December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe: Askari Msemwa aeleza alivyowapokea Kasekwa, Ling’wenya

Spread the love

 

ASKARI Mpelelezi (Detective Constable-DC), Ricardo Msemwa, shahidi wa Jamhuri, katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mohammed Abdillah Ling’wenya, ameanza kutoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano jijini Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ni katika kesi ya uhujumu uchumi, yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili Ling’wenya na wenzake watatu akiwemo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Shahidi huyo ameanza kutoa ushahidi wake mahakamani hapo leo Ijumaa, tarehe12 Novemba 2021, kuanzia saa 6:40 mchana akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, mbele ya Jaji Joackim Tiganga.

Kesi hiyo iliyoahirishwa jana Alhamisi hadi leo saa 4:00 asubuhi, imechelewa kuanza zaidi ya saa mbili hakukuwa na taarifa zozote licha ya washtakiwa kufikishwa kabla ya saa nne.

Akiongozwa na Wakili Hilla, DC Msemwa amedai, 2020 alikuwa anafanya kazi Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, Kitengo cha General Duty (Majukumu yote), ambacho kinahusika na kazi zote ikiwemo kulinda maeneo mbalimbali kama benki, kufanya msako na kufanya kazi katika chumba cha mashtaka.

DC Msemwa ameieleza mahakama hiyo, tangu Januari 2021, anafanya kazi katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, mkoani Dar es Salaam.

Katika ushahidi wake, DC Msemwa alieleza namna alivyompokea katika chumba cha mashtaka cha Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam, Ling’wenya, alfajiri ya tarehe 7 Agosti 2020, akitokea Kituo Kikuu cha Polisi cha Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Ni baada ya kukamatwa tarehe 5 Agosti 2020 kwa kosa la kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi.

DC Msemwa alidai mahakama, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Arusha, ACP Ramadhan Kingai, akiwa na wenzake watatu akiwemo, Mkuu wa Upelelezi wilayani Arumeru, Jumanne Malangahe, waliwafikisha watuhumiwa wawii kituoni hapo, ambao ni Ling’wenya na Adam Kasekwa.

Mahojiano ya Wakili Hilla na DC Msemwa yalikuwa kama ifuatavyo;

Wakili Hilla: Tarehe 7 Agosti 2020 ulikuwa wapi?

Shahidi: Mnamo tarehe 7 Agosti 2020, nilikuwa kazini Central kama Askari wa zamu ndani ya chumba cha mashtaka.

Wakili Hilla: Ukikuwa zamu ya muda gani?

Shahidi: CRO (chumba cha mashtaka), tulikuwa tunaingia zamu ya saa 12. Kati ya majira ya saa 11.45 kwa maana ya saa 12 kasorobo tayari nilikuwa kazini.

Wakili Hilla: Ukiwa askari wa zamu siku hiyo majukumu yako yalikuwa yapi?

Shahidi: Sikuwa peke yangu tulikuwa askari wengi, Incharge hutoa majukumu.

Wakili Hilla: Wewe majukumu yako siku hiyo ulipangiwa yapi?

Shahidi: Uwepo wa askari hao, incharge alitoa majukumu mimi nilipangiwa ku-deal na mahabusu, kwa maana ya kuwapokea mahabusu na kuwatoa.

Wakili Hilla: Uieleze mahakama baada ya kuingia kazini siku hiyo unakumbuka walifika kina nani?

Shahidi: Baada ya kuwa tumeingia kazini shifti ya asubuhi watu wa kwanza kufika walikuwa Kingai, afande Jumanne na wengine wawili wakiwa wameshika bunduki wakiwa na watuhumiwa wawili.

Wakili Hilla: Hao Kingai na Jumanne ni akina nani hasa?

Shshidi: Kwa kipindi hiko walichofika kwangu, nafahamu Kingai alikwua RCO Arusha na Jumamne nafahamu alikuwa afande kutoka makao makuu, hicho ndicho nilichokuwa nafahamu mimi kwa wakati huo.

Wakili Hilla: Nini kilifanyika kwanza walifika eneo gani?

Shahidi: Walifika Central Ilala, chumba cha kupokea ile charge room, wakiwa na watuhumiwa moja kwa moja.

Baada ya kufika afande Jumanne aliulizia nani anahusika na mahabusu, nikamwambia mimi, akaniamhia kuna watuhumiwa kutoka Moshi refence namba yao hii hapa, wanatuhumiwa kwa makosa ya kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi.

