January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe: Airtel yauza Sh.500 laini ya simu ya mshtakiwa

Spread the love

 

UPANDE wa utetezi, katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, wamemhoji shahidi wa Jamhuri, Gladys Fimbari kwa nini wameiuza kwa mtu mwingine namba ya simu ya mshtakiwa wa kwanza, Halfan Bwire Hassan na fedha hiyo hawakumpa mwenyewe. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Fimbari ambaye ni Meneja wa Kitengo cha Sheria cha Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania ameulizwa swali hilo leo Ijumaa, tarehe 14 Januari 2022 na Wakili John Mallya.

Ilikuwa ni baada ya jana Alhamisi, Fimbari ambaye ni shahidi wa tisa wa Jamhuri kuelezea miamala ambayo Mbowe aliifanya wakati akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Esther Martin kutoa ushahidi wake mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Wakili Mallya alimhoji Fimbari kwamba endapo Bwire atataka kuitumia namba hiyo kujitetea katika mashtaka yanayowakabili mahakamani hapo, ataipataje wakati imeuzwa kwa mtu anayeidaiwa kuitwa Godson Mnuru.

Wakili Mallya aliuliza swali hilo baada ya Fimbari kuwasilisha mahakamani hapo taarifa za miamala ya fedha na usajili wa namba za simu za 0782237913, inayodaiwa kuwa ya Hassan, 0787555200 inayodaiwa kuwa ya Dennis Urio na 0784779944, inayodaiwa kuwa ya Freeman Mbowe.

Fimbari alidai taarifa hizo alizoziwasilisha mahakamani, alizifanyia kazi tarehe 2 Julai 2021, baada ya Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi cha Jeshi la Polisi, kuiomba kampuni ya Airtel kutoa taarifa za usajili na mimala ya namba hizo kwa ajili ya uchunguzi.

Mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo;

Mallya: Hivi laini ya Airtel inauzwa Sh. ngapi?

Shahidi: Sh.500

Mallya: Kuna regulation ya 2020 inayo-regulate namna ya ku-hanlde sim card, unaifahamu?

Shahidi: Naifahamu

Mallya: Ulipokea P16 ambayo barua ya Polisi kusema wanaomba uchunguzi kweye nyaraka fulani fulani, ulishuhudia wanafanya upelelezi serious wa kesi fulani au walifanya masihala masihala?

Shahidi: Mimi nafanyia kazi kilicholetwa kwangu

Mallya: Uliambiwa namba zinafanyiwa uchunguzi?

Shahidi: Ni kweli

Mallya: Kwa kutumia regulation hizo, unafahamu hiyo namba inaonekana kama ya Bwire, sasa hivi wameiuza kwa mtu anaitwa Godson Mnuru, ni sahihi?

Shahidi: Sifahamu

Mallya: Sasa hivi haisomi Halfan Bwire, umeletewa barua kuambiwa inachunguzwa halafu namba mmeuza kwa Sh.500, Bwire akitaka kupata namba yake aji-defence ataitoa wapi?

Shahidi: Sikuulizwa swali kama hilo

Mallya: Kwenye namba ya Bwire wakati mnafanya uchunguzi kulikuwa na pesa zake kwenye laini mliyouza, zile pesa mlizipekea wapi?

Shahidi: Kwa utaratibu namba yoyote inapokaa zaidi ya miezi mitatu bila kutumika, fedha tumeiweka kwenye collection account.

Mallya: Shahidi umesema zile pesa ziliwekwa kwenye collection ya Airtel?

Shahidi: Nimeeleza ni utaratibu

Mallya: Hii sheria ninayosema laini ikikaa 90 days iwe deactivated, si ina taratibu zake ukipewa notice hii namba tunaichunguza?

Shahidi: Barua inasema inaomba taarifa za namba

Mallya: Hakuna mahali inasema tunachunguza uchunguzi wa kisayansi?

Shahidi: Inasema ili kukamilisha uchunguzi naomba kukamilisha taarifa zifuatavyo

Mallya: Huyu mshtakiwa akitaka ajitetee ni sahihi amnyang’anye Godson Mnuru aliyeinunua? Siku moja atakuwa na wajibu kupitia namba hiyo hiyo, namba mmeiuza hata 500 yake hamjapa?

Shahidi: Hizo taarifa zipo

Mbali ya Mbowe na Bwire kwenye kesi hiyo, wengine ni Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya wanaotuhumiwa kupanga vitendo vya kigaidi.

Shahidi huyo amemaliza kutoa ushahidi wake na kesi imeahirishwa hadi tarehe 17 Januari 2022 na watuhumiwa wote wanne wamerejeshwa rumande.

error: Content is protected !!