cha Polisi.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa swali kuhusiana na Sheria ya Ushahidi wakati wa onyo kuwa section one na two hukuweka, ukasema hiyo ni curable. Ulikuwa unamaanisha nini?

Kingai: Haiwezi kuathiri maelezo ya kuonywa.

Wakili wa Serikali: Uliulizwa swali kuhusiana na mtu wa pili katika maelezo yake kuwa mtu mmoja anaitwa Kakobe. Ukasema ukabaini kuwa mtu anaitwa Kakobe ndiyo Moses Lijenje. Eleza ni wakati gani ulibaini?

Kingai: Wakati tunawakamata watuhumiwa walikuwa wawili lakini tulikuwa tuna taarifa wapo watatu. Tuliwauliza yupo wapi mwenzenu? Wakasema anaitwa Kakobe ambaye ndiyo Lijenje.

Wakili wa Serikali: Mheshimiwa Jaji tunaomba tukomee hapa.

Jaji: Kama tumekukwaza, kwa niaba ya Mahakama naomba radhi. Naomba radhi kwa niaba ya utetezi na ninakushukuru kwa ushahidi wako.

Wakili wa Serikali: Mheshimiwa Jaji tuna shahidi mwingine lakini kabla ya kuendelea naye tunaomba ahirisho fupi. Ikiwezekana tuweze ku- resume saa tano na nusu.

Jaji: Upande wa Utetezi?

Kibatala: Mheshimiwa tumekubaliana kuwa hatuna pingamizi lolote.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!