July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Katiba yanguruma kama simba

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Goerge Masaju akifafanua jambo.

Spread the love

KESI ya madai inayohoji uhalali wa Bunge Maalum la Katiba kubomoa Rasimu ya Pili ya Katiba; kunyoa ibara na kuingiza sura mpya, itaingia katika hatua muhimu 15 Septemba.

Ni siku hiyo, jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo Na. 28 ya 2014, watatoa uamuzi wa ama kuruhusu au kutoruhusu mfungua madai kusikilizwa maombi yake ya kusitishwa Bunge Maalum la Katiba.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hali Halisi Polishers Limited na mhariri mtendaji wa MwanaHALISI, Saed Kubenea.

Katika shauri hilo, Kubenea aomba mahakama kutoa amri ya muda ya kusitisha shughuli za Bunge Maalum wakati mahakama ikisikiliza kesi ya msingi.

Majaji Augustine Mwarija, Dk. Fauz Twaib na Aloysius Mujuluzi, wanatarajiwa kutoa uamuzi kama pingamizi lililowekwa kuhusu ombi hilo na mlalamikiwa, lina maana au halina. Katika shauri hili, Kubenea anamshitaki mwanasheria mkuu wa serikali.

Pingamizi lilisikilizwa juzi Ijumaa kwa zaidi ya saa sita. Upande wa mlalamikiwa uliwasilisha hoja tatu kuishawishi mahakama itupilie mbali ombi la kusitishwa kwa muda kwa Bunge la Katiba.

Kubena, amefungua kesi hiyo Na. 28, chini ya hati ya dharura, pamoja na ombi Na. 29/2014, linaloomba kusitishwa kwa bunge. Anawakilishwa na wakili wa kujitegemea, Peter Kibatala.

Ndani ya chumba cha mahakama, Kubenea alionekana mchangamfu; aliyevaa ujasiri katika kufungua kesi inayovuta umma wa Watanzania kipindi ambacho Bunge Maalum linalalamikiwa kuvuruga rasimu ya katiba mpya iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju ambaye aliwasilisha maelezo ya moja ya hoja tatu za kupinga ombi hilo, aliiomba mahakama kutupa ombi la mdai kwa kile alichoita, “kesi hiyo haina msingi kisheria.”

Masaju alisaidiwa na mawakili wawili wa serikali, Gabriel Malata na Edson Mweyunge. Malata alitoa hoja kuwa ombi la muombaji limewasilishwa kinyume cha sheria kwa kutotajwa kifungu chochote cha sheria kinachoipa mahakama mamlaka ya kusitisha shughuli za bunge hilo.

Alidai kuwa kifungu cha 2(2) kilichotumika kufungua kesi, hakielezi kitu kama hicho na kwa hivyo ombi la muombaji, halina msingi wa kisheria.

Hoja ya pili iliyotolewa na Masaju, ilikuwa ni kwamba hakuna uhalali wa muombaji kutaka mahakama isitishe Bunge Maalum kwa kuwa, bunge lenyewe ni suala la kikatiba.

Masaju aliieleza mahakama kwamba ombo hilo linakasirisha, linachokoza na halina maana.

Wakili Mwiyunge katika hoja yake alieleza kuwa hati ya kiapo cha muombaji katika ombi hilo, imejaa upungufu wa kisheria. Alidai, muombaji hakueleza kama ameridhika na taarifa alizosema kwenye kiapo chake kuwa amesikia za kuhusu yanayoendelea bungeni. Alirejea kauli za wenzake kutaka ombi hilo litupwe.

Hata hivyo, Wakili Kibatala alitetea msingi wa ombi akieleza kuwa kifungu alichotumia kimetumika na majaji wawili katika maombi tofauti.

Ametaja kesi ya kwanza kutumika kifungu hicho, ni kesi ya Zitto Zuberi Kabwe dhidi ya Katibu Mkuu wa Chadema, ambako alitaka Kamati Kuu ya chama hicho kuzuiwa kujadili uanachama wake. Shauri hili lilitolewa uamuzi na Jaji Utamwa.

Kesi nyingine ambayo wakili Kibatala aliiwasilisha nbungeni, ni ombi la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) dhidi ya IPTL na wenzake lililoamuliwa na Jaji Robert Makaramba.

Katika kesi ya msingi ambayo pia itatajwa 15 Septemba, Kubenea anaomba Mahakama Kuu itoe tafsiri ya kisheria ya mamlaka ya Bunge Maalum na pia iseme kama bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha rasimu ya katiba kutoka ile halisi iliyowasilishwa bungeni 18 Machi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba.

Bunge Maalum la Katiba limeundwa chini ya Kifungu cha 25(1) na (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Na. 83 ya mwaka 2011 ambayo pia ndiyo iliwezesha kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aloiongoza Jaji Warioba.

error: Content is protected !!