Wakiwa hawajaondoka, tulifanya utaratibu wa kawaida kwa maana ya upekuzi na kuwasave watuhumiwa kwenye kitabu cha mahabusu.

Wakili Hilla: Baada ya kuwapekuwa na kuwaweka mahabusu, uliwafanya nini?

Shahidi: Kitu cha kwanza nilimpekua mtuhumiwa wa kwanza

Wakili Hilla: Kilichofuata ni nini?

Shahidi: Kilichofuata ni kuwachukua watuhumiwa na kuwapeleka mahabusu ya Central palepale

Wakili Hilla: Kingai na wenzake baada ya kuwapeleka mahabausu wewe ulifanya nini?

Shahidi: Baada ya kuwapekuwa watuhumiwa, nilijaza taarifa zao kweneye kitabu cha mahabusu, ikiwemo majina yao, hali yao kiafya, kosa wanalotuhumiwa nalo.

Nikawaingiza mahabusu, baada ya kuhakikisha watuhumiwa wameondoka wao waliondoka.

Wakili Hilla: Watuhumiwa walikuwa kina nani?

Shahidi: Walikuwa wawili kwa majina walikuwa Mohamed Abdillah Ling’wenya na Adam Kasekwa, ndio niliwaandika kwenye kitabu cha mahabusu

Wakili Hilla: Baada ya kuwa umewawaweka mahabusu, wale watuhumiwa umewaingiza mahabusu, kitu gani kiliendelea kuhusiana na watuhumiwa?

Shahidi: Baada ya kwamba nimewaweka mahabusu, haikuchukua muda mrefu Afande Kingai alikuja kuchukua mtuhumiwa kwa ajili ya kumhoji.

Kingai alimchukua mtuhumiwa anaitwa Kasekwa alisema nitolee Kasekwa kwa ajili ya kwenda kumuandika maelezo.

Baada ya kuchukua mtuhumiwa, kuandika maelezo haikuchukua muda mrefu afande Jumanne alifika kwa ajili ya kumchukua mtuhumiwa mwingine kuandika maelezo.

Wakili Hilla: Kama unakumbuka Kingai alikwenda naye wapi?

Shahidi: Alivyomchukua Kasekwa mimi mwenyewe nilimsindikiza naye kupandisha juu kule kwa RCO.

Wakili Hilla: Huyu mwingine aliyechukuliwa na Jumanne alimchukua kwa madhumuni gani na wakaelekea wapi?

Shahidi: Alisema nitolee mtuhumiwa nikaandike maelezo, akamchukua kule ofisini kuna chumba akaondoka naye.

Wakili Hilla: Ieleze mahakama baada ya watuhumiwa hawa kuwa wametolewa ni lini walirejea?

Shahidi: Walirejea siku ile ile

Wakili Hilla: Ieleze mahakama watuhumiwa tangu wanaingia, walivyotolewa na walivyorejeshwa hali zao kiafya zilikuwaje?

Shahidi: Sababu mtuhumiwa ametoka tuliandika kwamba ametoka na akirudishwa inabidi umrudishe upya kwa kufanya taratibu za mwanzo, utamuuliza majina yake, hali yake ya kiafya, utaingiza na namba ya kosa na kosa lenyewe analotuhumiwa.

Nilimpekua baada ya hapo nikawafikisha mahabusu kwa ajili ya hifahdi.

Upande wa utetezi uliyapinga maelezo ya onyo yanayodaiwa kuwa ya Ling’wenya, ukidai kuwa si halali kisheria, kwa kuwa hayakutolewa na mshtakiwa huyo na kwamba alilazimishwa kusaini karatasi yenye maelezo ambayo hakuyasoma.

Shahidi huyo wa jamhuri ameanza kutoa ushahidi wake, baada ya shahidi wa kwanza, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Arumeru mkoani Arusha, Mrakibu wa Polisi (SP), Jumanne Malangahe, kutoa ushahidi wake.

Katika ushahidi wake, SP Jumanne alidai, alichukua maelezo hayo ya onyo kwa hiari ya mshtakiwa pamoja na kumpatia haki zake zote kisheria, tarehe 7 Agosti 2020, kwenye Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam, akitokea Kituo cha Polisi cha Kati Moshi, mkoani Kilimanjaro, baada ya kukamatwa kwa kosa la kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi, tarehe 5 Agosti mwaka jana.

Kesi inaendelea. Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!